MSIGWA AU SUGU: NANI AMEKUSHAWISHI?

Nukuu shindani:

1.”Suala la Magufuli, alilianzisha Msigwa kama turufu yake kuwa aligoma kwenda Ikulu kwa sababu ya uaminifu wake kwa Chadema. Sugu akasema, alikuwa mwoga, alitakiwa kumkabili Magufuli na kumweleza ukweli abadili msimamo. Eneo hili lilimvuruga Msigwa kupita kiasi.”

2.”Kwa ujumla hoja za Msigwa zilijawa na takwimu,  ukuu na ufafanuzi, huku akizishibisha kwa kuzungumza kwa hisia na vitendo (subliminal communication) zinazowavuta zaidi watazamaji.”

BAADA ya mdahalo uliofanyika tarehe 25.05.2024 kwenye kituo cha Star TV ukikutanisha Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi (Sugu), wanasiasa wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaowania nafasi ya mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, yamejitokeza maoni, uchambuzi, na tafakuri kuhusu “nani zaidi.”

Andiko hili ni sehemu ya uchambuzi huo  kutoka kwa waandishi wawili tofauti; kila mmoja akichambua mdahalo kwa stadi zake. Kila mmoja ameweka hitimisho la kubeba mgombea aliyevutiwa naye. Mchambuzi wa kwanza anatumia lugha ya mchezo wa soka kulinganisha karama na hoja za wagombea. Anasema Msigwa ni beki (mlinzi) na Sugu ni straika (mshambuliaji). 

MSIGWA NA SUGU: VITA YA BEKI NA STRAIKA

KAZI ya straika ni kushambulia na kufunga, wajibu wa beki ni kuzuia mashambulizi na kudhibiti magoli. Mdahalo wa wagombea uenyekiti Kanda ya Nyasa (CHADEMA), Joseph Mbilinyi “Sugu” na Peter Msigwa, ukiutafsiri kimichezo, ilikuwa vita ya straika na beki. Nitafafanua.

Msigwa, ni mwenyekiti anayewania kutetea nafasi yake. Sugu, anaona Chadema Nyasa wanahitaji mageuzi, na yeye ndiye turufu ya mabadiliko ya kimsingi. Walikutanishwa Star TV, katika kipindi cha Medani ya Siasa, ili wanadi maono yao uongozi.

BONYEZA VIDEO HII USIKIE SEHEMU YA HOJA ZAO

Edwin Odemba, mwongoza mdahalo

Mwandishi wa Marekani, Ron Elving, kupitia chapisho la “It’s All About Politics” la Shirika la NPR, aliandika stadi ya kisiasa yenye jina “That’s Why Incumbents Used to Say No” – “Hii ni Sababu Waliopo Ofisini Hukataa”, ilikuwa baada ya mdahalo wa Rais madarakani, Barack Obama na mpinzani wake, Mitt Romney.

Hoja ya Elving ni kuwa waliopo ofisini, wanaposhiriki mdahalo dhidi ya wapinzani wao kuelekea uchaguzi, hujiweka kwenye mazingira magumu ya kushinda. Alitoa mifano, Gerald Ford, aliopoteza alama nyingi kwenye mdahalo dhidi ya Jimmy Carter, kisha akashindwa uchaguzi. Miaka minne baadaye, Carter naye akapigwa kwenye mdahalo na Ronald Rogan. Kadhalika, George Bush (Sr) kwa Bill Clinton.

Kutoka kwa Elving, naweza kuliweka vizuri jibu kwa nini waliopo ofisini siku zote mdahalo ni mgumu kwao; ni kwa sababu wanakuwa na mengi ya kujibu na kujitetea kuliko wanaogombea kwa mara ya kwanza. Hiyo ndiyo sababu Msigwa, alikuwa beki zaidi, akikosa fursa ya kushambulia, wakati Sugu alishambulia bila kuwa na mzigo wa kujibu.

Bahati mbaya kwa Msigwa, mwanzo mpaka mwisho, hakuwa na vitu vya kuonesha ambavyo angeweza kusimamia kama alama ya uongozi wake, zaidi ya kusema “amejenga watu.” Hao aliosema amewajenga, mtu maarufu ni Jessica Kishoa, ambaye ni miongoni mwa wabunge 19 wa Chadema, wenye mgogoro na chama hicho.

Mgombea anayetetea nafasi yake, kwa kawaida hutakiwa kutambia kwanza aliyofanya. Msigwa alikuwa na maelezo ya jumla bila kuainisha chochote ambacho kinashikika, alichokifanya. Kisha, akabanwa kuhusu kutojenga ofisi ya Chadema Kanda ya Nyasa kwa miaka 10 ya uongozi wake. Kuwaita nyumbu wanachama wenzake wa Chadema. Kukinzana na misimamo ya Chadema, hususan suala la Serikali kuhamisha wananchi Ngorongoro.

