Rais anapotosha wasaidizi wake, nao wanampotosha

MIAKA miwili na nusu inayoyoma tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, taifa letu linadidimia katika sintofahamu ya mdororo wa uchumi na mparaganyiko wa kijamii. Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli haielekei kujua chanzo cha sintofahamu zote zinazoendelea. Wanayemdhania ni adui wa serikali, kimsingi ndiye anasaidia serikali. Na wale wanaodhaniwa ndiyo wazalendo ndiyo hasa wamegeuka wasaliti na mafisadi wakubwa kwa kutumia mifumo ya serikali kujineemesha na kujilinda.

Na wale wanaodhaniwa ni watiifu na wazalendo wa taifa na serikali, ndio wanadidimiza taifa hili katika mitafaruku mingi. Kinachoonekana kutawala kwa sasa ni rais kupotosha watendaji wake, na wao kwa upande wa pili, wanampotosha rais wao. Hatimaye, rais wetu ana majibu ya kila kitu katika taifa letu. Anajifanya mwana uchumi, mwana usalama, mkurugenzi wa bandari, mbunifu wa viwanda, mhandisi wa majengo, waziri wa fedha, mratibu wa ujasiriamali wa mapapai, mtetezi wa haki za wafanya kazi, katibu mkuu wa utumishi anayejua watendaji wa halmashauri zetu wasiofanya kazi vizuri, mwana sheria nguli anayeshinda kesi mhakamani kwa amri moja, na kadhalika.

 

Wakati wa mjadala uliokufa kifo cha mende kuhusu uandikaji wa katiba mpya, pande zote ndani ya bunge la katiba zilianza kukubaliana kuwa rais ana madaraka makubwa yanayohitaji kupunguzwa na kudhibitiwa. Bahati nzuri, tume ya Jaji Warioba ilikuja kutoka kwa wananchi. Lakini mjadala juu ya hoja hii ulipopamba moto na kuelekea kupita, yaelekea kuna nguvu kutoka nje ya bunge hilo iliingilia na kurejesha nyuma mjadala huo.

Rasimu ya katiba inayopendekezwa ilipunguza kidogo sana madaraka haya. Kwa kuwa mchakato huo umekufa, hivi sasa Magufuli amemua kujipa madaraka zaidi ya yale yaliyo kwenye katiba ya sasa.

Kwa kutumia madaraka hayo, rais anapotosha watendaji wake na kukiuka katiba. Hali kadhalika, watendaji wake nao wanampotosha na kumhakikishia kuwa ana mamlaka na madaraka kufanya lolote katika nchi hii bila kuwajibila kwa yeyote. Wote, rais na watendaji wake, hawajui kuwa wanaangamiza taifa letu. Madaraka makubwa kwa rais wetu, yana madhara makubwa katika maeneo manne.
Kwanza, madaraka makubwa “yanamuua” rais mwenyewe. Hivi sasa yeye amejiona na kuaminishwa kuwa bila yeye hakuna kitu kitakachofanyika. Amefikia kuamini kuwa nchi yetu iliharibiwa na watangulizi wake kwa sababu ya kukaa ofisini na kuamini mno wasaidizi wao. Kwa hiyo, yeye anajiona yuko nje ya ofisi kuhakikisha hata mambo madogo ambayo yangefanya na wasaidizi wake, na anayafanya yeye mwenyewe. Na kwa kufanya hivyo, anaamini kuwa vyama vingine haviruhusiwi kufanya shughuli zao na bendera zao mahali popote anapopita lazima zishushwe. Madaraka haya “yanamuua” kwa sababu mwili wake una ukomo, na siky atakapokoma mambo yote yatarudi kama yalivyokuwa kabla hajawa rais.

