Kifo cha Magufuli kitufundishe thamani ya maisha – Mbowe

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema kifo cha Rais John Pombe Magufuli kinatukumbusha thamani ya maisha ya mwanadamu.

Mbowe aliyasema hayo jana, Machi 18,2021 kwenye salamu za rambirambi za Chadema kufuatia kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kilichotokea juzi Machi 17 2021 saa 12 jioni katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ya Chadema iliyosainiwa na Mbowe mwenyewe kwa umma pamoja na mambo mengine ilitoa pole kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, mke wa marehemu, Mama Janeth Magufuli, familia pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuondolewa na kiongozi aliyepo madarakani.

Mbowe alisema pamoja na kwamba nchi ipo katika wakati mgumu wa majonzi ma maombolezo ya kitaifa, kifo hicho kinatukumbusha na kutufundisha thamani ya maisha, upendo katika kutenda yaliyo mema wakati wa uhai hapa duniani.

“Tunapoendelea na maombolezo tukitumie kipindi hiki kama taifa kufungua ukurasa wa kulirejesha taifa kuwa moja na lenye kulinda na kuheshimu uhuru, haki, utu, utawala wa sheria, demokrasia na maendeleo ya watu. alisema Mbowe na kuongeza kuwa:

” Ni imani yetu kuwa Rais ajaye Mama Samia Suluhu Hassan atalinda misingi hiyo na ataongoza taifa kufikia maridhiano ya kitaifa.

Katika salamu hizo za rambirambi, Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema Chadema kinaamini kwa kuwa Mama Samia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba atalipatia taifa Katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi.

Aidha Mbowe alitoa wito kwa kwa wenye mamlaka ya kisheria kuheshimu na kulinda matakwa ya sheria na Katiba wakatu huu ambao taifa linapita katika kipindi kigumu cha mpito.

Like
2