Halafu, ikaibuliwa tuhuma nzito kuwa Msigwa akiwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, alipopigiwa simu kujumuika na wananchi Mbarali, Mbeya, ili asikilize changamoto zao, aliomba kwanza apewe pesa. Hili Msigwa alilijibu kwa ukali kuwa ni majungu.

Upande wa Sugu, alisema alikuwa na agenda 10. Bahati mbaya, ratiba iliwekwa vibaya. Haikumpa fursa Sugu kueleza kwa ufasaha agenda zake.

Pamoja na kutopata nafasi pana ya kujieleza, bado aliweza kujijenga kupitia yale ambayo yalianishwa kama kasoro za kiuongozi katika uongozi wa Msigwa, ambaye alikosa uvumilivu na kujikuta anajibu hata kabla mwongoza mada hajamruhusu. Haya aliyokuwa anafanya Msigwa ni rafu. Ni kawaida mabeki kucheza rafu kudhibiti mashambulizi au kuzuia magoli. Msigwa alikaba zaidi.

Joseph Mbilinyi (Sugu)

Shida kubwa ya Msigwa ni kuwa ana uwezo mkubwa wa kuyasema matatizo, ila huwa hatoi majawabu. Hili lilijionesha hata pale Msigwa alipoulizwa swali kuhusu mpango wake wa kuwasaidia wananchi wa Kanda ya Nyasa kwenye kilimo. Msigwa alizitaja fursa zilizopo na kulalamika kukosekana kwa uongozi mzuri, ila hakueleza kile ambacho atafanya.

Upande wa Sugu, alipoulizwa, naye alianza kwa kulalamika kuwa sera mbovu na siasa kuongoza kilimo ndiyo tatizo kubwa. Hata hivyo, alijinasibu kuwa amekuwa akihamasisha kilimo cha biashara, akasema ana ziara Marekani Juni 2024, inayoandaliwa na ubalozi wa Marekani Tanzania, ambayo moja ya agenda ni kuwaunganisha wakulima wa Nyasa na Marekani, lengo likiwa kutanua fursa zaidi.

Kuna swali liliulizwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Solomon, alimtaka Msigwa kueleza mambo gani ambayo hajayafanya Nyasa ili akipewa nafasi ayafanye. Kama kawaida yake, Msigwa alizunguka bila kujikita kwenye majibu ya swali husika. Mwongoza mdahalo angekuwa thabiti kutaka maswali yajibiwe kama yalivyoulizwa, Msigwa angepata tabu sana.

Kama alivyoandika Elving, mdahalo siyo kitu cha kukimbiliwa na waliopo ofisini, maana hujikuta wakihitaji kujitetea zaidi, wakati wanaowania ofisi kwa mara ya kwanza, wakiwa na mengi ya kushambulia. Pointi hii imekuwa dhahiri kwa Msingwa na Sugu. Msigwa alikuwa na wakati mgumu, Sugu alikuwa na utulivu, akajenga hoja, kisha akashambulia.

Kwa mfano, kipindi Msigwa akituhumiwa kuwa hutaka fedha kwa wananchi ili aende kusikiliza changamoto za wananchi, halafu Sugu naye akasema Msigwa haaminiki ndani ya Chadema, kwamba angekutana na Rais John Magufuli, angeweza kuyumba na kusaliti chama. Sugu alitumia maneno “kuuza mechi”. Eti, Msigwa angeuza mechi!

Maneno hayo yalimuumiza sana Msigwa, akahoji, “mimi siaminiki?” Sugu akasisitiza, “huaminiki.”

Suala la Magufuli, alilianzisha Msigwa kama turufu yake kuwa aligoma kwenda Ikulu kwa sababu ya uaminifu wake kwa Chadema. Sugu akasema, alikuwa mwoga, alitakiwa kumkabili Magufuli na kumweleza ukweli abadili msimamo. Eneo hili lilimvuruga Msigwa kupita kiasi.

Yote kwa yote, mdahalo wa Msigwa na Sugu ni kielelezo cha kutanuka kwa demokrasia na ukuaji wa nguvu ya kisiasa nchini. Kila lenye heri kwa wote, wanapojielekeza kwenye uchaguzi Mei 29, 2024.

Wagombea wakiwa katika picha ya pamoja na mwongoza mdahalo na baadhi ya wafuasi wao waliokuwa studio kushuhudia mchuano huo.

Mchambuzi wa pili analalia kwa Msigwa, akidai kuwa alimgaragaza Sugu. Ana hoja zipi?

NAMNA MCH. MSIGWA ALIVYOTEKA MDAHALO.

1. Msigwa alitokea katika vazi rasmi la kiuongozi na linaloendana na aina ya tukio husika.  He appeared presentable. Mtoko wa Msigwa ulionyesha uzoefu wake kwenye Public Speaking. Anajua vazi lipi huvaliwa wapi kwa wakati gani. “First impression matters.” Tofauti na mpinzani wake aliyetokea kwenye vazi kama ameenda kushiriki tuzo za muziki.

