Tarime “yaitika”

– Mbowe aahidi neema kwa wachimbaji madini wa Kitanzania

– Heche amshughulikia Waitara, wanaCCM 160 wahamia Chadema

MAELFU ya wananchi wa majimbo ya Tarime Vijijini na Tarime Mjini, wamejitokeza kwa wingi katika mikutano sita ya hadhara, iliyohutubiwa leo na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

Akihutubia wananchi wa maeneo ya Sirari, Kiongera, Nyamwaga, Nyamongo, Kisaka na Tarime Mjini, Mbowe, ameahidi kuwa Chadema itakapongia madarakani itafanya mageuzi makubwa ya kisera na kisheria, yatakayowezesha halmashauri, wachimbaji wadogo na kampuni za madini za Kitanzania, kujengewa uwezo na kuingia ubia na kampuni bwa za kigeni za uchimbaji wa madini.

Lengo ni kuhakikisha Watanzania wanamiliki na kunufaika moja kwa moja na migodi yao kwa kushirikiana na wawekezaji wakubwa wenye tija.

Mbowe amesema kuwa sera na uongozi mbaya wa Chama cha Mapinduzi (CCM), vimesababisha migodi kuwa chini ya kampuni za kigeni pekee, huku wachimbaji wadogo wenyeji wakihamishwa na maeneo yao yanachukuliwa na wageni.

“Nilikwenda kijiji cha Mwakitolyo, kule Solwa, mkoa wa Simiyu, kwenye uchimbaji mdogo wa dhahabu. Wachimbaji wadogo wamehamishwa, halafu serikali imewapa Wachina kazi ya kuwa wachimbaji wadogo. Leo, kwa sababu ya CCM, Watanzania hawana haki hata ya kuwa wachimbaji wadogo wa madini yao. Lazima tufanye mabadiliko,” alisema Mbowe.

Amesema kwamba gawio ambalo serikali kuu na halmashauri zimekuwa zikipata kutokana na madini ni dogo sana linapolinganishwa na kile ambacho wageni wanachukua

“Nimetoka Nyamwaga. Halmashauri ya Tarime Vijijini mnapewa bilioni 8 tu kwa mwaka kama fedha za mgodi kujitolea kwa jamii yaani “Corporate Social Responsibility” (CSR), lakini wanapata faida ya zaidi ya trilioni mbili. Nimetoka Nyamwaga, wananchi wamenieleza kwamba wanaandaliwa kuondolewa ili kupanua mgodi. Hawajalipwa fidia. Kwa hiyo, Watanzania wanaondolewa kwenye dhahabu yao, halafu halmashauri inakuja kupewa fedha kidogo.

“Chadema tukiingia madarakani tutahakikisha Watanzania hawaondolewi kwenye madini. Tutahakikisha wachimbaji wadogo, halmashauri na kampuni za Kitanzania zinajengewa uwezo na kuingia ubia na kampuni za kigeni, ili vijana wetu wafaidike na utajiri wa dhahabu,” alisema Mbowe na kushangiliwa na wananchi akiwa Nyamongo.

Naye John Heche, mjumbe wa Kamati Kuu, ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa Tarime (2015-2020), na aligombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini kupitiq Chadema (2020), aliwaomba wananchi wa Tarime, kuiondoa CCM madarakani, kwani imeweka wabunge wanaoitetea serikali, badala ya kutetea wananchi.

Akionekana kumlenga Mwita Waitara, mbunge wa sasa wa Tarime Vijijini (CCM), Heche alisema:

“Bandari zetu 54 zimegawiwa hovyo kwa Waarabu. Halafu mbunge mmoja wa Tarime, anaongea bungeni, anasema eti mbunge anayepinga bandari kupewa Mwarabu, huyo anampinga rais, atoke nje. Yaani mbunge kabisa wa Tarime anamtetea Samia, badala ya kutetea bandari zetu? Kwa kuwa ameamua kumtetea Samia badala ya ninyi wananchi, ni lazima tumwondoe ili akapate muda wa kutosha wa kumfanyia kazi Samia. Tumwondoe bungeni, aende akawe muosha vyombo nyumbani kwa Samia.”

Akizungumzia matatizo ya watu wa Nyamongo, Heche alisema walifungua kesi nchini Uingereza dhidi ya mwekezaji, wakipinga mauaji, wananchi kutolipwa fidia pamoja na athari za kiafya dhidi ya binadamu na mifugo, zilizosababishwa na mgodi huo kutiririsha maji yenye kemikali za sumu.

Akasositiza kuwa hata hivyo, wenyeviti wa vijiji 11 (CCM), walihongwa na kutoa ushahidi wa uwongo unaombeba mwekezaji kwenye kesi hiyo, kwa kutoa maelezo kuwa kila kitu kipo vizuri.

Akitaja majina ya wenyeviti hao, Heche aliwaomba wananchi wahakikishe wanawang’oa madarakani wenyeviti wa vijiji hivyo 11, katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika mwakani.

“Ni lazima tufanye mabadiliko. Wameuza kila kitu kwa wageni. Wameshindwa hata kuwapa watoto wetu elimu bora. Huku kwetu kuna dhahabu, lakini badala ya kuandaa na kufundisha mtaala maalum ili watoto wetu waje kuwa wamiliki, wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, wao wanafundisha watoto wetu eti wataje panzi ana miguu mingapi,” alisema Heche na kuongeza:

“Maji duniani yamepungua, lakini nchi yetu ina maji ya kutosha yanayofaa kunywa. Tuna mito, maziwa makubwa na maji mengi ardhini.Tusipowaondoa CCM, waliouza raslimali zetu, siku moja watakuja kusaini mikataba ya kuwauzia wazungu maji yetu,” alisema Heche.

Katika hatua nyingine, katibu wa uchumi wa CCM na mwanaharakati, wilayani Tarime, Damian Makori, alitangaza kujiondoa CCM na kujiunga Chadema.

Makori amejiunga Chadema pamoja na wanachama wengine 160 wa CCM.

Alisema ameamua kujiunga Chadema kwa sababu ameridhika kuwa CCM imezidi kuuza raslimali za nchi, na anataka kushirikiana na wanaChadema katika kuikomboa nchi na kurejesha raslimali kwa wananchi.

Like