KWANINI NATOFAUTIANA NA RAIS KIKWETE KUHUSU WALIMU WA SHAHADA SHULE ZA MSINGI

BAADA ya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutoa maoni kuwa shahada ya kwanza ya ualimu iwe kigezo cha walimu wanaotakiwa kufundisha shule zetu za msingi, hoja yake imeibua mjadala miongoni mwa wananchi. Wapo wanaounga mkono na pia wanaotofautiana na hoja yake hata kama kama hawapingani naye.

Mimi ni miongoni mwa wale wasiopingana naye lakini natofautiana naye. Nilitamani kutofautiana na msimamo huo bila kuandika chochote. Hata hivyo, nimeshawishika kuandika machache baada ya Dk. Richard Mbunda kuandika makala fupi akiteteaoa hoja ya Rais Kikwete.

Dk. Mbunda anatoa hoja za kuunga mkono hoja na kushawishi Watanzania wakubali hoja hiyo. Kukubaliana na hoja ya Rais Kikwete kusingenifanya niandike chochote, lakini hoja zake za kuunga mkono hoja hiyo zinafanya kila anayeitazama kwa kina sekta ya elimu hapa nchini kudadisi hoja hizo.

Kama ilivyo sifa yake, Dk. Mbunda ni mwandishi mzuri na mjenga hoja hodari. Dk. Mbunda anasema kuwa hoja hiyo ni muhimu kisera na kwamba uamuzi wa kuwa na walimu wa shahada kwenye shule za msingi kutatusaidia leo na siku za usoni kama taifa. Anaongeza kuwa hatua hii itakwamua hali ya elimu nchini. Miongoni mwa hoja zake kuu za kutushawishi ni hizi hapa:

a) Walimu wa diploma na cheti ni waliofeli kwenye hatua zao za awali za elimu, na kwa hiyo wale wa shahada ni “vipanga.” Kwamba waliofeli wanaweza kutengeneza tu watakaofeli, na vipanga watatengeneza vipanga.

b) Watanzania wanaogopa mabadiliko. Kwamba kuwa na walimu wa shahada ni mabadiliko muhimu kwenye elimu yetu.

c) Tuondoe mafunzo ya diploma kwa walimu isipokuwa kwa mahitaji maalumu. Kuwa tuandae tu wasomi wa shahada kwani huko ndipo kwenye ubora.

d) Wasimi wa shahada wanamudu Kiingereza kuliko wa diploma na wa cheti.

e). Uzoefu wa nchi nyingine zinazofanya vizuri kielimu ni wa shahada na kuendelea.

Nafikiri, hoja za Dk. Mbunda kwa maandishi zinaonekana ni za kukubaliana na pia kuunga mkono hoja ya Rais Kikwete. Japo kwa heshima, nafikiri hoja zake ni za kukubaliana lakini hazitoshi kuunga mkono hoja husika.

RRais Kikwete anajaribu kusema kuwa tukiwa na walimu wa shahada kwenye shule za msingi tutakwamua hali ya elimu yetu. Kukubaliana naye na kuunga mkono hoja yake, ni lazima kuonesha kuwa kigezo cha walimu wa shahada kitatatua changamoto za elimu yetu ambazo ni zaidi ya walimu wa diploma au cheti.

Kwa bahati mbaya, hoja za kuunga mkono muono huo zaidi ya kuukubali tu ni kibarua kizito. Ni kwa sababu hiyo, ningependa kujadili baadhi ya hoja hizi japo kwa ufupi. Tuanze hivi.

Utamaduni wetu katika mijadala

Watanzania tumeandaliwa na kuzoeshwa kujadili masuala yetu ya kitaifa kwa mfumo wa pande mbili tu, yaani faida na hasara au ubaya na uzuri wa jambo. Kwa njia hiyo, tunalazimishwa kubaki na lolote lililopo hata kama silo linalotufaa lakini kwa sababu tu lina faida kadhaa.

Matokeo yake ni kuwa wanaotakiwa kuwajibika kunyoosha mambo wanabaki upande salama na kurusha lawama kwa wananchi kwa kutochagua lililo na faida hata kama faida hizo ni hafifu ukilinganisha na wanachostahili.

Mfano mzuri ni wa mjadala huu unaoendelea. Hoja hapa si walimu wenye shahada au diploma. Hoja hapa ni: Je, mfumo wa elimu tulionao unafaa kwa ajili ya watoto wetu? Au je, unafaa kwa ajili ya mahitaji ya mazingira yetu? Jibu ni HAPANA!

Shahada au diploma na cheti?

Kulichukulia suala la elimu kama bidhaa ambayo inaongozwa na mantiki ya pande mbili za faida na hasara nii kama mtu anayeuliza wauza magari kama anunue TOYOTA au IST!

