NECTA Wapingwa

Wanafunzi Mlandizi wanakalia vumbi kwa kukosa madawati

Siku moja baada ya Baraza la Mitihani (NECTA) kusitisha utaratibu wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora wa matokeo ya kidato cha nne, Baraza hilo limeshauriwa kuboresha mazingira, vigezo na viwango vya ushindani baina ya shule na shule ili kuchochea ubora wa elimu badala ya kufuta kabisa utaratibu wa ushindani.

Ushauri huo umetolewa na Mwanaharakati wa Maendeleo, Edward Kinabo, wakati akitoa maoni yake kuhusu uamuzi huo wa NECTA na hali ya elimu nchini.

Jana, Kaimu Mtendaji wa NECTA, Athumani Salumu Amasi, alisema Baraza hilo limesitisha kutangaza shule bora na wanafunzi bora kwa kile ilichoeleza kuwa utaratibu huo haukuwa na tija kwasababu ya mazingira ya shule ni tofauti, na kwamba kufanya hivyo kulikuwa kunazitangazia shule biashara tu.

Akizungumzia uamuzi huo wa NECTA, kupitia taarifa yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana, Kinabo, amesema ushindani ni muhimu katika elimu kwani huchochea hamasa, bidii pamoja na wajibu wa shule na wanafunzi kutaka kufanya vizuri zaidi na kwamba NECTA haikupaswa kufuta kabisa ushindani bali walipaswa kuboresha utaratibu wa ushindani.

“Kama hoja ya NECTA ni kuepuka kushindanisha shule zote na wanafunzi wote kwa kuwa wanasoma katika mazingira tofauti, basi kilichopaswa kufanywa na NECTA si kufuta kabisa ushindani, bali ni kuyapanga matokeo ya shule hizo katika makundi tofauti tofauti ya shule zinazofanana na kisha kuzitangaza shule bora zilizofanya vizuri zaidi kulinganisha na shule nyingine kwenye kundi husika. Na wangeweza pia kutangaza mwanafunzi bora kwa kufuata utaratibu huo huo”, alisema Kinabo.

Mwanaharakati huyo alifafanua kuwa shule za binafsi zingeweza kupimwa kwenye kundi lake na shule za serikali zingeweza kugawanywa katika makundi kadhaa kulingana na mfanano wa mazingira yao.

Kinabo ambaye pia alikuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kibaha Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, alisema hatua ya NECTA ya kusitisha ushindani kwa hoja ya shule kuwa na mazingira tofauti, ni sawa na serikali kukubali kuyakumbatia matabaka katika elimu, jambo ambalo alisema ni kinyume na malengo ya kitaifa na kimataifa yanayosisitiza haki na fursa sawa kwa watoto wote kupata elimu iliyo bora.

“Serikali inapaswa kuhakikisha ushindani unaendelezwa na shule zote zinaboreshwa ili kuondoa matabaka na kuwahakikishia watoto wa kitanzania haki na fursa sawa ya kupata elimu iliyo bora. Siyo sahihi hata kidogo kuridhika na hali ya baadhi ya wanafunzi kusoma kwenye shule zenye mazingira bora na wengine mazingira duni”, alisisitiza.

Alidai kuwa hatua hiyo ya NECTA ya kufuta ushindani wa shule, inaonekana kulenga kuficha aibu ya shule nyingi za serikali hususan ya sekondari za kata ambazo nyingi zimekuwa hazifanyi vizuri kulinganisha na shule binafsi.

“Serikali inapaswa kuchukua hatua za kuboresha mazingira na ubora wa elimu inayotolewa kwenye shule zake zote za msingi na sekondari badala ya kuweka mpira kwapani, kwa kukimbia changamoto ya kiushindani kutoka kwa shule binafsi” aliongeza Kinabo.

Akitoa mfano wa hali duni ya elimu inayozikabili shule za serikali, Kinabo alisema shule za msingi katika mamlaka ya mji mdogo wa Mlandizi, wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani zinakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa madawati, hali inayosababisha wanafunzi wengi kusoma wakiwa wamekaa sakafuni.

“Tatizo la madawati ni kubwa karibu kwa shule zote za Mlandizi, zikiongozwa na shule ya msingi Mtongani. Hali kama hii ndiyo inayosababisha wanafunzi wa shule za serikali kukosa msingi mzuri wa elimu na kufanya vibaya kulinganisha na wa shule binafsi”, alisema Kinabo na kuonesha picha za baadhi ya wanafunzi wa mji wa Mlandizi wakiwa wamekaa chini kwa kukosa madawati

Alitoa wito kwa serikali kupitia TAMISEMI na Wizara ya elimu kuingilia kati kwa haraka na kutatua tatizo kubwa la madawati lililopo kwenye shule mbalimbali nchini, hususan kwa kuanzia na Mji wa Mlandizi na wilaya ya Kibaha, kwani tayari kumeshathibitika kuwa na changamoto kubwa ya uhaba mkubwa wa madawati.

Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mbalimbali vilivyopo wilaya ya Kibaha pamoja na wadau mbalimbali wa elimu nchini, kujitokeza kwa wingi katika kuisaidia serikali kwa kuchangia madawati.

Katika hatua nyingine, Kinabo, alisema pamoja na viwango mbalimbali vya ufaulu vilivyotangazwa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, bado hali ya ubora wa elimu nchini ni mbaya kwasababu ya mfumo wa elimu na mitaala yake kushindwa kuzalisha wasomi wenye ujuzi na stadi zinazohitajika katika soko la ajira.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa shirika la UNICEF na Tume ya Kimataifa ya Elimu, iliyozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana, asilimia 75 ya vijana wa kitanzania hawana ujuzi wala umahiri unaohitajika katika soko ajira na asilimia 62 ya watoto wa umri wa miaka 10 Tanzania, wa shule za msingi, hawawezi kusoma vizuri hata sentensi fupi ya kawaida, huku asilimia 83 wakiwa hawamudu kuhesabu vizuri tarakimu.

Kwa ujumla, ripoti hii, ya hivi karibuni kabisa, imeweka bayana kuwa wanafunzi nchini Tanzania hawapati msingi mzuri wa elimu wala kujengwa katika ujuzi na stadi muhimu zinazoweza kuwapa fursa ya kuja kuajirika au kujiajiri, alifafanua kuhusu ripoti hiyo.

Ili kuboresha hali ya elimu nchini, Mwanaharakati huyo, ameishauri serikali kuongeza uwazi na ushirikishwaji wa wadau wengi zaidi wa elimu katika mchakato wa kupokea na kuchakata maoni ya kuboresha mfumo, mitaa na sera ya elimu unaoendelea nchini.

Alisema ushiriki wa kina wa wadau katika mchakato huo na uzingatiaji wa maoni yao ndiyo utakaosaidia kufanya mageuzi makubwa na yenye tija ya mitaala ya elimu, mfumo wa udhibiti ubora wa elimu, maslahi ya walimu pamoja na motisha, ili sera, mipango ya elimu pamoja na bajeti za sekta ya elimu, viweze kujielekeza kwenye haja ya kuzalisha wasomi wenye ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira nchini na dunia nzima kwa ujumla.

Like