Magufuli amejenga kwenye msingi mbovu ulioachwa na Mkapa – 006

Baada ya marais Ben Mkapa na John Magufuli, na wapambe wao, kusoma andiko lililotangulia kuhusu “uzi mwembamba unaounganisha Mkapa, Kikwete na Magufuli – 005,” walikerwa na uwasilishaji wangu wa kumbukumbu hizi za kihistoria zinazowagusa, na walijadili mambo kadhaa kuhusu mwandishi huyu wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu, Ijumaa mbili zilizopita. Nafanyia kazi mazungumzo yao, huku nikiendeleza mjadala huo juu ya uzi mwembamba unaowaunganisha. 

KATIKA mfumo wa utawala wa Tanzania, urais au uwaziri si ufalmeau umalkia. Ni utumishi. Kwa kuwa tumekubaliana kuishi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, tunalazimika kufuata kanuni za mfumo wenyewe. Tuvumiliane.

Bahati mbaya tuliyonayo, wakati mwingine tunajikuta chini ya watu ambao hawakujiandaa au hawakuandaliwa kuongoza, au waliandaliwa lakini hawakuandalika. Kwa mfano, Benjamin William Mkapa alipochukua fomu kugombea urais katika mchuano ndani ya chama chake, gazeti la Uhuru, linalomilikiwa na CCM liliandika kama vile halikuamini kilichokuwa kimetokea: “Mkapa naye achukua fomu.”

Kwa sababu hiyo, wapo waliosema, “kumbe hata chama chake hakikumtarajia.” Walimuona kama msindikizaji. Lakini walisahau kwamba, kwa fursa ambazo Mkapa alikuwa amepewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais Ali Hassan Mwinyi – akiwa afisa tawala; mhariri mkuu wa gazeti la serikali; balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Kanada, na Marekani; waziri wa habari, waziri wa sayansi, teknolojia na elimu ya juu; waziri wa mambo ya nje, mwandishi wa Rais Nyerere, na nyinginezo; kwa elimu na upeo wake, Mkapa alikuwa ameandaliwa.

Mwaka 1993, wakati vyama vingi vya siasa vilipokuwa vimepata usajili wa kudumu, huku siasa za mageuzi zikiwa zimepamba moto, nilitumwa na kuishi kijijini Butiama kwa Mwalimu Nyerere, kwa wiki kadhaa. Moja ya majukumu yangu ilikuwa kuandaa kwaya kwa ajili ya ibada ya kutabaruku Kanisa la Parokia ya Butiama, ambalo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilijenga kwa heshima ya Mwalimu Nyerere ambaye kabla ya hapo alikuwa anaenda kusali Parokia ya Zanaki.

Mwalimu Nyerere alikuwa na utaratibu wa kusali misa kila siku. Wakati ule, Butiama ilikuwa imeshapewa hadhi ya parokia. Paroko wa kwanza, ambaye ndiye alisimamia ujenzi wa kanisa, alikuwa Padri Karol Schlakta kutoka Poland. Mwalimu Nyerere alikuwa na ratiba ya kwenda shambani asubuhi. Misa ilikuwa saa 10 jioni. Ukiondoa siku ambazo alikuwa nje ya Butiama, Mwalimu Nyerere hakuwahi kukosa misa siku yoyote.

Siku moja nikiwa na shemeji ya Mwalimu Nyerere, aliyeitwa Dolores Nyerere (Mama Pendo) ambaye alikuwa mke wa Joseph Nyerere (wote ni marehemu sasa), kukawa na mjadala kuhusu uchaguzi mkuu wa 1995. Kumbuka hapo ilikuwa mwaka 1993.

Mama Pendo alimwambia mwenzake: “Mimi naona Mkapa anafaa.” Sisi wengine tuliona kama Mama Pendo alikuwa anaota ndoto za mchana. Hatukumbishia, wala hatukumkubalia. Tulibaki kumshangaa kwamba huyu katoka wapi na jina la Mkapa!

