TRA: MIFUMO IMARA IMESAIDIA KUONGEZA KODI

MAMLAKA  ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mifumo imara waliyoianzisha imesaidia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari za mitandao ya kijamii Dar es Salaam leo Mei 29, 2024, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi na Mawasiliano kwa umma, Hudson Kamoga amesema kwa miaka mitatu iliyopita ya Rais Samia Suluhu Hassan, TRA imeongeza mapato kutoka trilioni 18 mwaka 2021/2022 hadi trilioni 24 mwaka 2022/2023.

Amesema mafanikio hayo yamechagizwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na Watanzania kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari kupitia utoaji elimu unaofanywa na TRA.

Kamoga ameongeza kuwa TRA imeimarisha mifumo yake ya ukusanyaji kodi ambapo mambo mengi kwa sasa yanafanyika kupitia mifumo ya kidigitali badala ya ukusanyaji wake wa kawaida ambayo ilikuwa inawachukua muda mrefu kukusanya mapato.

“Katika mazingira ya namna hii mambo mengi yamerahisishwa na watu wamekuwa na hiari ya kulipa kodi na ukwepaji wa mapato umepungua kwa kiasi kikubwa sana na tunatarajia ifikapo mwezi wa 8 mwaka kesho kutakuwa na mfumo maalum ambao utapunguza kwa kiasi kikubwa ukwepaji wa kodi,” amesema Kamoga.

Baadhi ya washiriki wa semina

Vile.vule, amezungumzia utaratibu maalumu wa kufuatilia ulipaji kodi bila shuruti kwa kutenga muda maalum wa ukaguzi wa ukwepaji kodi mitaani.

“Utaratibu wa kufuatilia kama wafanyabiashara wanalipa kodi bila shuruti, nakwa sasa tuna kampeni ya mlango kwa mlango ikiwa ni pamoja na kujua changamoto za mteja, tukigundua mtu hatoai lisiti, hana mashine ya EFD lakini anafanyabiashara, hatutampa muda maalum wa lini tunakwenda kumkagua, tunatamani kila mfanyabiashara kuitikia wito wa mheshimiwa rais wa kulipa kodi kwa hiari,” amesisitiza Kamoga

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Mitandaoni (JUMIKITA), Shaaban Matwebe amesema huu ni wakati wa taasisi za serikali na binafsi kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii.

“Digital Platform ni dunia, haikwepeki unaweza kuwa na ‘Followers’ (wafuatiliaji) 50,000 lakini ukiweka tangazao linaweza kuonekana na watu zaidi ya hao. Ikitokea taasisi imewatambua watu hawa kama mlivyofanya TRA basi amejua ukubwa wetu lazima tumpongeze,” amesema Matwebe.

Aidha baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki semina hiyo, walitoa ushauri kwa TRA kuboresha mazingira ya utoaji huduma ili yawe rafiki kwa mlipa kodi.

Semina hiyo ya siku moja imeandaliwa na TRA kwa kuwashirikisha waandishi wa habari za mitandaoni ambao ni wanachama wa JUMIKITA. Elimu iliyotolewa ni pamoja na umuhimu wa matumizi wa mashine za kielekroniki, uchumi wa kidigitali pamoja na utaratibu wa uondoshaji mizigo maeneo ya forodha.

Like
2