Diallo aitibua CCM kuhusu ushindi wa uchaguzi mkuu 2015, afya ya mgombea urais

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza nchini Tanzania, Dk. Anthony Ngw’andu Diallo, amekosoa vikali utendaji wa kiongozi wa nchi hiyo aliyepita, hayati John Magufuli, kwa sababu ya kukiuka misingi ya utawala bora, kukosa uungwana na kuongoza kwa ubabe.

Dk. Diallo pia ameweka wazi kwamba chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM)- katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kilikuwa na kila dalili za kushindwa, hivyo wakaamua kutumia “mbinu” za ziada ili kuweza kuingia madarakani.

Katika mahojiano maalum kwenye kipindi cha The Big Agenda kinachorushwa na kituo cha televisheni cha StarTV Ijumaa – Julai 9, 2021, Dk. Diallo alisema wazi kwamba kwa kipindi cha miaka mitano; 2015-2020, Watanzania wengi waliishi kwa hofu kutokana na kuwa utawala wa kibabe usiofuata sheria na kusigina Katiba.

“Kwa kipindi hicho, tumepita katika kiza kifupi, kila mtu hakuwa na hakika kesho ataamka salama, kwa kuwa tulikuwa na utawala wenye kutumia zaidi ubabe na kuacha uugwana uliozoeleka Tanzania,” alisema.

Alisema baada ya kifo cha Magufuli, hivi sasa watu wengi wana “raha mioyoni,” kwa kuwa hakuna mtu akisikia watu wanagonga mlango kwake usiku anataharuki kama ilivyokuwa enzi za utawala wa hayati Magufuli

Dk. Diallo pia alidokeza kuwepo kwa mfumo mzuri wa kufuatilia kwa karibu historia za viogozi wa juu kabla ya kuchaguiwa au kuteuliwa ili kuepusha nchi kuwa na viongozi wenye kichaa.

“Nadhani tuwe waangalifu tu katika kuchagua. Lazima kuwepo na fuatiliaji mahsusi, huko nyuma tulishachagua watu walishakwenda hospitali, kwenye hospitali za vichaa, sasa mtu ana historia ya kuwa na jalada la gonjwa wa akili Hospitali ya Mirembe, halafu mnamwachia achukue nchi?” Alishangaa Dialo. 

Mirembe ni hospitali maalum kwa magonjwa ya akili iliyoko Dodoma.

Siku moja baada ya mahojiano haya kurushwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Kenani Kihongosi, alijitokeza kumshamblia Dk. Diallo kwamba kwanini ayaseme hayo sasa wakati Magufuli hayupo?

Kenani alisema ni vyema viongozi wote wa CCM kuwa na nidhamu na kuonyesha wanaheshimu wenzao hata kama wametangulia mbele ya haki.

Akizungumza na SAUTI KUBWA, Dk. Azavery Lwaitama alisema ni vyema taasisi za nchi, hasa za usalama kfuatilia kwa ukaribu tabia, mwenendo na maisha ya kila anayetaka kuwa kiongozi wa juu ili kuepusha nchi na “majanga.”

Dk. Lwaitama, mhadhiri mstaafu, alisema Tanzania katika kiindi cha miaka mitano iliyopita itakuwa imejifunza kitu kukana na utawala wa Rais Magufuli, kwani kiongozi huyo hakutaka kufuata Katiba wala kusikiliza ushauri wa watu wengine.

Wakati wa utawala wake, Magufuli aliwahi kutamka hadharani kwamba uamuzi wake, kwa kiasi kikubwa, haitabiriki kwa sababu hutegemea siku hiyo ameamkaje.

Akizungumzia namna CCM ilivyokuwa na hofu ya kushindwa uchaguzi mkuu, Diallo ambaye aliwahi kuwa mbunge na naibu waziri wa maji na baadaye utalii, alisema kulikuwa na kila dalili ya chama tawala kushindwa

“Mwaka 2015 vyombo vyote vya Sahara Media Group (StarTV na Radio Free Afrika) tuliamua kuweka nguvu nyingi sana kutokana na ukweli kwamba CCM ilionekana kushindwa, na tulipata shida zaidi na kila mahali vyombo vyetu havikuruhusiwa kuonekana, hadi tulipofanya utaratibu wa kuweka vijana ili vionekane na kusaidia ushidi wa mgombea wetu,” Aliongeza.

Dk. Diallo pia alisema kwamba wakati wa utawala wa Magfuli, vingozi wa chama waliwekwa pembeni kiasi kwamba baadhi yao walikuwa wakisukumwa na vyombo vya usalama kumsogela anapokuwa kwenye ziara.

“Vingozi wa chama tuliwekwa pembeni, tulikuwa hatualikwi kwenye ziara za kiserikali, na hata kwenye misafara, magari yetu yalikuwa yanapangwa mwishoni, jambo ambalo halikuwa sawa,” alisema.

Utawala wa Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano, ulijaa tuhuma nyingi za kuonea, kuteka na hata kuua wapinzani na watu waliokuwa wakipinga namna alivyokuwa akiendesha nchi.

Baadhi ya tuhuma hizo sasa zinaibuka na kuwekwa wazi kupitia vyombo vya habari ambavyo ama vilifungwa au kuzuiwa kufanya kazi huku wahariri na wamiliki wake wakitishwa, kufunguliwa kesi za kubambika za jinai.

Anthony Diallo
Like