Nilikumbuka kauli hiyo ya Mama Pendo miaka miwili baadaye nilipokuwa nyumbani kwa Mwalimu Nyerere tena, nikiambatana na wageni wake watano – wawili kutoka Poland, watatu kutoka Musoma. Walikuwa viongozi wa dini ambao Mwalimu alikuwa amewaalika kwa chakula cha jioni. Kilikuwa kipindi cha mchakato wa urais ndani ya CCM mwaka 1995, na walikuwa wamebaki wagombea watatu – Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa, na Cleopa Msuya – wakisubiri mkutano mkuu wa kuteua mgombea.

Wageni wake walikuwa wanadadisi kujua Mwalimu Nyerere alikuwa anamtaka nani. Mwalimu alisimulia jinsi ambavyo, katika mkutano wao wa NEC, Halmashauri Kuu ya CCM, walikuwa wamechuana vikali. Alisema: “Pale Dodoma tumeshinda pesa za bangi. Sisi tumo ndani tunajadiliana namna ya kupata mgombea bora, kule nje ya ukumbi kuna watu wana pesa za bangi wanatafuta rais. Nafurahi kwamba tumewashinda…”

Mwalimu Nyerere hakuwa anataja majina ya wagombea. Alitaja tu baadhi ya kauli zao. Kwa mfano, alisema: “Kuna mgombea wetu mmoja, anasema kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe. Ala! Hivi anadhani huu umaskini walionao watanzania wamejisababishia? Na kazi ya kiongozi ni ipi?”

Kwa kujua kilichokuwa kinaendelea, tulielewa alikuwa anamsema Msuya. Na pale pale baadhi yetu tukajua huyo si chaguo la Baba wa Taifa. Askofu Justin Samba alikuwa miongoni mwa wageni wake. Katika hali ya udadisi na kuchochea mjadala, akachombeza:
“Lakini Mwalimu, naona huyu wa kati huyu ana nafuu…”

Mwalimu Nyerere akajibu haraka: “Ndiyo! Ben, ana integrity (uadilifu) kubwa sana…” Hakufafanua. Kesho yake, Mwalimu Nyerere alikuwa anakwenda Croatia kusuluhisha mizozo ya kisiasa, akiwa mwenyekiti wa South-South Commission. Alisema kuwa angejitahidi kurudi mapema ili amsaidie Rais Mwinyi kwenye kikao cha uteuzi wa mgombea.

Akasema: “Wakati mwingine nawaza, bora niwaachie siasa zao, niendelee kulima mahindi na maharage. Lakini nikiwaachia wakavuruga nchi mahindi yenyewe nitayauza wapi? Maana sera watakazotengeneza ndizo zitaelekeza masoko yetu yaweje… Sioni umuhimu wa kushiriki siasa za wenzetu Ulaya, halafu nishindwe kusaidia chama changu kupata mgombea mzuri.”
Katika mazingira haya, hata kama Mkapa hakuwa amepewa maandalizi rasmi ya kuwa rais, Mwalimu Nyerere alimtaka. Kauli za Mwalimu Nyerere na Mama Pendo ni sehemu ya ushahidi huo.

Baadaye sana mwaka 2012, nilipata fursa ya kumsikia Rais Mkapa mwenyewe (akiwa mstaafu) akisimulia jinsi alivyofanya uamuzi wa kugombea urais. Alisema kuwa baada ya kuwa na nia hiyo, aliona ni vema kwanza amjulishe Mwalimu Nyerere, ili kupata maoni yake (baraka) kabla hajachukua fomu.

Anasema hakutuma mtu, wala hakupiga simu. Aliandika barua kwa kalamu ya wino, akaifunga kwenye bahasha, akasafiri nayo hadi Butiama, akamkabidhi Mwalimu Nyerere mkononi. Yaliyofuata ni historia. Kwangu, huu ni ushahidi mwingine kwamba Rais Mkapa hakuzuka tu, wala Mwalimu Nyerere hakumpigania hivi hivi.

Hata hivyo, nadhani Mwalimu Nyerere – katika roho yake ya kijamaa – hakuwahi kufikiri kwamba Mkapa aliyemjua angeweza kuwa shabiki wa sera za kibepari. Alimuona ni mjamaa mwenzake ambaye angeweza kuwa tumaini la kurejesha sera zake (Nyerere) na kulinda baadhi ya misingi ya Ujamaa na Azimio la Arusha lililokuwa limeuawa na serikali ya awamu ya pili. Kama binadamu wengine wote, Mwalimu alidanganyika.

