Alama zisizofutika za Maswali Magumu – 004

Maswali Magumu na vyama vya siasa vidogo vidogo

Yalikuwepo masuala mengi mazito yaliyosababisha mijadala na uchambuzi mzito. Lakini haya machache yameteuliwa ili yawe msingi wa hoja zinazoibuka katika kitabu hiki. Bila woga wala upendeleo, niliandika na kuchambua matukio haya kwa makala nzito, nikielekeza hoja zangu kwa rais moja kwa moja. Katika kipindi hiki, makala ya Maswali Magumu ilipata umaarufu mkubwa. Siku moja, kiongozi mmoja mwandamizi wa chama kikubwa cha siasa, aliniambia, “nimekutana na Abdulahman Kinana, (ambaye baadaye aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM), akasema kuwa makala za Maswali Magumu za Ngurumo zimekuwa na nguvu katika masuala ya kitaifa kuliko baadhi ya vyama vya siasa vidogo vidogo.”

Maswali Magumu, Hull City, na vikao vya Ikulu

Siku nyingine nikiwa nchini Uingereza, wakati najiandaa kurejea Tanzania, nilitembelewa na Mbelwa Kairuki, ambaye alikuwa amejiunga na masomo ya shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara katika Chuo Kikuu cha Hull, nilikokuwa. Kabla ya kwenda Hull, alikuwa msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje chini ya Dk. Asha Rose Migiro na Bernard Membe.

Tulizungumza mengi. Mojawapo ninalokumbuka katika mengi tuliyozungumza ni kwamba, “nyumbani Tanzania, Jiji la Hull linafahamika sasa kwa mambo mawili – timu ya soka ya Hull City, (ambayo ilikuwa imeingia katika Ligi Kuu ya Uingereza kwa mara ya kwanza), na Maswali Magumu ya Ansbert Ngurumo.”

Aliporejea nyumbani kutoka masomoni baada ya mwaka mmoja, aliteuliwa kuwa mwandishi wa hotuba za rais, Ikulu, kuziba pengo lililoachwa na Januari Makamba, ambaye alikuwa ameamua kuondoka Ikulu ili ajiandae kugombea ubunge katika Jimbo la Bumbuli, mkoani Tanga. Nilipata kujua baadaye kuwa pamoja na baadhi ya watendaji wa serikali, hasa wapambe wa rais, kunichukia kwa sababu ya maandishi yangu, kuna wakati watendaji wa Ikulu walijadili baadhi ya makala za Maswali Magumu huku wakinilaumu na kunirushia maneno makali; na wakati mwingine walizitumia kuchunguza au kufuatilia baadhi ya mambo niliyoibua kupitia uchambuzi huo. Waligundua kuwa ilikuwa kazi bure kuchukia mwandishi anayethubutu kumwambia rais ukweli ambao baadhi ya wasaidizi wake wanaogopa kusema.

Maswali Magumu na mashujaa waliokufa.

Siku moja niliitwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Habari MAELEZO, nikiwa na Absalom Kibanda, aliyekuwa mhariri mtendaji wa Tanzania Daima, nikiwa naibu mhariri mtendaji. Raphael Hokororo, aliyekuwa mkurugenzi, baada ya kuzozana nami kuhusu makala zangu, mbele ya wasaidizi wake na Kibanda, alinitisha kwa maneno haya: “Ngurumo, unataka kuwa shujaa? Kumbuka kuwa mashujaa wote ni marehemu…”

Mara baada ya kutoka ofisini mwake, niliandika kauli yake katika blogu yangu. Hakunipigia simu, wala sikuitwa tena ofisini kwake, lakini baadaye Kibanda alinieleza kwamba mkurugenzi wa MAELEZO alikuwa amempigia simu kulalamikia chapisho langu kwenye blogu; kwamba nilikuwa nimeenda mbali, kwamba nilimumbua na kumchonganisha na wakubwa wake na wananchi waliosoma blogu yangu, hasa kwa kunukuu maneno makali aliyotumia kunitisha.

Maswali Magumu na wabunge, Ansbert, na Ansberta

Mwaka 2010 nilikutana na mtu ambaye alijitambulisha kama shabiki wa makala za Maswali Magumu, akanieleza kuwa amempa mtoto wake jina la Ansbert kwa kuenzi uchambuzi wa makala zangu. Mwaka 2016, nilipigiwa simu na msomaji wa magazeti, ambaye alijitambulisha kama mwalimu wa sekondari moja mkoani Geita, akasema alianza kusoma Maswali Magumu akiwa masomoni nchini Urusi.
Alisema baada ya serikali kushindwa kuwalipia ada na gharama nyingine za maisha, yeye na wenzake waligundua kuwa wakati serikali ilipowatelekeza, walitetewa na waandishi wawili kupitia gazeti la Tanzania Daima – M.M Mwanakijiji na Ansbert Ngurumo. Binafsi, sikuwa nakumbuka kama niliwatetea.

Alinieleza kuwa baadaye yeye na wenzake walilazimika kurejea nyumbani Tanzania. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhitimisha masomo yake. Alipooa na mkewe akapata ujauzito, alitamani amuite mtoto wake kwanza Ansbert, lakini kwa kuwa aliyezaliwa alikuwa mtoto wa kike, alimpatia jina Ansberta – kwa heshima ya Maswali Magumu.

Nimekutana pia na baadhi ya wanasiasa vijana – mmoja ni mbunge sasa – ambao wameniambia kuwa walipokuwa wanafunzi wa chuo kikuu, walikuwa wanasoma makala za Maswali Magumu kila Jumapili ili kujifunza mambo mengi, kupata taarifa nyeti na kuzitumia kujenga hoja; na kwamba makala zangu ziliwasaidia kujenga ujasiri. Mmoja wao aliniambia kuwa alikuwa anasoma Maswali Magumu ili kupata hoja za kuhutubia wananchi katika mikutano ya hadhara alipogombea udiwani.

Ushuhuda wa diwani ambaye ni “uzao wa Maswali Magumu”

Humphrey Sambo, Diwani wa Mbezi Dar es Salaam, anasema: “Nakumbuka nilikuwa natumikia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi, Mtaa wa Luis. Nilianza kusikia habari za magazeti yaliyokuwa yaandika mambo ya siasa. Nikasoma makala za Ansbert Ngurumo (Maswali Magumu), kipindi hicho nilikuwa hata sitaki kusikia habari za vyama, hasa vya upinzani, nikiamini kuwa vingeleta vita.

“Lakini kupitia makala za Ansbert Ngurumo katika gazeti la Tanzania Daima nikajikuta nimekuwa shabiki, mpenzi na msomaji wake. Nikaanza kujikuta natoa elimu ya uraia kwa wengine. Nikaingia kwenye ulingo wa siasa za upinzani. Nikagombea uenyekiti wa Kata ya Mbezi kupitia Chadema. Nikashinda. Sehemu zote niliposimama kutoa elimu ya uraia, niliongozwa na makala za Ngurumo. Leo mimi ni diwani wa Kata ya Mbezi (tangu 2015) ambayo naamini naitumikia vizuri. Mimi ni uzao wa siasa za upinzani niliyeibuliwa na makala za Ansbert Ngurumo na wezake wachache.”

Like
5

Leave a Comment

Your email address will not be published.