Kabudi, Biswalo tumbo joto sakata la fedha zilizotoroshewa China

SAKATA la fedha zilizotoroshewa China ambazo Rais Samia Suluhu Hassan alidokeza kuwa “zilipigwa” baada ya vigogo kuzichukua kwa watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi kama sharti la kuwafutia kesi, limewatia matatani vigogo wawili wanaodaiwa kuhusika na upigaji huo.

Wahusika wakuu ni Profesa Palamagamba Kabudi (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika awamu ya tano wakati sakata hilo lilipotokea), na Jaji Biswalo Mganga (ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Mashitaka).

Taarifa ambazo SAUTI KUBWA inaendelea kuzifuatilia zinasema kuwa wiki iliyopita kikosi maalumu cha Usalama wa Taifa kiliwatia nguvuni Prof. Kabudi na Jaji Biswalo, kila mmoja kwa wakati wake, kikawahoji juu ya wizi huo.

Prof. Kabudi aliwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa kwa siku nne. Vyanzo vyetu vinasema, ”alivurugwa kabisa, jasho lilimtoka mfululizo, akaomba maji ya kunywa, na katikati ya mahojiano alizimia mara kadhaa.”

Kabudi amekuwa anafanya jitihada za kumtafuta wakili ambaye ni rafiki yake wa zamani, Dk. Ringo Tenga ili amsaidie kwa kumpa msaada wa kisheria, hasa utetezi.

Ingawa Dk. Tenga alikuwa ameonyesha huruma na nia ya kutaka kumsaidia, taarifa zinadai kuwa wanafamilia wake walimuonya na kumkumbusha kuwa Prof. Kabudi na Rais John Magufuli ndio walimsababishia madhila na kumweka ndani (Dk. Tenga) kwa mashitaka ya uonevu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, utetezi wa Prof. Kabudi ni kwamba yeye alipokuwa waziri katika serikali ya Magufuli alikuwa hawezi kumkatalia lolote. Amenukuliwa akisema, “yule alikuwa amiri jeshi mkuu. Nisingeweza kumkatalia.”

Taarifa kuhusu hali ya Jaji Biswalo hazikuwa wazi hadi tunachapisha habari hii, lakini wiki mbili zilizopita alikuwa chini ya ulinzi wa kikosi cha Usalama wa Taifa akihojiwa kuhusu wizi huo.

Biswalo, kwa mujibu wa nafasi yake wakati ule, ndiye alikuwa anaamuru nani awekwe ndani, nani aondolewe, kwa vigezo gani na kwa kulipa kiasi gani cha fedha.

Amekuwa analaumiwa na baadhi ya waliolipa fedha hizo kwa jinsi alivyowatisha baadhi yao, na hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilisema kuwa fedha walizotozwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi ili waachiwe hazionekani katika makusanyo ya serikali.

Mmoja wa watu waliotishwa na Biswalo ni Tito Magoti, kama anavyosimulia katika video hii.

Erick Kabendera, mwandishi wa habari ambaye alitekwa na baadaye akabambikiwa kesi ya uhujumu uchumi, baadaye akalipishwa zaidi ya milioni 200 (zilizochangwa na Wasamaria wema) ili aachiwe huru, baadaye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema:

“Biswalo alitumia nafasi yake kinyume cha maadili ya utumishi wa umma. Nakumbuka siku nilipoachiwa huru, alipiga simu na kutishia kunirudisha jela kama ndugu na marafiki wangefika nyumbani kunipa pole, ikiwemo (juu ya) kifo cha mama. Siku zilizofuata uliwekwa ulinzi kufuatilia wageni wangu.”

Harbinder Seith Singh, mtuhumiwa mwingine wa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, aliachiwa baada ya kulipishwa shilingi milioni 200 ikiwa sehemu ya kiasi alichotakiwa alipe – shilingi bilioni 26. Orodha ya watuhumiwa walioachiwa baada ya kulipishwa mamilioni ye fedha ni ndefu. Wengi wao ni wafanyabiashara wakubwa wenye asili ya Kiasia.

Kwa mwenendo wa serikali ya Tanzania, kwa muda mrefu, Mkurugenzi wa Mashitaka hawezi kufanya uamuzi wowote wa aina hii bila idhini ya rais. Kwa sehemu kubwa ofisi yake hutekeleza amri au maagizo ya rais.

Taarifa zinadai kuwa wizi huu wa fedha na kuzificha China ni sehemu ndogo ya ufisadi mkubwa uliofanyika katika serikali ya awamu ya tano ukihusisha vigogo ambao wasingeweza kuguswa na chombo chochote cha dola.

Jitihada za kupata maoni ya Prof. Kabudi na Jaji Biswalo hazikuzaa matunda. Lakini taarifa tulizonazo ni kuwa serikali ina ushahidi usiotiliwa shaka (ndani ya duru za kibalozi na kiusalama) juu ya ushiriki wa wawili hawa katika utoroshaji wa fedha hizo.

Ikumbukwe kuwa katika awamu ya tano, hakuna mtumishi yeyote wa serikali aliyeruhusiwa kwenda nje ya nchi bila ruhusa ya rais. Ingekuwa vigumu zaidi kwa kiongozi mwandamizi wa serikali kubeba furushi la pesa na kulitoroshea nje ya nchi bila kibali, ulinzi na idhini ya mifumo ya serikali.

Uchunguzi unaendelea…

Like
2