Maana, siku ya mazungumzo ya Butiama niliyotaja hapo juu, katika wagombea hao watatu, mtu ambaye Mwalimu Nyerere hakumgusia kabisa, ni Kikwete. Kwa mbali, alimsema Msuya kama nilivyoeleza hapo juu, bila kumtaja jina.
Kwa kuwa aliyekuwa ametoa kauli hiyo yenye ukakasi ni Cleopa Msuya, na kwa kujua nguvu na ushawishi wa Mwalimu Nyerere katika mchakato huo, tulijua kuwa kinyang’anyiro kilikuwa kimebaki kati ya watu wawili – Kikwete na Mkapa – ingawa chaguo la Mwalimu lilishajulikana.

Ni Mwalimu huyu huyu aliyekuwa kiongozi wa kwanza kumkosoa Rais Mkapa alipoona serikali inaelekea asikotarajia. Hakujali mapenzi yake na jitihada alizotumia kumpitisha na kumpigania kwenye kampeni. Alijali mustakabali wa nchi.

Hakuona mantiki ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kushindanishwa na benki kubwa kutoka nchi za nje; na baadaye kuuzwa kwa makaburu wa Afrika Kusini. Alihoji, “NBC inaweza kufungua tawi Washington au London?” Alijua maana ya mfumo mpya wa siasa za vyama vingi; na mianya inayoweza kutumiwa na watu wanaojikomba kwa rais, kumdanganya, kumhujumu, kumpotosha au kuibia taifa.
Alitambua kuwa katika mfumo unaoongozwa na kizazi kilichokulia katika vitisho na nidhamu ya woga ya siasa za chama kimoja, tena chenye viongozi waliokuwa wamegoma kuruhusu mfumo wa vyama vingi, wanahitajika watu jasiri wa kuuliza maswali magumu, na kukosoa watawala kila zinapoonekana dalili za ukengeufu.

Baba wa Taifa hakuwa mtu wa maswali mepesi mepesi, na hakukubaliana na visingizio vya “tuwape muda kwanza.” Akiwa mstaafu, alitambua kuwa kuzuia ni bora kuliko kuponya, na kwamba wanaosifu makosa ya rais wanamharibu, na wanaharibu nchi. Bahati mbaya, alifariki dunia kabla swali lake halijajibiwa.

Mwalimu Nyerere hakutaka serikali iuze viwanda au mashirika ya umma hovyo hovyo kama ilivyofanya. Katika mawazo yake ya kijamaa, hakuanzisha mashirika haya kwa ajili ya watu wachache, bali kwa ajili ya “kuhudumia” wananchi maskini.

Nilipomsikia kwa mara ya kwanza John Magufuli, akiwa mgombea urais, anazungumzia kutengeneza “Tanzania ya viwanda,” akilini mwangu nilijua anasumbuliwa na dhambi yake na wenzake iliyowasukuma kuua, kugawa, na kuuza viwanda na mashirika ya umma zaidi ya 400. Walitenda dhambi hiyo kwa sababu ya kutosikiliza washauri na wakosoaji. Walisikiliza ushauri potofu na sifa za wapambe wao.

Kwa bahati mbaya au nzuri, yanapotajwa mafanikio ya serikali ya Rais Benjamin Mkapa, miongoni mwa mafanikio yanayotajwa, ni kuendeleza sera ya soko huria aliyorithi kwa mtangulizi wake, Rais Ali Hassan Mwinyi; kuuza mashirika ya umma kwa watu na makampuni binafsi; kuvutia wawekezaji walete mitaji na kuwekeza hapa nchini.

Sera za Rais Mkapa zilisifiwa na Shirika la Fedha Duniani na Benki ya Dunia. Imani ya “wahisani” iliyokuwa imepotea chini ya Rais Mwinyi, ilirejea. Kwa kauli yake mwenyewe, Rais Mkapa alikuwa anajitapa kuwa “sasa tunakopesheka.”