Yaani ni kama tunaambiwa tujadili faida na hasara za kuwa na walimu wa shahada na vilevile swali kama hilo kwa walimu wa diploma na cheti na kisha tuchague walimu sahihi ni wapi.

Lakini elimu haijadiliwi kwa njia hiyo. Kuangusha mzigo wa changamoto za elimu yetu kwa walimu wa diploma na cheti ni sawa na kusema kuwa mwalikwa hakufika sehemu ya tukio kwa sababu ya viatu alivyovaa. Lakini tunafahamu kuwa mwalikwa anavaa viatu na si viatu vinavyomvaa yeye.

Kwa hiyo, tatizo la elimu ya nchi yetu haliwezi kurushwa tu kwa walimu wa diploma au cheti kama ambavyo utatuzi wake hauwezi kuwa walimu wa shahada.

Kwenye kundi sogozi la wanazuoni, waliokubaliana na maoni ya Dk. Mbunda, kwa sehemu kubwa wengi wao walionesha kuwa hilo ndio tatizo kuu la elimu yetu. Kwa nini basi natofautiana na Rais Kikwete kupitia hoja za Dk. Mbunda? Nina sababu.

Mosi, ni kuhusu hoja ya kuwa walimu wa diploma na cheti ni waliofeli. Hoja hii ni hatari na inafedhehesha walimu.

Mwanasosholojia wa elimu, Stephen J. Ball, kwenye makala yake ambayo imefanyiwa rejea nyingi sana ya “THE TEACHER’S SOUL AND THE TERRORS OF PERFOMATIVITY” anaonesha jinsi walimu wanavyokandamizwa, wanayodhulumiwa na kufanywa dhalili kwa hoja za utendaji wa majukumu yao.

Ball anaonesha kuwa ajenda ya utendaji bora kwa walimu imeambatana na vitisho, ubaguzi na udhalilishaji kiasi ambacho mhusika anabaki bila matumaini ya kubadili hali yake.

Kwamba kwenye mazingira hayo, mtu anakosa uhakika wa kesho yake na kwa sababu ya mifumo isiyotabirika, mwalimu anaishi bila kujua atashambuliwa na nani kesho.

Bila ya kujali mema ya mwalimu, mara nyingi haonekani kama mtu anayefanya vizuri vya kutosha. Na ni msingi huu unaoongoza hoja ya kuwa walimu wa diploma na cheti ni waliofeli. Ukweli ni tofauti.

Mfumo wetu wa elimu umekaa kimitihani

i) Walimu hawafundishi maarifa bali wanashindisha mitihani.

ii) Wanafunzi hawajifunzi maarifa bali wanatafuta kushinda mitihani.

iii) Kuvuka hatua moja ya elimu hakupimwi kwa waliojifunza na kupata elimu bali waliofaulu mitihani.

Kwenye mazingira haya, wengi hawavuki hatua moja kwenda nyingine, si kwa sababu hawakujifunza lakini ni kwa sababu hawakufaulu mitihani. Na kuishia kwao kwenye diploma au cheti cha ualimu si kipimo cha kuwa hawakujifunza.

Ipo mifano ya watu wengi ambao hawakufaulu mitihani moja kwa moja, lakini kwa sababu familia zao zilikuwa na mbadala, walipita njia zingine na wakafika hatua za juu za kielimu.

Wakafika vyuo vikuu na wakawa wasomi wakubwa, na wengine wakawa wakurufunzi wazuri. Kama wasingepata upenyo huo, nao labda wangeishia ngazi ya diploma au cheti cha ualimu au chini ya hapo. Kwa hiyo, haiwezi kuwa kweli kuwa hao wa diploma ni watu waliofeli.

Aidha, kwa sababu ya fursa kupanuka, idadi ya wanaofika vyuo vikuu imeongezeka. Wakati zamani ufaulu ulikuwa na maana ya kusoma shule au vyuo vya serikali, sasa kumbe hata kusoma shule na vyuo binafsi ni kufaulu.

Haina maana kuwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu sasa walifaulu mitihani ya kidato cha sita kwa daraja la kwanza kama ilivyokuwa huko nyuma kwa sababu ya nafasi finyu.

Kama firsa hiyo isingekuwepo, hao wangejikuta kwenye diploma na tungewaita waliofeli. Kwa hiyo sasa, “kushinda mitihani hakujaongezeka kwa maana ya kale, bali uwanja umetanuka zaidi na wanaoingia vyuoni wameongezeka.”

