Msiba wa Magufuli: Watanzania wakesha mitandaoni, TBC washindwa kupiga Wimbo wa Taifa

DAKIKA chache baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kutangaza kifo cha Rais John Pombe Magufuli, Watanzania waliibuka na kuanzisha mijadala kadhaa kupitia mitandao ya kijami, huku wengine wakitumia simu kuwataarifu ndugu na jamaa zao.

Katika video fupi iliyorekodiwa awali, Samia aliutangazia umma wa Watanzania kuhusu kifo hicho, na taarifa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii saa 5:00 kamili usiku Machi 17, 2021.

Samia alisema Rais Magufuli alifariki dunia jana jioni saa 12 jioni Machi kutokana na maradhi ya moyo.

Baada ya video hiyo kuanza kusambaa kwenye mitandao watu walianza kufuatilia ili kupata uhakika zaidi wa taarifa hizo kupitia Televisheni ya Taifa (TBC).

Hata hivyo, katika hali ambayo hai haikutarajiwa, TBC hawakuwa wamejiandaa au hawakuandaliwa kutangaza tukio hilo kubwa la msiba wa kitaifa kwani muda huo waliendelea kupiga nyimbo za dini kwa muda mrefu tofauti na ilivyotarajiwa kwamba muda huo wangekuwa wanapiga wimbo wa Taifa kuashiria msiba huo mkubwa wa Taifa.

Aidha, katikati ya nyimbo hizo za dini, TBC walijiunga moja kwa moja na video ya Mama Samia kuhusu kifo hicho huku pia wakishindwa kuwasiliana na vituo vingine vya televisheni kwa kuwapa mawasiliano ili wote wajiunge na kutangaza msiba huo kwa pamoja.

Siku za maombolezo zazua mjadala.

Baada ya tangazo la makamu wa rais kuhusu siku 14 za maombolezo, mjadala wa kisheria na kikatiba uliibuka, baadhi ya watu wakidai kuwa kiongozi huyo amekiuka sheria kuhusu utaratibu wa vifo vya viongozi wa kitaifa.

Mmoja wa wachambuzi, Salim Hussen, wa Dar es Salaam, alisema siku za maombolezo kwa kiongozi mkuu wa nchi ni 21.

“Ibara ya 8 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la kiingereza imetaja siku 21 za maombolezo, Sasa hizi huenda ni busara lakini mama huenda ameshauriwa vibaya au ametumia busara tu, ni vema sheria na katiba vifuatwe hususani nyakati kama hizi” alisema huku akisisitiza kuwa tabia ya kukiuka katiba yamekuwa mengi, japo hayapaswi kuzoeleka.

CHADEMA wasitisha mkutano na waandishi wa habari.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilikuwa kimepanga kufanya mkutano na waandishi wa habari leo asubuhi lakini kiliusitisha baada ya habari za kifo cha Magufuli kutangazwa.

Kupitia tangazo rasmi la Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, mkutano huo na vyombo vya habari utafanyika siku nyingine.

Aidha Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ametangaza siku 21 za maombolezo na bendera za chama hicho nchi nzima zitapepea nusu mlingoti.

Video ya Lema.

Baadhi ya wanasiasa na wanaharakati waliatu walisambaza video inaonyesha Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akistabiri kifo cha Rais John Magufuli. Katika video hiyo, Lema anamtaka Magufuli abadilike, aache tabia za ukatili katika uongozi wa nchi.

Lema alitoa kauli hiyo mwaka mmoja baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani mwaka 2016.

Like
2