Mikopo ya kihuni ndiyo inayokuza deni la taifa

Na Gift Mathayo

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha takwimu za ongezeko la deni la taifa, ikisema kuwa takwimu sahihi ni shilingi bilioni mbili (2,000,000,000 )za Kitanzania badala ya bilioni 12 zinazozungumzwa. Kanusho hilo lilitolewa Jumamosi tarehe 19 Mei 2018. Siku hiyo hiyo, msemaji wa serikali, ambaye pia ndiye msajili wa magazeti, alitoa tamko ambalo aliliita ONYO dhidi ya gazeti la Mwananchi, kwa kile alichoita upotoshaji wa habari kuhusu deni la taifa. Kwa mara nyingine, serikali inahangaika kutengeneza  propaganda za kisiasa kwa kutumia taasisi za umma kuhusu jambo linalogusa maslahi na maisha ya wananchi.

Mwezi uliopita, katika sakata la upotevu wa Sh. 1.5 trilioni ambazo hata mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali  (CAG) alionyesha kuwa hazionekani zilipo, walipobanwa wakadanganya bunge kwa maelezo yasiyokubalika kimahesabu na yasiyoendana na mwenendo wa kibajeti. Hatimaye, Ikulu nayo iliandaa “igizo” maalumu la kuwataka  CAG na katibu mkuu wa wizara ya fedha waseme hadharani mbele ya vyombo vya habari na rais “iwapo pesa hizo zimeliwa.” Kama ilivyotarajiwa, wote walijibu, “hapana, hazijaliwa.”

Kwanini ni igizo? CAG ndiye alionyesha kwenye vitabu vyake kuwa pesa hizo hazijulikani zilipo. Rais anapomwita Ikulu kumhoji hadharani aseme kama “zimeliwa,” mbele ya vyombo vya dola, anakuwa amemweka mtegoni. Hicho nacho ni kitisho cha wazi. Na katika ukweli wote, CAG hajawahi kusema popote kuwa “zimeliwa.” Alisema hazijulikani zilipo. Kwa hiyo, kitendo cha rais kumtaka aseme kama zimeliwa au la ni igizo ambalo wenye akili walielewa shabaha yake kwa kuwa hata kabla ya kuulizwa, kuna watu walishajua kwamba angeulizwa kwa kuwa ndiyo ilikuwa sababu hasa ya CAG kualikwa Ikulu.

Vile vile, hakuna mtu aliyetarajia Dotto James, katibu mkuu wa wizara ya fedha, aseme tofauti na alivyosema, kwani licha ya ukweli kwamba rais, aliyemuuliza swali hilo, ni bosi wake na alimpanga ajibu hivyo,  ni ukweli wa kimungu pia kwamba rais ni mjomba wake. Hata hapo wizarani yupo kimkakati kama alivyokuwa Tanroads wakati mjomba akiwa waziri wa ujenzi. Tatizo kubwa la serikali ya awamu ya tano, hasa rais mwenyewe, ni kudhani kwamba wananchi ni wajinga mno kiasi kwamba hawana uwezo wa kuchambua na kupembua kauli, mwenendo wa watawala, na masuala yanayotokea. Kwa sababu hiyo, hata kemeo la BoT na onyo la msemaji wa serikali vitapokelewa katika mazingira hayo, na wachambuzi wataendelea kuonyesha udhaifu huu.

Tukiachana na propaganda na vitisho vya serikali, ukweli halisi ni huu. Kati ya Januari na Aprili mwaka 2018 zilitolewa taarifa kadhaa tofauti kuhusu Deni la Taifa. Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha Dotto James wakati akiongea na waandishi wa habari alisema Deni la Taifa limefikia shilingi trillioni 27.04; Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akasema deni la Taifa ni dolla za kimarekani bill 25.42; halafu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)  pamoja na kuomba radhi kwa Rais alisema Deni la Taifa ni shilingi trillioni 46.08.

Mtu wa nne kuongeza utata kuhusu ukubwa wa Deni la Taifa alikuwa Waziri wa Fedha, Dk P Mpango. Siku waziri huyo alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19, alisema mpaka Desemba 2017, Deni la Taifa lilikuwa limefikia shilingi trilioni 47.756.

Kwa kuwa serikali haitaki kujadiliwa wala kukosolewa, na wanaokosoa huitwa vibaraka au wametumwa na majina mengine mabaya takwimu hizi zilibaki zikijadiliwa kwenye mitandao ya kijamii. Wakati mjadala juu ya mkanganyiko huo ukipoa, Benki Kuu (BoT) wiki hii imetia chumvi katika kidonda kwa kutoa ripoti ya mwelekeo wa uchumi kwa miezi mitatu ya kwanza mwaka huu, inayoonyesha deni hilo limeongezeka kwa zaidi ya Sh12 trilioni na kufikia shilingi trilioni 60.

Viongozi wa serikali wanapotoa utetezi wao kuhusu ongezeko la deni hujificha katika shimo linaloitwa uhimilivu wa deni. Hata wataalamu wanasema hivyo hivyo. Mathalani vyombo vya habari vimemkariri Mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Repoa, Dk Blandina Kilama akisema suala la msingi kwenye Deni la Taifa ni uhimilivu wake.

“Mikopo ya muda mrefu ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo si vibaya kwa kuwa Serikali inakuwa na nafasi ya kuilipa huku ikiendelea kutoa huduma za jamii kama kawaida. Mikopo ya muda mfupi ndio mibaya kwa kuwa huhitaji fedha nyingi zinazoweza kuathiri uwezo wa Serikali,” alisema mtafiti huyo.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema takwimu zinaonyesha, uwiano wa deni hilo na Pato la Taifa ni asilimia 36 wakati ukomo wake ni asilimia 56, jambo linalomaanisha kuwa bado ni himilivu.

