Uzi mwembamba unaounganisha Mkapa, Kikwete na Magufuli – 005

MTANZANIA yeyote, au raia wa nchi yoyote, aliyefuatilia utendaji wa serikali zetu tangu mwaka 1995 hadi sasa, atakuwa amegundua kwamba kuna uzi mwembamba unaunganisha marais wetu. Ni watawala wale wale katika mfumo ule ule. Wanatofautiana sura, tabia, na vipaumbele. Wanapotazamwa kwa jicho la karibu, wote wana hulka zinazofanana. Kila mmoja wao ametumia hisia zake binafsi kujaribu kutengeneza Tanzania anayoitaka – katika mfumo ule ule wenye katiba ile ile inayolalamikiwa, inayogandamiza wananchi na kutukuza watawala. Wote hawapendi kukosolewa. Ni wababe, kila mmoja kwa viwango vyake. Makala zifuatazo zinasaidia kuonesha kuwa Mkapa, Kikwete, na Magufuli, ni watawala wale wale, katika zama tofauti; na kila mmoja amekuwa anarudia mambo ya mtangulizi wake kwa staili mpya, na kughilibu wasiotunza kumbukumbu au walio wepesi wa kusahau, akidai anajenga Tanzania mpya.

Ya Mkapa na Jenerali Ulimwengu, Magufuli na Tundu Lissu

KUTOKANA na jina la safu ya Maswali Magumu, kuna watu, hasa mashabiki na wasomaji wa maandishi yangu, wamenibatiza jina “Mzee wa Maswali Magumu.” Ingawa safu yenyewe ilipata jina rasmi mwaka 2002, ilianza miaka saba kabla ya hapo, na hadi sasa inajadili masuala ya zamani na ya sasa, lakini ilipata umaarufu mkubwa kuanzia mwaka wa kwanza wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete (2006).

Baadaye nilipata kuambiwa kuwa kilichovutia wasomaji wengi tangu wakati huo, ni ujasiri wa mwandishi kumsema, kumkosoa na kumshauri rais bila kumung’unya maneno, katika kipindi ambacho takribani vyombo vyote vya habari vilikuwa vinafanya kazi ya kumsifu, kumtukuza na kumtetea kwa kila jambo.

Wakati huo, ilikuwa vigumu kukosoa Rais Kikwete, na swahiba zake wawili – Rostam Azizi na Edward Lowassa. Nilipoanza kuwakosoa, mhariri mmoja rafiki yangu, alinishauri, “achana nao, hawa watu watakuua au watakuroga.” Hatimaye, king’ang’anizi changu kilifanikiwa kukuza umaarufu wa safu hiyo, na kuhamasisha waandishi waoga kwamba inawezekana kuandika habari na uchambuzi wa kweli usiowapendeza rais, waziri mkuu, na watu wao wa karibu.

Baada ya miaka miwili hivi, nami nilianza kusoma maandishi ya watu wengine, ambayo yalikuwa makali kuliko hata Maswali Magumu. Lakini kikubwa kilichoendelea kutofautisha Maswali Magumu na safu nyingine, na kuipa umaarufu, ni kwamba ilifanikiwa kujitambulisha kama uchambuzi huru ulio maalumu juu ya Ikulu na rais. Uchambuzi huu umefanikiwa kuchokonoa, kusumbua, na kufikirisha watawala katika awamu tatu mfululizo –Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, na John Magufuli.

Katika miaka 10 ya Rais Kikwete, kuna waliokuwa na mawazo potofu kwamba nilikuwa na ugomvi binafsi na rais. Wapo walionitisha kwa meseji za simu. Wengine walinitisha kwa kauli za moja kwa moja. Wengine walipiga simu, wakinitaka niachane na tabia ya kumkosoa rais, vinginevyo, yangenipata “makubwa.”

Mwanzoni mwa Februari 2013, nilitangazwa kwenye mtandao wa Jamii Forums kwamba, “Ngurumo is no more” (kwa maana kuwa nilikuwa nimeaga dunia). Aliyebandika andiko hilo alisema kuwa nilikuwa nimegongwa na gari usiku wa manane nikiwa naendesha gari kurejea nyumbani.