Katika utawala wake, kwa jitihada za watu na mashirika mbalimbali, Tanzania ilifanikiwa kufutiwa madeni makubwa ya nje. Wapenda michezo wanakumbuka kuwa hata Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na Daraja la Mkapa, ni miongoni mwa miundombinu ya kisasa inayoakisi kumbukumbu nzuri za utawala wake.

Iwapo atapenda kujibu swali langu la mwaka 1998: “Rais Mkapa unajivunia nini?” kwa kuchepuka na kukwepa muktadha wa swali na uchambuzi wenyewe kuhusu suala la rushwa, anaweza kutaja mafanikio hayo na mengine. Wakati anaondoka, kwa mujibu wa mrithi wake, uchumi wa nchi ulikuwa umeimarika kiasi, na akiba ya fedha za kigeni ilikuwa ya kutosha miezi kadhaa ya mwenzake kuanzia kazi.

Ni kweli, hakuondoka madarakani bila mchango kwa taifa, lakini ameacha urathi (legacy) unaoendelea kusumbua warithi wake na wananchi. Bado ana maswali ya kujibu. Kwa mfano, Wazanzibari hawajapona vidonda vya Januari 26 na 27, 2001, vilivyosababishwa na watawala kung’ang’ania madaraka, hata kwa gharama ya damu ya wananchi.

Yamejirudia mara mbili, Oktoba 2010 na Oktoba 2015; wapinzani wakaepusha shari kwa kususia uchaguzi wa marudio Machi 2016. Na kama mwaka 2010 Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa amegombea urais wa Muungano kupitia Chadema, alivyokataa kuingiza vijana barabarani ili kudai kura zake, akihofia serikali ingeua raia wengi, ndivyo 2015 Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Ukawa – Umoja wa Katiba ya Wananchi – uliojumuisha Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, alivyogoma kutumia “mafuriko yake” kudai kura zake halali zitangazwe.

Dk. Slaa na Lowassa, kwa nyakati tofauti, “walisingizia damu” wakaacha kudai kura zao. Walijua kuwa damu ya raia ingemwagwa, maana watawala walishajipanga hata kwa kununua magari ya bei mbaya, yenye kutumia maji ya kuwasha, ili waumize wananchi, badala ya kutumia fedha hizo kununua madawati. Ni kweli kwamba uamuzi huo wa Dk. Slaa (2010) na Lowassa (2015) uliumiza wafuasi wao na kuathiri mno harakati za upinzani zilizofuata baadaye.

Ndivyo na Maalim Seif Sharif Hamad, aliyegombea urais Zanzibar kupitia CUF, alivyofanya. Iwapo angetumia ngangari ya mwaka 2001, damu ingemwagika, na taifa lingepata vidonda vipya visivyotibika. Mwaka 2001, kwa ubabe wa Rais Mkapa, Tanzania, ambayo imekuwa inasifiwa duniani kote kwa kuhifadhi wakimbizi, nayo ilizalisha wakimbizi. Ubabe wake ulileta aibu kwa taifa. Na katikati ya aibu hii, kuna wananchi waliokuwa wanampigia makofi, wanashangilia maslahi ya muda mfupi, wanampotosha rais.

Rais Mkapa alikuwa na kaulimbiu ya “uwazi na ukweli.” Lakini hakuwa muwazi wala mkweli. Serikali yake ilisaini mikataba mibovu “gizani.” Na wengine wanasema kipindi hicho ndipo nchi iliuzwa rasmi kwa wawekezaji. Hata serikali za Kikwete na Magufuli, licha ya tambo za kwenye vyombo vya habari, zimeendelea kusaini mikataba gizani.

Ubabe wa Rais Mkapa ulipalilia ukatili wa polisi. Tabia ya polisi wa IGP Omar Mahita; ya IGP Said Mwema; na ya polisi wa IGP Ernest Mangu na IGP Simon Sirro, iliasisiwa Ikulu wakati wa Rais Mkapa.

Kwa kuwa ndiye alikuwa rais wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi, alipaswa kujenga mazingira salama kwa demokrasia ya vyama vingi. Ndiye alipaswa kufuta sheria 40 kandamizi zilizotajwa na Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu Francis Nyalali mwaka 1991.

Kama Rais Mkapa angesikiliza wapinzani, kama angeheshimu waandishi wa habari, wachambuzi na wakosoaji wake, ndiye angepatia nchi katiba mpya ambayo bado Watanzania wanaendelea kupigania.