Kadhalika, wanafunzi wengi kwenda vyuo vikuu kusoma ualimu imekuwa matokeo ya ufadhili wa serikali kwa njia ya mikopo. Miaka michache nyuma, vijana wengi walikwenda ualimu si kwa sababu ya kufaulu sana bali kwa sababu ya mkono wa serikali kuongeza walimu. Bila hivyo, hao wengi wangekuwa na diploma na tungewaita waliofeli.

Muhimu zaidi, wengine ni wahanga wa changamoto za kiuchumi. Wazazi wengi waliamini kuwa watoto wakisoma ualimu wa cheti au diploma wangepata ajira haraka na kusaidia katika kukwamua uchumi wao. Walitumaini kuwa vijana wao wangeweza kujiendeleza wakiwa kazini. Hawa si waliofeli bali wahanga wa uchumi.

Kimsingi, hali hii ipo karibu sekta zote sasa. Wazazi wanataka watoto waende kusoma diploma au cheti kwa sababu za kiuchumi, si kwa sababu ya kufeli.

Kwenye mazingira haya; hoja ya kufeli inaweza kuwa na maana kama kuna walimu wa diploma au cheti waliofeli mitihani ya ualimu na bado wakapata kazi za ualimu.

Ualimu ni matokeo ya masomo ya ualimu na si matokeo ya vidato. Kama ambavyo wahasibu ni wahasibu kwa matokeo ya uhasibu na si kwa sababu ya kidato cha sita, kama mawakili walivyo mawakili kwa sababu ya matokeo ya uwakili; kwa nini walimu wapimwe kwa vigezo pandikizi?

Ukweli ni kuwa, hawa wenye shahada wanafika hapo kwa kushinda mitihani badala ya kujifunza. Wanaokwenda diploma na cheti wanapita huko kwa sababu wanashindwa mitihani na si kushindwa kujifunza. Kwa maana ya elimu za awali, walimu wa diploma, cheti au shahada kama zilivyo kada nyinginezo wanafika hatua hizo bila kuwa wamejifunza.

Kwa ujumla, mfumo wetu wa elimu unahitaji mabadiliko badala ya kuchagua kundi la waathirika wa mfumo huo na kuwadhulumu hadhi zao.

Pili, si kweli kuwa Watanzania wanaogopa mabadiliko. Hoja ni mabadiliko ya aina gani. Mabadiliko yanayolenga kuhifadhi mfumo wa elimu uliochoka, si mabadiliko hitajika na kuyahoji hakuwezi kuwa ni kuogopa mabadiliko bali uhitaji wa mabadiliko ya kweli.

Kuwa na walimu wa shahada katika shule za msingi hakujibu hoja kuu tatu zifuatazo:

i) Umuhimu wa elimu

Kama dhana kuu ya elimu ni ajira, tutabaki na mfumo wa elimu unaokanyaga utu wetu. Watu wataendelea kushindana katika “kushinda mitihani” ili wapate ajira bila kuwa wamejifunza juu wanachokifanya au wanachosema wanajua.

ii) Walimu wanahitaji rasilimali zaidi ya elimu yao ili kuwa wabunifu darasani

Walimu wazuri hutokana na mazingira bora kazini na nje ya kazi, mafunzo kazini na uhakika wa kutodhulumiwa hadhi zao.

iii) Mazingira bora ya watoto kujifunzia

Mazingira bora ya watoto kujifunzia yanaboresha si tu mazingira ya mwanafunzi kujifunza lakini pia kazi ya mwalimu kufundisha.

Mfumo wetu wa elimu una changamoto lukuki kwenye maeneo haya matatu muhimu. Kuwa na walimu wa shahada hakuondoi matatizo haya kama ambavyo hayajaletwa na walimu wa diploma au cheti.

Tatu, kuondoa daraja la cheti na diploma ni kujenga zaidi mfumo wa elimu unaoondoa utu wetu.

Hivi wanaojenga hoja hii hawajui jinsi gani mfumo wetu wa elimu bado haujaachana na kasumba za ukoloni?

Mfumo wa elimu yetu kama ulivyokuwa wakati wa ukoloni, unajibu mfumo wa kiuchumi uliovunjikavunjika ili kukidhi matakwa hafifu ya uchumi huo.

Kuondoa walimu wa diploma na cheti ni kujitia upofu kuhusu uhalisia huu. Kutumia walimu wa shahada ambao ni matokeo ya mfumo huo ni kuendeleza mfumo wenyewe na siyo kuubadili.

Kuchagua kuwaangushia walimu wa cheti na diploma madhila ya mfumo huu, ni sawa na kuishi upande hasi wa filamu ya STEPFORD WIVES, ambapo watu wanatakiwa kutojali kuhusu uhalisia na tunu za ubinadamu na kuishi kwenye dunia ya kufikirika.

Hata hivyo, mjadala kuhusu elimu yetu na uchumi unahitaji muda wa kutosha.