Ndani ya muda mfupi, taarifa hizi zilileta taharuki kubwa kwa rafiki zangu, hadi pale walipojua kuwa ulikuwa uzushi tu, na kwamba inawezekana kuna mtu alikuwa ameuawa usiku huo, akidhaniwa ni Ngurumo.

Kuna rafiki zangu kadhaa, wakiwamo viongozi wa dini, wamewahi kunionya na kunitaka nifanye kazi nyingine, au niandike masuala mengine, niachane na siasa au rais; wakiamini kwamba serikali inaongozwa na watawala dhalimu ambao wangeweza kuondoa uhai wangu.

Baadhi ya rafiki wa karibu na wapambe wa Rais Kikwete walinichukia, na hata kunitumia ujumbe kwamba wangeniundia ajali. Mwaka 2010, Jumapili moja nikiwa Mwanza kikazi, mtu mmoja aliyekerwa na uchambuzi wangu juu ya ombwe la uongozi, alinipigia simu na kunitaka tuonane. Tulipokutana katika hoteli moja Jijini Mwanza, alinitisha kwa maneno, akanitaka niachane na Kikwete.

Hakujua kwamba pale tulipokuwa sikuwa peke yangu. Kuna watu wangu nilioambatana nao , wakati naenda kukutana naye, ambao walikuwa chonjo wanafuatilia mazungumzo yetu, kwa kuhofia kwamba mtu huyo angeweza kunidhuru. Hakuwahisi, hakuwaona, na aliondoka bila kujua kuwa alikuwa anafuatiliwa.

Katika mazungumzo yetu, nilimjibu kwa upole, nikamweleza mambo makubwa na mazito ambayo nilikuwa nimeyahifadhi, sijayandika. Alikuwa amedhani kwamba kwa kunishambulia ana kwa ana, ningekuwa mpole na mnyonge. Baada ya maelezo yangu kuhusu udhalimu wa serikali, na baada ya kugundua kwamba sikuwa na hila wala woga, na kwamba naijua vema serikali aliyokuwa anaitetea, na kwamba yapo nisiyoweza kuandika, naye aliguswa; akaanza kusimulia jinsi alivyoonewa kwa kuvuliwa ukuu wa wilaya. Mazungumzo yakabadilika. Ghafla, tukajenga urafiki wa mashaka.

Mwaka 2015 mwanzoni, nilikutana na mmoja wa wapambe wa karibu wa Rais Kikwete, ambaye alikuwa ameanza kugundua matatizo ndani ya serikali, na ameanza kukubaliana na uchambuzi wangu kuhusu utendaji wa serikali ya awamu ya nne. Aliniambia: “Unajua siku zote unamwandika Kikwete sisi wengine, kwa kuwa tupo karibu naye, kuna mambo hatukuona; tulidhani unamwonea, na kwamba labda mna ugomvi binafsi. Leo tunapotazama nyuma, tunaona kuna mambo uliyajua na kuyasema, lakini sisi hatukuwa tunayaona. Uliyajuaje?”

Kwa muda wote huo, safu ya Maswali Magumu, imejijenga kuwa uchambuzi unaokera walio madarakani, unaogusa na kutetea wananchi wa kawaida.

Katikati ya mwezi Agosti 2015, wakati kampeni za uchaguzi mkuu zinakaribia kuanza rasmi, nilipokea simu kutoka namba nisiyojua. Nilipojibu, mpigaji akajitambulisha kuwa ni John Pombe Magufuli, ambaye alikuwa mgombea urais kupitia CCM. Akasema mkewe alikuwa amemnunulia nakala ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili. Ndani ya gazeti hilo kulikuwa na makala ya Maswali Magumu iliyokuwa inahoji uhalali na mantiki ya ahadi ya Magufuli kwa walimu kwamba kama angeshinda angewagawia laptopu.

Nilikuwa nimeorodhesha madai ya walimu ya muda mrefu ambayo serikali iliyapuuza, nikamkumbusha kuwa mkewe ni mwalimu – angeweza kumkumbusha. Nikahoji kama anajua idadi ya walimu wote, mazingira wanakoishi na kufanyia kazi, uwezo wao kutumia laptopu – kama ni kwa anasa au taaluma, na mambo mengine mengi.

