Ni gharama kuwa na Ikulu tatu, ni hatari kuwa na Ikulu tatu, ni mgogoro kuwa na Ikulu tatu

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alihama Ikulu ya Magogoni akaenda kuishi Msasani, lakini kazi aliendelea kufanyia Ikulu, katika ofisi ya rais, Magogoni.

Kwa kauli zake za mara kwa mara, hakuipenda Ikulu ile hata kama alipaita “mahali patakatifu.” Kisiasa alipaona kama kumbukumbu ya ukoloni. Hakuona fahari kukalia kiti na kulalia kitanda alicholalia mkoloni.

Katika awamu zilizofuata, marais wamekuwa wanaishi na kufanyia kazi Ikulu ya Magogoni. Hata hivyo, ni Baba wa Taifa aliyeanzisha hoja ya kuhamishia makao makuu ya nchi kwenda Dodoma – kwa sababu alizotoa.

Hakuna kumbukumbu ya wazi ikiwa Rais Nyerere aliwahi kuapisha mteule wake yeyote nje ya Ikulu Magogoni au kufanya dhifa ya kitaifa kwa wakuu wa nchi nje ya Magogoni.

Zipo kumbukumbu za wageni ngazi ya mawaziri wa kigeni au wageni maalum waliotumwa ujumbe maalum wakamkuta Mwalimu Nyerere ama Butiama au Msasani.

Wakati mwingine, wageni kama hao walimfuata akiwa ziarani mikoani. Kwa wakuu wa nchi, alilazimika kurudi Magogoni. Tendo moja kuu la kihistoria alilofanya Mwalimu nje ya Magogoni ni kutangaza kuingia vitani na Uganda. Alitangaza akiwa Songea. Alitaka kujenga utamaduni kuwa Ikulu ni sehemu nyeti.

Hivi sasa tukubali tuna mgogoro wa kisiasa na kikatiba. Kama vyombo vyetu vya habari vingekuwa huru, pamoja na mihimili mingine, tungeweza kuwa na mjadala mpana juu ya kinachoendelea nchini. Wana taaluma, bunge, asasi za kiraia na majukwaa mengine vingehoji tuna Ikulu ngapi?

Lakini kwa sababu vyombo hivi vinaishi katika zama za hofu, si ajabu siku hizi kuona watu ambao wangeibua maswali ndio wanajipanga kutetea – tena kwa hoja dhaifu – makosa ya rais.

Awamu ya tano ilitangaza kuhamia Dodoma. Kabla hata ya uhamaji kukamilika tukaona shughuli za kiserikali zinafanyika Chato. Waziri Mwigulu Nchemba ni mmoja wa wateule wa kwanza wa rais kuapishiwa Chato, nyumbani kwa rais. Na vikao nyeti kama Baraza la Usalama la Taifa, Baraza la Mawaziri, mapokezi ya wakuu wa nchi na vikosi vya gwaride vikaanza kufanyikia Chato.

Katika hali ya kushangaza kidiplomasia, hata mawaziri wa kigeni wakaanza kupatiwa mapokezi ya hadhi ya wakuu wa nchi wanapotua Chato. Chato imechukua kiwango kipya hata kama haijatamkwa na sheria kuwa ni Ikulu yetu.

Kama Chato si Ikulu basi ni nyumbani kwa Rais wetu. Kwa kuwa Rais ameendelea na kazi akiwa Chato, ichukuliwe kuwa Rais anafanyia Kazi nyumbani kwa sababu maalum. Vinginevyo, kama yuko likizo na Ikulu yetu ni Dodoma, tungetarajia makamu wa rais awe Dodoma apokee wageni wa kitaifa.

Na endapo wageni wangependa kufika Chato kumsalimia Rais wetu “aliye likizo,” basi wangeenda baada ya shughuli iliyowaleta. Utaratibu wa sasa unatuchanganya na kuchafua itifaki ya kitaifa.

Ikiwa Rais amehamishia Ikulu Chato kwa muda kwa sababu maalumu (usalama au afya), sababu hizo zinawahusu pia wafanyakazi wengine. Kwa hiyo, wafanyakazi waruhusiwe kufanyia kazi zao nyumbani kama rais anavyofanyia kazi zake nyumbani. Ni gharama kuwa na Ikulu tatu, ni hatari kuwa na Ikulu tatu na ni mgogoro kuwa na Ikulu tatu. Ikulu tatu ni ishara ya kuwa na marais vivuli watatu.

Hali hii isipuuzwe kwa sababu inaleta ombwe. Baadhi ya maamuzi yanachanganywa, na baadhi ya watendaji wanachanganyikiwa namna ya kufanya.

Wapo watumishi wa Ikulu ambao hawapo Dar, Dodoma wala Chato, na wanadai kuwa wapo kazini. Humo katikati wamo mawaziri wanaojifanya kutenda kazi katika kila wizara (super ministers) na wanawakoga wenzao kwa kudai kuwa wanachoamua wao ndicho rais anakwenda nacho. Urais wetu sasa umegawanywa kama keki.

Lipo na jingine. Fuatilieni. Tayari kuna “mashindano” ya kila waziri kupendekeza kitu wizarani kwake kiitwe jina la rais, huku mawaziri wengine wakiwapa majina ya rais watoto waliowazaa na “nyumba ndogo.” Ni dalili ya jahazi kwenda mrama.

Rais amejilimbikizia madaraka na kazi nyingi, matokeo yake mawaziri vimbelembele wamepora yale yanayomponyoka. Zipo na tarifa za mmoja ambaye ameamua kukalia kiti cha rais huko Chamwino kwa kisingizio cha “kutafuta document Ikulu.”

Pamoja na kuongozwa na katiba, serikali huongozwa pia kwa kufuata mila na desturi za serikali zilizojengwa kwa muda mrefu.

Misingi ya taifa hili ilijengwa na Baba wa Taifa. Hatujengi misingi mipya. Yeyote anayebomoa misingi iliyoachwa na Baba wa Taifa ajue kuwa tutamhoji – gizani au nuruni.

Sasa hivi kunajengeka tabia ya kupenda vyeo kupitiliza na kuvitumia kufanya lolote bila hofu au aibu ya kuhojiwa. Kila kitu kizuri kinakimbiziwa Chato kana kwamba ni eneo maalumu kuliko mengine yote nchini. Tuseme kweli; haya ni matumizi mabaya ya madaraka. Ni ufisadi. Ni ulimbukeni tunaopaswa kuukemea.

Rais wa Ethiopia Salhe Work Zewde akisalimiana na Rais Magufuli alipowasili nchini katika ziara ya kikazi Chato jana
Like
5