Tanzania yatakiwa iache kumtesa Zara mwanaharakati wa Australia

SERIKALI ya Tanzania imetakiwa kuacha “kumtesa” na kumwachia haraka mwanaharakati Zara Kay, raia wa Australia, aliyekamatwa, kuhojiwa na vyombo vya usalama jijini Dar es Salaam tangu Desemba 28, mwaka jana.

Taarifa zinaeleza kwamba Zara alikamatwa siku hiyo na Polisi kwa tuhuma za “kumdhihaki Mtume,” kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii akiwa Dar es Salaam, lakini baadaye kosa hilo lilibadilika katika mahojiano na Polisi na kuwa “kumiliki pasipoti ya Tanzania kinyume na sheria.”

Zara ambaye alizaliwa Tanzania miaka 29 iliyopita, ni raia wa Australia anayeishi London, Uingereza. Ni mwanaharakati anayepinga wasichana kulazimishwa kuvaa hijabu akitumia zaidi mtandao wake wa faithlesshijab.org kuhimiza kuheshimika kwa uhuru wa kila mtu, hasa wasichana wa Kiislamu kufanya wanachotaka bila kulazimishwa; ikiwamo kuvaa hijabu.

Miongoni mwa taasisi za kimataifa zinazotaka kuachwa haraka kwa Zara ni pamoja na Jumuia ya Taasisi ya Kimataifa za Walioacha Uislam kutoka UingerezaMarekani, Ufaransa, Canada, Australia, India, Sri Lanka, Uturuki, Morocco, Mali na nchi zingine.

Kupitia taasisi hiyo ya kimataifa, nchi hizo zinataka Zara kuachiwa mara moja na kurejeshwa kwa pasipoti yake ya Australia ili awe huru kusafiri na kurejea Uingereza ambako hufanya shughuli zake.

Sambamba na taasisi hizo, serikali ya Australia imeeleza kufuatilia shauri la Zara na kuiomba Tanzania “kulimaliza mapema.”

Tangu kukamatwa kwake mwaka jana, Desemba 28, mwaka jana, Zara amemaliza siku 29, akihangaikia haki yake Polisi ambako pasipoti zake zimeshikiliwa.

Zara “alihifadhiwa” na baadaye kuhojiwa na Polisi kwa muda wa saa 32 kabla ya kuachiwa siku iliyofuata kwa dhamana ya Polisi. Aliamuriwa kuripoti Polisi kila baada ya wiki moja.

Taarifa za awali zilizotolewa na Zara mwenyewe na taasisi zinazotaka aachiwe haraka zilieleza kwamba mwanaharakati huyo huenda alikamatwa kutokana na misimamo yake ya kutaka kila mwanamke awe huru na kwamba mwaka jana, mwezi Mei, akiwa London, aliandika kwenye mtandao wa Twitter kuhusu kudorora kwa haki za binadamu nchini Tanzania.

Hata hivyo, serikali ya Tanzania imekanusha tuhuma hizo na kueleza kwamba Zara anashikiliwa kwa kukiuka sheria za uhamiaji.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Simon Sirro amesema kuwa Zara anaendelea kushikiliwa kwa kuwa bado anahojiwa na Idara ya Uhamiaji na kuhimiza kuwa “hakuna hoja yoyote inayohusu uanaharakati wake.”

SAUTI KUBWA imeelezwa na Kamishina wa Uhamiaji, Uraia na Pasipoti wa Tanzania, Gerald Kahiga kwamba Zara anaendelea kuhojiwa na suala lake liko mbioni kukamilika ili hatua stahiki zichukuliwe.

Zara aliyeingia Tanzania Septemba 6, mwaka jana na kupewa viza ya siku 60, ambayo iliisha Desemba 5, 2020, hata hivyo iliongezwa hadi Januari 20, mwaka huu.

Imebainika kuwa Zara alipewa pasipoti ya Tanzania Namba AB100678 Desemba 31, 205 ambayo iliisha muda wake Desemba 30, 2015. Hata hivyo, aliomba na kupewa pasipoti mpya Namba AB652209 Julai 31, 2014 ambayo ingeisha Julai 30, 2024.

Pamoja na kuwa na pasipoti ya Tanzania, Zara pia anamiliki pasipoti ya Australia Namba PA8029098 iliyyotolewa Julai 24, 2018 ambayo bado haijaisha muda wake na kwamba ndiyo aliyoingia nayo nchini.

Sheria za Tanzania zinaonesha kwamba ikiwa Zara atapatikana na hatia ya kutoukana uraia wa Tanzanaia wala kurejesha pasipoti yake, atahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh. 500,000.

Zara
Like