Mwanzoni, alisifia uandishi wangu, na jinsi ambavyo naye amekuwa msomaji wa kudumu wa Maswali Magumu. Wakati huo alikuwa anazunguka mkoa kwa mkoa “kujitambulisha” kabla ya kuanza kampeni. Kwa sauti ya upole ambao sijawahi kusikia kwa Magufuli, alifikisha kwangu  ujumbe aliokuwa amekusudia.

Alisifu uchambuzi wangu wa huko nyuma, kwamba amekuwa anafurahishwa na jinsi ninavyoichapa serikali – labda kwa kuwa sikuwahi kuandika masuala yake kabla ya hapo. Lakini alisisitiza: “Kwa makala yako ya leo, Ngurumo umenionea.” Alisema kuwa hajawahi kutoa ahadi ya kugawa laptopu kwa walimu, na kwamba alikuwa amelishwa maneno kwa sababu za kisiasa.

Alisisitiza kuwa hata kauli ya mwaka 2011 aliyonukuliwa na vyombo vya habari akisema wananchi wa Kigamboni wasioweza kulipa nauli mpya ya pantoni “wapige mbizi,” haikuwa ya kweli;  kwamba hajawahi kutamka maneno hayo. Nilimwelewa, lakini sikumwamini.

Nilisoma mazingira ya simu yake hiyo, nikamjibu tu: “nimekusikia mheshimiwa.” Naye akajibu: “Nimekusamehe.” Neno lake hilo kwamba amenisamehe lilinishtua. Nikajiuliza, “huyu ananisamehe kwa kosa lipi, na kwa mamlaka yapi?” Kwa mbali, lilinijengea taswira ya kiongozi mbabe asiyependa kuhojiwa au kusahihishwa, na anayependa kuadhibu. Ninaposhuhudia anayofanya sasa akiwa madarakani, naelewa kwamba sikuwa nimekosea. Huyu ni kiongozi anayedhani kwamba bila kuumiza au kuadhibu wengine, madaraka yake hayatatambulika.

Baada ya Magufuli kuwa amepata urais, Maswali Magumu yalisitishwa kwa muda, huku nikiwa naandika uchambuzi usio na jina maalumu katika magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na Mawio na, kama kawaida, uchambuzi wangu ulijielekeza kwa rais na Ikulu.

Mnamo mwezi Machi 2016 nilipokea ujumbe kutoka kwake, kupitia kwa rafiki yake ambaye ni mhariri mwenzangu niliyewahi kufanya kazi naye ofisi moja (2004 -2006), akaniambia: “Mheshimiwa rais amenituma, anasema, alikufanyia nini, mbona unamwandama hivyo katika maandishi yako?” Nilitabasamu, halafu nikamjibu kirafiki: “Ndugu yangu, hata wewe? Alivyokwambia hivyo, wewe umemjibu nini? Au nawe unaamini kwamba namshambulia rais? …Ni hivi, hajanifanyia jambo lolote baya. Sina ugomvi naye binafsi. Natimiza wajibu wangu. Mwambie naye aendelee kutimiza wajibu wake.”

Baadaye nilikutana na wapambe kadhaa wa Rais Magufuli, wasiopendezwa na uchambuzi wangu. Mbunge mmoja wa CCM kutoka Mkoa wa Kigoma alinipigia simu na kuhoji: “Mbona unamshambulia rais wetu hivyo?” Nikamuuliza kwa upole, “kwani nimebadilika? Huyo aliyetoka nilikuwa namfanyeje?” Akacheka na kukata simu.

Mwingine aliniandikia na kuhoji: “Kwa miaka 10 mfululizo ulimwandika vibaya Rais Kikwete. Inakuwaje unaacha kumwandika sasa, unamwandama Rais Magufuli anayeonesha dalili zote za kuongoza nchi kwa uadilifu na kuchukua hatua dhidi ya ufisadi wote uliofanyika huko nyuma?”

Ndugu zangu hawa ni kielelezo cha tabia ya kundi fulani la Watanzania. Ndivyo wanavyofikiri. Hawajui kwamba sikuwahi kumwandika vibaya rais yeyote, bali nimewahi kuchambua kauli, matendo, mwenendo, na mambo kadhaa waliyofanya na waliyosahau au waliyopuuza wakiwa madarakani.