Tatizo ni uhuni katika ukopaji na matumizi. Serikali inasimamia ujenzi wa miradi mikubwa kama wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge, reli ya kisasa (SGR), na ununuzi wa ndege kwa ajili ya kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATC) lakini inasema miradi hiyo inajengwa kwa fedha za ndani.

Hadi kufikia Julai 2017 Deni la Taifa liliongezeka kwa asilimia 15 katika kipindi cha miezi 13 iliyopita, ilionyesha ripoti ya mapitio ya uchumi ya Agosti 2017 ya BoT. Deni lilifikia kiwango cha Sh53.3 trilioni kutoka Sh46 trilioni kwa mwaka ulioishia Juni 2016. Mwaka ulioishia Juni,2016 deni hilo liliongezeka kwa asilimia 20 kutoka Shilingi trilioni 38.2 zilizorekodiwa Juni 2015.

Kilichosababisha deni kukua kufikia kiwango hicho ni mikopo mipya kutoka vyanzo vya ndani na nje ukiwamo wa dola milioni 505 sawa na shilingi trilioni 1.2 ambao Serikali iliuchukua kutoka Benki ya Credit Suisse ya Uswiwi mwezi Juni.

Ukuaji wa deni hili unatisha hasa ikizingatiwa kwamba katika kila hotuba Rais John Magufuli hakosi kujigamba kwa namna alivyobana matumizi kwa kuondoa watumishi hewa, kuwafukuza kazi watumishi walioghushi vyeti, kuzuia safari za nje na kukataza semina na warsha kufanyika kwenye kumbi za hotelini.

Katika kila hotuba yake hakosi kutamba kwamba ununuzi wa ndege na miradi yote mikubwa kama reli ya SGR “inajengwa kwa fedha zetu wenyewe”. Lakini huishia kuwachanganya wananchi anapowashukuru wahisani, mashirika ya fedha ya kimataifa, pamoja na wakopeshaji wengine.

Wananchi wanachanganyikiwa zaidi BoT inapotoa ripoti inayoonyesha katika miezi mitatu deni limeongezeka kwa shilingi trilioni 12 na kufanya jumla kuwa shilingi trilioni 60. Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye ni mchumi na mfuatiliaji mkubwa wa Deni la Taifa anasema, “siku za usoni uwezo wetu wa kugharimia deni utaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi” na anatoa ushauri kwamba ni vema Bunge likachukua wajibuwa wake wa kuidhinisha madeni.

Deni la Taifa linazidi kupaaa wakati Ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017 inaonyesha matumizi mabaya ya fedha na ubadhirifu mkubwa uliosababisha Serikali Kuu kupewa hati chafu. Miongoni mwa fedha ambazo zimefisidiwa ni shilingi trilioni 1.5. Ripoti ya CAG ilionyesha kwamba serikali ilipanga kukusanya shilingi trilioni 29 lakini ilikusanya trilini 25 na ikatumia shilingi trilioni 23.5 hivyo shilingi trilioni 1.5 haijulikani. Deni la Taifa linaongezeka wakati shilingi trilioni 1.5 hazijulikani zilipo na hakuna kiongozi mwenye wasiwasi.

Fedha hizo ni karibu sawa na mkopo wa dola 505 ambao serikali ilichukua kutoka taasisi ya Credt Suisse ya Uswisi. Hata huo mkopo serikali ilidai ilikuwa inafanya mazungumzo ya kukopa dola milioni 300 lakini Zitto aliwaumbua kwa kusema siyo kwamba serikali inafanya mazungumzo bali imeshakopa zaidi ya dola milioni 500. Jiulize, kwa nini wanaficha kiasi halisi walichokopa?

Siku chache baadaye Taasisi ya Credit Suisse iliwaumbua kwa kuthibitisha kuikopesha Tanzania dola milioni 500 kwa masharti ya kulipa kwa miaka mitano na baadaye BoT ilionyesha serikali imekopa dola milioni 505.

Serikali inasema mambo yote yatawekwa wazi lakini imeshindwa kuweka wazi zilipo shilingi trilioni 1.5. Serikali inajivunia kuondoa watumishi hewa na kuwafukuza waliodaiwa watumishi walioghushi vyeti lakini ripoti inaonyesha matumizi ya mishahara serikalini katika kipindi cha 2016/ 2017 ni makubwa kupita kiasi. Serikali imetamba kubana matumizi, mfano wote wanaokwenda kutibiwa nje lazima kibali kitoke kwa Rais Magufuli, lakini ni katika kipindi hicho matumizi yameongezeka tena wengine wamepewa kibali kwa ajili ya kupandikiza mimba.

Angekuwepo Mwalimu Julius Nyerere asingevumilia kuona hali hii, angesema; angekemea. Lakini viongozi wote wastaafu wanaona, wanasikia watu wakilia na wanasoma takwimu za kutisha kiuchumi wamekaa kimya.

Like
7
1 Comment
  1. Mbongo 6 years ago
    Reply

    Kitendo cha wastaafu kukaa kimya huku huyu mwizi na muuaji akiendelea kuiharibu nchi ni cha kushangaza sana. Hali ya hii miaka miwili na nusu ni mbaya kiasi hiki ikifika 2020 hii nchi itakuwa na hali ya kutisha sana kwenye kila sekta muhimu.

    2

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.