Nne, hoja ya lugha ya Kiingereza kwenye eneo hili imejielekeza vibaya.

Mimi naamini kuwa hatuwezi kuwa na mfumo wa elimu unaopuuza lugha ya Kiingereza kama tunavyotaka kuaminishana, walau kwa sasa. Kwa upande mwingine, nafikiri kuwa kusema walimu wa shahada wanamudu vizuri Kiingereza kuliko wale wa cheti na diploma na kwa hiyo iwe sababu ya kuondoa level hiyo ya elimu, ni sawa na kula matunda ya mti wenye sumu ukijifanya kuwa huwezi kufikiwa na sumu hiyo.

Kwa mfumo.wetu wa sasa, si sahihi kwamba watu wenye shahada ndio waliofunzwa lugha ya Kiingereza vizuri. Kwenye mafunzo ya shahada siko wanakojifunza kumudu lugha hiyo pia. Kwa hiyo, walimu wa shahada na diploma kama zilivyo kada nyinginezo, wana matatizo yanayoelekeana ya lugha hii kutokana na msingi waliojengewa katika elimu ya msingi na sekondari.

Tano, ni uzoefu wa nchi nyingine.

Hoja ya kuwa nchi zilizoendelea kielimu zimefika hapo kwa kuwa na walimu wa shahada kwenye elimu za awali ni hoja ya kuchagua kipi cha kusemea badala ya kujadili mfumo mzima wa elimu wa nchi hizo kama kitovu cha mafanikio hayo.

Japo ni kweli kuwa kiwango cha elimu ya walimu kimekuwa sehemu ya mmatokeo ya mafanikio kwenye nchi hizo, si kweli kuwa hoja hiyo ni ya msingi. Kimsingi, walimu wa shahada kwenye nchi hizo ni matokeo ya mfumo ulioboreshwa na si kinyume chake.

Nchi nyingi zinazotolewa kama mifano hapa nchini, kama Finland au Australia, zimefika hapo kwa sababu kadhaa zifuatazo:

i) Mfumo bora wa elimu umekuwa matokeo ya mfumo bora wa uchumi.

ii) Mfumo wa elimu ni wa kujifunza badala ya kushinda mitihani.

iii) Mazingira ya kujifunza na kufundishia ndiyo yanavutia walimu kwenye mifumo yao.

Hoja hizi tatu bado zimepinda hapa kwetu. Mazingira haya yakiwa bora, hoja ya walimu wenye elimu kubwa kwenye shule za msingi itakuwa inajipa yenyewe na hakuna atakayeipigia kelele.

Hitimisho

Kama asemavyo Paul Freira kwenye kitabu chake cha PEDAGOGY OF THE OPPRESSED, mwalimu kuwa kwenye kitovu cha elimu bila mfumo mzima wa elimu kukidhi mahitaji ya jamii husika, ni sawa na mnyonge anayejifunza kwa picha ya yule anayemkandamiza.

Freira, kwenye mada ya kwanza kabisa ya kitabu chake, anasistiza juu ya ukombozi wa njia za ufundishaji. Anasema kuwa njia hizi ni lazima ziwe zijibu matakwa ya jamii. Kwenye mada ya pili anasistiza juu ya nadharia za elimu.

Kusema kuwa walimu wa shahada ndio wenye kufaa kwenye shule za msingi hata kama mfumo wenyewe umekorogeka, ni sawa na kusadiki ile dhana ya elimu ambayo Freira anaiita “Banking Model of Education,” kwamba walimu ni washirika active kwenye mfumo wa elimu na wanafunzi ni washirika passive; kwamba kazi ya mwalimu ni kuingiza kila liwalo kwenye “kifaa” kinachoitwa mwanafunzi.

Mapendekezo ya walimu wenye shahada kwenye shule zetu za msingi kwa maana ya hali ya sasa si hoja ya mabadiliko bali hoja ya kukwepa wajibu wa kushughulika na mabadiliko hitajika ya mfumo wa elimu yetu.

Mjadala wetu unahitaji kuwa kwenye mfumo mzima wa elimu ndani ya uchumi wetu na si matokeo ya mfumo ambayo tungependa yawe ya mfumo uliomarika katikati ya mfumo uliokorogeka.

Ni mwalimu gani wa shahada anayependa kufundisha akitokea kwenye zile nyumba za walimu?

Ni mwalimu gani wa shahada anayependa kufundisha kwa malipo yale ya walimu?

Ni mwalimu gani wa shahada anayependa kufundishia kwenye ofisi zile za walimu?

Ni mwalimu gani wa shahada anayependa kufundisha kwenye mazingira yale ya usimamizi wa elimu?

Ni mwalimu yupi wa shahada?

Like
3