Wakati wapambe hawa wananishutumu, kwangu hiyo imekuwa ni njia nzuri tu ya kurudisha watawala mstarini, na kuwakumbusha wajibu wao. Imekuwa ni njia yangu ya kusemea, kutumikia, na kutetea wananchi wanyonge wasio na pa kusemea.

Kwa sababu ya watu wenye hisia na maoni kama ya watu hawa, na baada ya kumwelewa Rais Magufuli, niliamua kuandika upya Maswali Magumu katika gazeti la MwanaHALISI ili kuendeleza kazi nzuri niliyoanza miaka zaidi ya 20 iliyopita. Vile vile, niliamua kujibu maswali ya baadhi ya wasomaji kwa kirefu, kwa nia ya kutoa elimu ya uraia, kuhusu demokrasia na umuhimu wa vyombo vya habari vilivyo huru katika ujenzi wa taifa.

Na hili si suala la Rais Kikwete au Rais Magufuli, kwani hata katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa, nilitishwa na wapambe wake, ambao walinionya kwamba nisipoacha “kumlima rais” ningekiona cha mtema kuni.

Nakumbuka jinsi nilivyofukuzwa kwenye mkutano wa ufunguzi wa kampeni za Rais Mkapa mwaka 2000, katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam. Nikiwa ndio naingia kwenye uwanja huo, katikati ya umati wa wananchi, askari aliyevaa suti kama za kaunda alinisogelea, na kuniambia, “ondoka hapa hatukuhitaji.” Kabla sijaelewa kilichokuwa kinaendelea, nilimjibu, “nipo kazini.” Naye akasema, “nasi tupo kazini, hatukutaki hapa.” Nilipoona ameanza kuita wenzake wanibebe, nikashtuka, nikaondoka mwenyewe haraka haraka na kurudi kwangu Magomeni.

Kwa kuwa mkutano ule ulikuwa unarushwa moja kwa moja kwenye televisheni, niliufuatilia nikiwa sebuleni. Kwa hiyo, miaka 16 baadaye niliposikia Rais Magufuli anajitapa na anatisha wapinzani na wote wanaomkosoa, akisema kwamba yeye hajaribiwi na atawavunja miguu, nilitambua kuwa watawala wetu ni wale wale, mfumo wao ni ule ule, na mienendo yao ni ile ile. Na hii ni sehemu ya uzi mwembamba unaounganisha utawala wa Mkapa, Kikwete, na Magufuli.

Ubabe wa Rais John Magufuli na vitisho vya serikali yake dhidi ya vyombo vya habari na wachambuzi wanaokosoa mwenendo wa utawala wake, wanasiasa, wasomi, wanaharakati, wafanyabisahara, na makundi mengine, si mambo mapya. Haya ni marudio au mwendelezo wa mfumo na hulka ile ile ya utawala mkongwe wa CCM, chini ya marais tofauti. Wanazidiana tu upeo na hulka binafsi.

Nakumbuka Januari 2001 alipouawa Rais Laurent Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baadhi ya wafanyakazi wenzangu waliotoka msibani walinifikishia ujumbe mzito kutoka kwa watu waliojiita “vijana wa Mkapa.”  Wakati huo nilikuwa nafanya kazi katika gazeti la The African, lakini pia nilikuwa naandika makala kwenye gazeti la Rai (iliyovuma kweli kweli) katika kampuni ya Habari Corporation iliyokuwa inamilikiwa na kusimamiwa na akina Jenerali Ulimwengu, Salva Rweyemamu, Johnson Mbwambo, Gideon Shoo, na Shaban Kanuwa.

Katika kipindi hicho hicho, serikali ilitangaza kumvua uraia Ulimwengu, ambaye alikuwa anaandika uchambuzi mzito juu ya utawala wa Rais Mkapa ujulikanao kama “Rai ya Jenerali Ulimwengu.” Akaambiwa si Mtanzania. Walimchanganya na wengine ambao walikuwa wamekosana na wakubwa kadhaa ndani ya mfumo tawala, wakawatangaza kwenye vyombo vya habari. Lengo lilikuwa kumdhalilisha Ulimwengu na kukata makali ya makala zake.