Kilichomshinda Rais Mkapa katika miaka 10 (1995-2005), ni kile kilichofanywa na Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini katika miaka minne tu (1994-1999). Ndani ya miaka minne, Mandela alitengeneza taifa jipya, akawezesha upatikanaji wa katiba mpya, akashiriki kuongoza kama mtangulizi, akaachia wenzake, akapumzika.

Kwa sababu ya kazi nzuri ya Rais Mandela, ndiyo maana tumeshuhudia, Rais Thabo Mbeki akipumzishwa kabla ya kipindi chake kuisha. Na Rais Jacob Zuma, mmoja wa warithi wake, aliburuzwa mahakamani kujitetea dhidi ya tuhuma za ufisadi akiwa bado Ikulu.

Ingawa Rais Magufuli alikuja na ilani ya kuanzisha mahakama ya mafisadi, na baadaye akatangaza kuianzisha, kwangu mimi, lengo lake haliwezi kutimia iwapo katiba itaendelea kulinda marais waliofanya ufisadi, eti wasishitakiwe kwa makosa waliyotenda. Kinachoonekana ni kwamba mahakama hiyo ilianzishwa kisiasa ili itumike kuumiza wale ambao watakosana na watawala.

Kama Rais Mkapa angeacha msingi huo, tusingekuwa tunasikia kauli za rais anayeingia madarakani akiwaahidi watangulizi wake kwamba, “nitahakikisha nawalinda mpunzike salama.” Ulinzi pekee wanaostahili wastaafu ni utumishi wao uliotukuka. Kwa upenyo huu, ipo siku nchi itapata rais jizi ambalo litakomba hazina yote na kugawia ndugu zake, au kuitapanya litakavyo, na hakuna lolote tutakalomfanya kwa kuwa katiba na sheria, vikibaki hivi bila kubadilishwa, vinalinda udhaifu huo.

Hata kitendo cha rais kugomea mabadiliko ya katiba ni kielelezo cha utovu wa uadilifu unaofanana na aina ya katiba iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Rais anayechukia ufisadi lazima awe rais anayetamani katiba ndiyo isimamie vita dhidi ya ufisadi. Ufisadi haupigwi vita kwa hisia au uamuzi binafsi wa rais.

Rais Mkapa alikuwa na fursa ambayo hakuitumia. Aligoma kutikisa misingi ya urais wa kifalme, unaoambatana na vitisho na hofu; akalea mazingira ya udikteta unaoanza kusumbua nchi. Urais wa Mkapa kwa kutisha wakosoaji ulijaza watu hofu; ukazaa chuki za kiitikadi, na umezaa na kulea ubabe wa marais wengine, hasa Rais Magufuli, ambaye akiwa waziri walishirikiana kuuza nyumba za serikali.

Na kama waliouza nyumba hizo hawatafikishwa mahakamani, basi mahakama hiyo haitakuwa ya mafisadi, bali ya mahasidi ambayo itatumika kuumiza na kutesa mahadisi wa rais.

Kama Rais Mkapa angeacha misingi ya kukuza demokrasia, Rais Magufuli asingeona kwamba mifano ya maraisi wa kuigwa ni Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda. Nasema haya kwa sababu, katika siasa za Tanzania, ninapomsikiliza na kumtazama Rais Magufuli naona kivuli cha marais waliomtangulia, hasa Rais Mkapa.

Kwa kuwa hatujaweka misingi imara ya kitaifa katika katiba, kila utawala wa awamu mpya ya serikali unapoingia madarakani, unaanzisha mipango kana kwamba nchi imepata uhuru jana – jambo ambalo hata Rais Mkapa amelilalamikia katika kikao kimojawapo nje ya nchi –  na hata rais anatishia kufuta baadhi ya mambo mema ya watangulizi wake ili aweke ya kwake kwa sababu za kisiasa.

Ni kwa sababu anatumia udhaifu wa kimfumo alioachiwa na watangulizi wake. Bado marais wetu hawajengi taifa. Wanajenga awamu zao za utawala wa nchi.

ITAENDELEA…

Like
19

Leave a Comment

Your email address will not be published.