Tanzania yasitisha somo la Historia ya ‘kumtukuza Magufuli’

Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako

VITABU vipya vya “Historia ya Tanzania” vilivyokuwa vimechapwa kwa agizo la Rais John Magufuli havitatumika tena. Badala yake, vitaandaliwa vingine – endapo kutakuwa na umuhimu huo, SAUTI KUBWA imeelezwa.

Somo hilo lilipangwa lifundishwe kwa wanafunzi wa shule za awali hadi sekondari za juu kuanzia Julai Mosi mwaka huu. Kwa taarifa zilizopo, sasa itabidi somo hilo lisubiri au halitakuwepo kabisa kutokana na udhaifu uliogundulika.

Taarifa ambazo zimeifikia SAUTI KUBWA zinaeleza kwamba kusitishwa kwa somo hilo kunatokana na kile kinachoelezwa kuwa ni mkanganyiko wa “usahihi wa historia” iliyokuwa imelengwa na imechapishwa kwenye vitabu hivyo vya kiada.

Sehemu kubwa ya historia hiyo ilikuwa imeandikwa kama propaganda za kusifu watawala na kubeba taarifa nyingine zisizokuwa sahihi, hasa katika kuelezea mwenendo wa kuimarika kwa uchumi na maendeleo ya siasa nchini Tanzania.

Chanzo chetu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) kimeiambia SAUTI KUBWA: “Sehemu kubwa ya vitabu vilivyochapishwa imebeba historia potofu; inasifia mmoja wa marais wa Tanzania kuwa ndiye kinara wa mabadiliko ya maendeleo yanayoonekana sasa, hatua ambayo haina usahihi.” TEA ndiyo waandaaji wa mitaala ya elimu nchini Tanzania.

Alisema vitabu hivyo vilisheheni sifa kwa Rais Magufuli, huku viongozi wengine waliomtangulia wakitajwa kwa mbali kama sehemu ndogo au “wakibebeshwa lawama” kwa baadhi ya madhila yaliyoonekaa kushamiri Tanzania.

Miezi michache kabla ya kifo chake, Rais Magufuli ndiye alitamka hadharani, na kaagiza waziri wa elimu, kwamba kuna ulazima wa kubadili mitaala na kuandika upya vitabu vya somo la Historia na kwamba lianze kufundishwa haraka tangu madarasa ya awali. Magufuli aliaga dunia Machi 17, 2021.

Ofisa mwandamizi wa TEA ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema kuwa uamuzi wa kusitisha vitabu hivyo umefikiwa baada ya serikali kubaini kwamba somo hilo litakuwa limejaa hadaa za kisiasa, jambo ambalo ni upotoshaji wa historia halisi ya Tanzania. 

Rais Magufuli alitaka somo hilo liwe maalumu, akidai kwamba Watanzania wengi hawajui historia ya nchi yao. Hata hivyo, historia ya Tanzania, miaka nenda rudi, imekuwa ikifundishwa shuleni katika somo la historia na kama sehemu ya somo la Uraia.

Kauli ya Rais Magufuli ilitolewa Desemba 9 mwaka jana wakati akiapisha mawaziri wapya Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, akamwagiza Prof. Joyce Ndalichako kuhakikisha somo la Historia ya Tanzania linaanza kufundishwa upya na haraka – na kwamba liwe ni somo la lazima kwa kila mwanafunzi.

Februari 12, 2021 Prof. Ndalichako alisema wizara hiyo ilikuwa imeanza utekelezaji wa maagizo ya Rais Magufuli mara moja kwa kuandaa muhtasari ambao ungewezesha somo hilo kuanza kufundishwa kutoka madarasa ya chini hadi kidato cha sita.

Alisema kwamba somo hilo lingesaidia “kujenga moyo wa uzalendo” kwa kuwafanya Watanzania kuifahamu nchi yao, kuithamini na kuipenda na kujenga moyo wa kulinda rasilimali; akasema maandalizi – ikiwa ni pamoja na kuandika vitabu hivyo – yalikuwa yanaendelea vema.  

SAUTI KUBWA inazo taarifa kuwa kazi ya kuandaa na  hatimaye kuchapishwa vitabu vya somo hilo ilikamilika mwezi Aprili, 2021 na zilikuwa zikisubiriwa fedha za kuanza kuvisambaza shuleni.

Wadau wengi wa elimu walilaumu serikali kwa kuanzisha somo hilo kana kwamba ni jipya huku wanafunzi wamekuwa wakilisoma miaka yote kuanzia madarasa ya chini.

Akitoa maoni yake, mhadhiri mstaafu wa vyuo vikuu, Dk. Lenny Kasoga, amesema kuwepo kwa “somo la Historia linalojitegemea” ni mzigo mwingine kwa serikali na matumizi mabaya ya raslimali fedha. 

“Wanafunzi wamekuwa wakisoma historia ya nchi yetu. Sasa kuwaongezea somo jingine ni kuwapa shida watoto wetu. Kwanza tayari wana masomo mengi sana,” aliongeza msomi huyo wa siasa ya uchumi.

Akiwa mjini Morogoro Februari 12, 2021, Rais Magufuli alikumbusha tena umuhimu wa somo hilo na kutishia kumfukuza kazi Prof. Ndalichako kwa kuendelea kuchelewa kulianzisha.

Juni 26, 2021, Prof. Ndalichako alitangaza kusitishwa kwa mchakato wa kuanza kufundishwa Historia ya Tanzania, akiueleza umma kwamba kuna “mambo yanaboreshwa kwanza.”

Wachambuzi wa siasa na wanazuoni walitoa maoni na kutoona mantiki ya kuanzishwa kwa somo jipya, na sasa wanabashiri kwamba huenda somo hilo halitakuwepo tena kwa kuwa si kipaumbele cha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alirithi madaraka kutoka kwa Magufuli.

Mwalimu Phoebe Makelemo, ambaye sasa ni mshauri wa masuala ya elimu katika balozi kadhaa nchini ni mmoja wa wataalamu wa elimu ambaye alipinga kuanzishwa kwa somo hilo, alihoji umuhimu wa somo hilo sasa na uharaka wake huku akitahadharisha kupotoshwa au kuandaliwa kwa mtaala ambao hauna vigezo ili tu kukidhi matakwa ya rais.

Mwalimu huyo alisema katika kuandaa mitaala yapo mambo ya msingi kuzingatia, na kwamba ana shaka endapo yalifuatwa.

Mambo hayo ni pamoja na kufanya maandalizi ya ufundishaji ni kuchambua muhtasari wa somo na vitabu vya kiada kwa somo husika ili kubaini mada kuu na mada ndogo zilizopo na kuzipangilia kimantiki kufuatana na mazingira ya ufundishaji unaoukusudia, uandaaji wa azimio la kazi, uandaaji wa somo na zana pamoja na mbinu za kufundishia.

“Shaka ni kwamba mambo haya hayakuzingatiwa kwa kuwa kulikuwa tu na msukumo wa rais, na kwamba muda haukuweza kutosha kuwa na mitaala yenye maana pana na kubeba dhana iliyokusudiwa,” alisema na kuongeza: “Hawa walichofanya ni kazi ya zima moto.”

Like
1