Nilitumiwa tena ujumbe kuwa, “bosi wako ameshughulikiwa; bado wewe… endelea na uchokozi wako, utaona!” Sikuwa na tatizo la uraia, lakini kwa kujua hulka ya watawala wa Kiafrika wasiopenda kukosolewa, nilihisi lolote lingeweza kunitokea. Baadaye nilipoanza kuandika uchambuzi katika gazeti la Mwananchi Jumapili, baada ya kushauriana na rafiki yangu Absalom Kibanda, akiwa mhariri wa gazeti hilo, tulikubaliana kuwa uchambuzi huo uitwe Maswali Magumu.

Huko nyuma, hata kabla ya safu ya Maswali Magumu, Alhamisi moja, mwaka 1998, niliandika uchambuzi juu ya suala la rushwa, ukachapishwa kwenye gazeti la Rai ukiwa na kichwa cha habari: “Rais Mkapa unajivunia nini?” Uchambuzi huo ulilalamikiwa sana na Rais Mkapa. Alinuna na kugomba. Alikwenda mbali hadi akamtuhumu Ulimwengu, rafiki yake wa siku nyingi, kwamba ndiye alikuwa ameandika uchambuzi huo kwa kutumia jina langu. Rais Mkapa aliniona mimi ni “mtoto mdogo tu” ambaye nisingeweza kuandika masuala mazito kwa kauli nzito kama ile, tena kwa kumuuliza anajivunia nini.

Siku hiyo hiyo, Paschal Dismas, aliyekuwa mhariri wa habari wa The African, alikuwa amenipanga kuambatana na Kikwete katika ziara ya kisiasa jimboni kwake Chalinze, wakati huo akiwa pia waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Jimbo la Chalinze lilikuwa halijagawanywa. Kwa sasa eneo la jimbo la zamani la Chalinze ndilo linajumuisha majimbo ya Chalinze na Bagamoyo.

Pamoja na waandishi wengine, tulipanda gari moja na waziri, na tulikuwa na magazeti ya siku hiyo tunajisomea. Lakini yeye hakuwahi kusoma gazeti la Rai. Jioni yake tuliporejea Dar es Salaam, waziri alikuwa anawahi hafla Ikulu, ambayo Rais Mkapa alikuwa amemwandalia mgeni wake, Rais Bakili Muluzi wa Malawi.

Kesho yake tukiwa ofisini kwa Kikwete kwa ajili ya kuendelea na ziara jimboni kwake, nilianzia kwa Simon Ileta, aliyekuwa ofisa habari wa wizara. Akanitania akisema, “jana mbona mmemgonga sana mzee?” Nikamjibu, “mbona hiyo ni kawaida ya Rai? Ulitarajia tuandike kwa staili tofauti?” Nilijua alikolenga. Sikufafanua.

Lakini sikuwa nimejua uzito wa alichokuwa anazungumzia. Baada ya kuanza safari tukiwa ndani ya gari lake, Kikwete akauliza kwa utani, “Kwani Rai mmeandika nini jamani? Maana rais amekasirika kweli kweli; jana alishindwa kujizuia hata mbele ya wageni.” Swali la Kikwete lilinifanya nitambue kuwa alikuwa hajasoma kilichoandikwa, na hakujua kuwa aliyeandika kilichomuudhi rais ni mimi. Naye nilimjibu kama nilivyomjibu Ileta, kwamba ni uchambuzi wa gazeti kuhusu utendaji wa serikali.

Hata hivyo, sikujua uzito wa maandishi yangu hadi niliporejea ofisini jioni. Wakati huo, ofisi zetu zilikuwa kwenye ghorofa ya tano, kwenye Jengo la NSSF, katika makutano ya Barabara za Morogoro na Bibi Titi Mohamed, Jijini Dar es Salaam. Nikiwa nashuka ngazi, nilikutana na Muhingo Rweyemamu(+), wakati huo akiwa mhariri wa makala wa gazeti la Mtanzania. Akaniambia kwa utani, “Mkapa anakutafuta. Ile makala uliyoandika imemkera sana, nasikia anasema ataondoka na kichwa chako!”