2. Msigwa anaifahamu Katiba ya CHADEMA, anajua kwamba chama kinaongozwa kwa mujibu wa katiba na maamuzi yanafanywa kwa mujibu wa katiba. Hii ni sifa muhimu kwa mgombea.

3. Msigwa alikuwa bora katika kufafanua kauli zake na misimamo yake iliyozua gumzo. Kwa mfano, Msigwa anasema: ” Maasai ni Watanzania wenye haki ya kuishi Ngorongoro lakini mtindo wao wa kimaisha haukidhi tafsiri ya indigenous group kwa mujibu wa UN Charter.” Watu wengi hata hatukua tunajua kama kuna tafsiri ya UN juu ya indigenous groups.

4. Msigwa hakujikita katika mipasho na mzaha bali alijikita kueleza mitazamo yake kama kiongozi, tofauti na mpinzani wake.

5. Msigwa anasema: “CHADEMA ni chama cha demokrasia na kuwa na maoni tofauti ndiyo demokrasia yenyewe.” Hii inaonesha kujiamini kwa kiongozi lakini zaidi inaonesha kwamba Msigwa anajua anakitumikia chama cha kidemokrasia.

6. Msigwa anakifahamu chama  anajua ili CHADEMA Kanda ya Nyasa ishinde uchaguzi wa serikali za mitaa inahitaji kuwa na wanachama wangapi na wagombea wangapi kwa kuwa na takwimu za idadi ya vijiji, vitongoji, mitaa na wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, jambo ambalo mpinzani wake halifahamu.

7. Msigwa anafahamu uchumi wa kilimo wa wananchi wa Kanda ya Nyasa.  Kwa mfano, anasema: “27% ya pato la watu wa Nyasa linatoka kwenye kilimo, huku magunia 73 kati ya 100 ya mahindi yanayozalishwa hapa nchini yanazalishwa mikoa ya Kanda ya Nyasa.” Kwa takwimu hizi unaona Msigwa ni kiongozi anayejibidiisha kufahamu mambo yayoihusu Kanda ya Nyasa na maisha ya watu wa kanda yake.

Wagombea wakisalimiana ukumbini kabla ya kuanza mdahalo

8. “Dhana ya Uongozi Mgomba.” Msigwa anasema kazi mojawapo ya kiongozi ni kuzalisha viongozi wengine, kulea na kuwafundisha. Msigwa amethibitisha ubora wake katika kulea viongozi wachanga na vijana kwa kuwataja kwa majina viongozi aliowalea kama vile Fakii Lulandala, Joseph Lyata, Jesca Kishoa, Rose Mayemba, Jackson Mnyawami, nk.jambo ambalo mshindani wake alishindwa kujipambanua nalo.

9. Msigwa ameweka msimamo bayana kupinga rushwa, huku mshindani wake akihalalisha rushwa kwa kuwatuma wakapokee rushwa kama watapewa. Inaonyesha hajui kama anahamasisha uvunjifu wa sheria za nchi na anawatuma wanachama wenzake kwenye mtego wa kunaswa na sheria za jinai.

10. Msigwa kaonesha kuwa na uelewa mpana wa mambo mengi kuliko mpinzani wake.  Hili linathibitishwa na uwezo wake wa kufanya marejeo mbalimbali kutoka kwa wasomi nguli na wanafalsafa nguli duniani.

11. Msigwa amethibitisha kutoogopa kuongea mambo ambayo wengi hawapendi kuyasikia, akisisitiza matumizi sahihi ya akili katika kufikiri na kufanya maamuzi na hii ndiyo zawadi kubwa zaidi ambayo Mungu amempa  mwanadamu – zawadi ya UTASHI.

12. Msigwa wakati wote aliongea mambo kwa kichwa chake, huku akiitazama hadhira yake bila kutegemea kusoma kwenye makaratasi au simu. Tofauti na mpinzani wake ambaye wakati wote alionekana akisoma kwenye simu na notes zilizoandaliwa mapema.

Kwa ujumla hoja za Msigwa zilijawa na takwimu,  ukuu na ufafanuzi, huku akizishibisha kwa kuzungumza kwa hisia na vitendo (subliminal communication) zinazowavuta zaidi watazamaji.

Naongeza sentensi ndogo mwishoni:

Kila mtu anaweza kuwa Mwanasiasa, lakini sio kila Mwanasiasa anaweza kuwa Kiongozi. MSIGWA ni Mwanasiasa na Kiongozi.

Uchambuzi huu ni maoni binafsi ya waandishi. Hawakutaka kutumia majina yao ili kuepuka mgongano wa kimaslahi. Maoni yao si msimamo wa SAUTI KUBWA. Ni juu ya msomaji kujenga hitimisho lake kwa kuzingatia ushawishi wa hoja.

Like