Kwa jinsi Muhingo alivyokuwa mtu aliyependa utani, tulicheka, kila mmoja akaendelea na safari yake; na tungeweza kuishia katika kicheko. Lakini niliunganisha maneno ya watu watatu hawa – Ileta, Kikwete, na Muhingo. Nikahisi uchambuzi wangu ulikuwa umegusa pabaya. Nikalazimika kuusoma upya kwa jicho la msomaji. Kweli, nikagundua kuwa ulikuwa uchambuzi wenye ukweli mchungu kwa watawala.

Katika maandishi yangu, nilikuwa nahoji majigambo ya rais kwamba anapambana na rushwa. Nilimrejesha kwenye historia ya mbio zake za kusaka urais. Nikamkumbusha kuwa kama si jitihada binafsi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yeye (Mkapa) asingeteuliwa kuwa mgombea, na hata baada ya kuteuliwa, asingepata urais.

Nikamkumbusha kuwa hata kura za kuwapiku washindani wake wakuu – Kikwete na Cleopa Msuya – zilitiliwa shaka, kwani wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, walijua, na walisema kilichofanyika ili Mkapa apitishwe.

Nilienda mbali na kuzungumzia hata kampeni yake nzito na ngumu, na kwamba licha ya nguvu na ushawishi wa Mwalimu Nyerere, taarifa zisizo rasmi zinasema, na watu wake wananong’ona, kuwa kama si mbinu kutumika, si ajabu rais angekuwa Augustino Lyatonga Mrema wa NCCR-Mageuzi. Nikamkumbusha jinsi matokeo ya Jiji la Dar es Salaam yalivyofutwa kihuni, baada ya serikali kubaini kuwa majimbo mengi yalikuwa yamechukuliwa na wapinzani.

Baada ya hapo nilirejea uamuzi wake wa kuunda tume ya kuchunguza mianya ya rushwa, chini ya Joseph Warioba; na mapendekezo ya tume hiyo ambayo yeye rais alikataa kutekeleza. Na kila alipohojiwa kuhusu suala hilo alisema, “sikuwatuma kuchunguza rushwa au wala rushwa, bali mianya ya rushwa.”

Nilisisitiza kwamba ingawa aliingia kwenye kinyang’anyiro akiwa anaitwa “Mr. Clean,” ndani ya miaka mitatu ya utawala wake, alikuwa ameanza kupoteza sifa ya usafi uliomfanya Mwalimu Nyerere amnadi na ampendelee dhidi ya akina Kikwete na Msuya.

Nilisema pia kwamba kwa vigezo vyote hivyo, Mkapa alikuwa amepata urais wa kupewa si wa kuchaguliwa. Hivyo, hakuwa madarakani kwa ridhaa ya wananchi, bali kwa ridhaa ya waliolazimisha awe rais kwa njia zozote zile. Nikahitimisha hoja yangu kuwa rais anayeingia madarakani kwa “wizi wa kura” hawezi kuaminika kwa wananchi anapokuwa anazungumzia kupambana na rushwa, kwa kuwa naye ni zao la rushwa, hata kama si yeye aliyeziiba.

Nilionesha kuwa Rais Mkapa hakuwa na uwezo wala nia ya dhati ya kupambana na rushwa. Nikahitimisha uchambuzi wangu kwa kuhoji kwamba iwapo atashindwa hilo, huku akitambua kuwa hiyo ni moja ya mambo muhimu yaliyomfanya Mwalimu Nyerere ampiganie, atajivunia nini?

Baada ya kupitia uchambuzi huo, nami niliridhika kwamba nilikuwa nimeandika “kitu kikali.” Nilielewa sababu ya rais kukasirika – kibinadamu – ingawa sikukubaliana na hasira zake. Lakini sikudhani kwamba zingekuwa hasira za kudumu, na zenye kuumiza watu kwa sababu ya uwezo wao wa kutia shaka, kufikiri, na kuhoji; kwa kuwa katika mfumo wa kidemokrasia, kiongozi anayechukia wananchi wanaomkosoa anakuwa hajui kazi yake na wajibu wa wapiga kura wake.

Baadaye nilipata taarifa kuwa uchambuzi wangu ule, ni moja ya maandishi yaliyomfanya Rais Mkapa amuwazie mabaya Jenerali Ulimwengu, ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Habari Corporation iliyokuwa inamiliki gazeti la Rai, lililochapisha uchambuzi huo. Haikuwa nia yangu, na sikuju kabla, kwamba kwa uchambuzi wangu nilikuwa ninachangia kumwongezea matata.

Uchambuzi wangu nao ulifanywa kuwa chachu ya “ugomvi” wa marafiki hao wa zamani, vijana wa Mwalimu Nyerere, ambao walikuwa wamekosana kwa sababu zisizonihusu mimi. Nilitambua, na ukweli umebaki hivyo hadi leo, kwamba Ulimwengu ni mmoja wa watu waliokuwa karibu na Mkapa katika harakati za kuamua, kutangaza, na kugombea urais; na alishirikiana na wengine kumpigania wakati wa kampeni.

Tulisikia baadaye kuwa tofauti zao za awali zilianza pale Ulimwengu alipoweka pembeni urafiki, akaendekeza taaluma ya uandishi wa habari katika masuala yaliyohusu serikali ya Rais Mkapa. Kosa la kwanza ni pale gazeti la Mtanzania lilipoandika kuhusu uteuzi wa Paul Kimiti kuwa waziri mkuu, rais alipokuwa anaunda serikali. Rais Mkapa alichukia, akabatilisha uteuzi, Kimiti akakosa uwaziri mkuu, fursa ikamwangukia Frederick Sumaye, rafiki mwingine wa zamani wa Rais Mkapa.

Hata pale Ulimwengu alipoomba kufanya mahojiano maalumu na rais, akitaka gazeti lake liwe la kwanza kumhoji, aligonga mwamba, na fursa hiyo ikachukuliwa na mwandishi wa habari kutoka nje ya nchi. Ufa ukaanza kujengeka kati ya wawili waliofahamiana, walioheshimiana, na hata kutambiana kirafiki katika mambo kadhaa.

Hali hii isiyo ya lazima, ilikuja kumtesa zaidi Ulimwengu kwa sababu ya tabia na hulka yake ya kufikiri, kuhoji, na kutilia shaka wenye mamlaka, sana sana kupitia safu yake – rai ya jenerali ulimwengu. Kwa hiyo, hata maandishi yetu, sisi wadogo, yalihusishwa na Ulimwengu kwani wakubwa walidhani ndiye mwenye uwezo na sababu za kufikiri, kuchambua, kuhoji, au hata kudiriki kuandika mambo mazito kama kitaifa.

Sikujua pia kwamba kwa uchambuzi wangu nilikuwa nimechochea “ugomvi” mkali kati ya serikali na gazeti makini kwa wakati ule, kiasi cha serikali kudiriki kutuma makachero wake wachunguze nani anaandika nini, na kuripoti kwa wakubwa wao. Baadhi yao walifanikiwa kujichomeka kwenye chumba cha habari kwa kuomba kazi na kuajiriwa kama waandishi wa habari. Kumbe walikuwa na jukumu tofauti. Walibainika na kuondolewa baada ya muda kupita. Kama ni madhara, yalikuwa yameshatokea. Na kwa hatua hiyo, “vijana wa Mkapa” walikuwa wamefanikiwa kutuchongea rasmi kwake.

Siku serikali ya Rais Mkapa ilipotangaza kumvua uraia Jenerali Ulimwengu, katika mazingira yenye utata, chumba kizima cha habari kilipatwa na simanzi na mshtuko mkubwa. Nami nilijua kuwa ingawa “ugomvi” wake na rais ulitokana zaidi na msimamo wake, uandishi wake, na hasa ukweli aliokuwa anafichua kupitia maandishi yake, nilikuwa miongoni mwa watu waliochangia katika madhila yaliyompata.
Kitendo hiki kiliambatana na propaganda nyingi za serikali dhidi ya waliovuliwa uraia; na ilifanikiwa kwa sababu kulikuwa na mianya ya kisheria ya kusaidia serikali kutimiza azima yake.

Lakini hata leo, wanaomfahamu vema Ulimwengu tangu akiwa kijana mdogo pale Kamachumu, waliosoma naye elimu ya msingi, sekondari na chuo kikuu, waliofanya kazi naye akiwa mwanachama wa TANU Youth League na CCM, wanaojua alivyowakilisha taifa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa katika fursa alizopewa nje ya nchi; waliojua ukaribu wake na Mwalimu Nyerere; waliomsikiliza akijenga hoja nzito bungeni, walioshuhudia akijiuzulu ukuu wa wilaya na kujikita moja kwa moja katika uwekezaji na uandishi wa habari; wanapomlinganisha na baadhi ya viongozi wetu wazembe, waongo, wala rushwa, na mafisadi, wanatambua kuwa sababu kuu iliyofanya serikali imdhalilishe Ulimwengu ni hulka yake ya kutopenda kunyamaza, na mbaya zaidi, kusema ukweli mchungu na kuibua maswali magumu dhidi ya serikali iliyoongozwa na rafiki yake wa zamani.

Kwanini nimetoa simulizi refu la Ulimwengu na Rais Mkapa? Nimeona mwelekeo huu unajirudia katika kila awamu ya serikali. Katika kipindi chote hicho, nimeshuhudia wakosoaji wa serikali wakitishwa na kuumizwa. Vyombo vya habari vinafungwa, tena kwa kutumia sheria ya kikoloni katika nchi huru. Baadhi ya wanaharakati wameteswa na kuumizwa vibaya kwa sababu ya kutofautiana na mipango au uamuzi wa serikali. Wengine wamepoteza maisha. Mimi mwenyewe nimeponea chupuchupu!

Na wakati serikali inafanya hayo, inadhamiria kunyamazisha wananchi wanaofikiri kinyume cha maoni ya watawala. Haitaki mawazo mbadala. Haiko tayari kuboresha kazi zake, bali inataka ipigiwe makofi.

Kwa bahati mbaya zaidi, serikali ya Rais John Magufuli, imerejesha ubabe wa serikali ya Rais Mkapa. Rais mwenyewe alishasema hadharani Februari 5, 2016, kwamba anadhamiria “kuua upinzani,” na kwamba mkakati wake ni “kupiga mchungaji ili kondoo watawanyike,”  ili wananchi wakose mtu wa kuowangoza. Haya yanayowapata viongozi wakuu wa upinzani ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira hiyo.

Ukweli ni kwamba hata akifanikiwa kutekeleza hayo anayopanda, hataweza kuua upinzani wa vyama, raia mmoja mmoja, wasomi, waandishi wa habari, wanaharakati; nje au ndani ya chama chake. Sana sana, atajiua yeye mwenyewe bila kujua. Kwa kadiri watawala wetu watakavyoendelea kuonesha ukatili dhidi yetu, ndivyo wananchi nao watakavyojengewa usugu mioyoni mwao, na ukatili dhidi ya serikali.

Rais Mkapa alipambana na Ulimwengu kwa kumvua uraia. Magufuli amepambana na Tundu Lissu kwa risasi za moto mchana kweupe. Mbali na Lissu, wapo wengine waliopotea na wanaoendelea kuteswa katika mikono ya “watu wasiojulikana.” Hapo hapo anapambana kumtesa Freeman Mbowe na wabunge wenzake kwa kesi za kutunga, na kwa kuwafilisi au kuwaharibia mali zao. Na sasa anafanyia mabadiliko sheria ya vyama vya siasa ili kuviweka chini ya himaya yake moja kwa moja na kuvizuia kisheria kumpinga.

Jambo ambalo rais anasahau ni kwamba kadiri atakavyodiriki kuua wakosoaji wake akidhani anapunguza kauli asizopenda, ndivyo watakavyoibuka wapinzani wakali zaidi kuliko wanaouawa. Damu ya binadamu inapomwagwa na binadamu mwenzake, tena kikatili, ina tabia ya kuzungumza. Na damu inapozungumza, watawala hawatanusurika; na taifa litatetereka. Lakini kwanini tuangamize taifa kwa sababu ya woga wa watawala kuhojiwa, kupingwa, na kukosolewa? ITAENDELEA…

Like
47

Leave a Comment

Your email address will not be published.