Pili, madaraka makubwa ya rais yanaua uchumi wa nchi. Sehemu kubwa ya uchumi wa taifa letu, ilikuwa mikononi mwa sekta binafsi. Kwa hiyo, serikali ilikuwa inafaidi kwa njia ya kukusanya kodi. Ili sekta binafsi iweze kuwa na uhakika wa mitaji na uwekezaji wao, lazima rais na wasaidizi wake, waonyeshe kwa kauli na vitendo kuwa wanaheshimu umuhimu wa mali binafsi. Rais wetu wa sasa na watendaji wake wana hulka ya kutishia kufunga, kutaifisha, kuadhibu, kuharibu na hata kudhalilisha mali za watu binafsi. Matokeo yake, ama wawekezaji wanakimbia au wanafunga miradi yao. Mdodoro wa sasa wa kichumi unatokana na hali hii ambayo kiini chake ni madaraka makubwa ya rais juu ya mali za watu.

Tatu, madaraka makubwa ya rais yanaua wanyonge wale wale ambao rais huyo huyo anajidai kuwatetea. Kwa kitendo cha rais kutumia madaraka yake vibaya na kusababisha sekta binafsi kuzorota, watetezi wa haki za raia kutishiwa na vyombo vya habari kufungiwa; wanaoumia sana ni wanyonge ambao hawana pa kwenda.

Imebaki sasa mnyonge mwenye bahati ni yule anayepenya ukuta wa usalama na kutoa kilio chake mbele ya rais. Kuna watanzania wangapi ambao hawawezi kumwona rais? Ikiwa rais anatatua matatizo madogo, wasaidizi wake wilayani na mikoani, wanafanya nini? Wafanya biashara wanapofunga biashara, wanaoumia si wafanya biashara bali ni wanyonge wa chini ambao mkate wao wa kila siku ulitegemea uwepo wa biashara hizo.

Nne, madaraka makubwa ya rais, yanaandaa machafuko katika taifa. Inapotokea rais kujizungusha ukuta wa vyombo vya dola na kuonekana kuvipendelea wazi wazi na hadharani, wale ambao wamegandamizwa na vyombo hivyo au watendaji wa serikali, wanachukia na kufikia kusema liwalo na liwe. Wana usalama wanaotumika vibaya kuteka, kutesa, kuua na kuumiza bila kuwajibishwa, ni watoto wa watanzania – ukiondoa wale wa kigeni walioazimwa kwa kusudi maalum. Rais ambaye anataka tuamini kwamba alichaguliwa kwa mapenzi ya watu wanyonge, anapodumu madarakani kwa kutegemea polisi, anakuwa anaandaa wananchi kufanya maasi.
Madaraka ya rais ni kipengele kimoja cha muhimu sana kilichotumika kutufikisha hapa tulipo. Rais anatumia madaraka kuagiza mtu auawe, ateswe, agungwe, anyimwe dhamana au hata afukuzwe kazi. Lakini pia madaraka ya rais yanaweza kutumika kwa yeye kukaa kimya pale mambo mabaya yanapotendeka ili kumpendelea yeye na serikali yake. Tuliona wakati wa uchaguzi wa rais wa Zanzibar. Rais Magufuli alijificha nyuma ya kauli kwamba “hana mamlaka ya kuingilia” lakini huku akituma majeshi kumlinda kiongozi aliyeingia kwa Wii wa kura Zanzibar.

Baadaye, wananchi wamekuja kuelewa kuwa Magufuli na She in wote wameingia maarakani kiharamu.

Hali ya wananchi kukata tamaa imeongezeka baada ya wananchi kugundua kuwa, wale waliokuwa msitari wa mbele kutetea kuwa madaraka ya rais yapunguzwe katika mchakato wa katiba mpya, hivi sasa ndio wamegeuka watetezi wa madaraka hayo makubwa, na hata kupendekeza yaongezwe.

Mtetezi anapogeuka msaliti, mnyonge anakuwa hana njia nyingine isipokuwa kuasi. Profesa Palamagamba Kabudi na Humphrey Pole pole waliokuwa upande wa wananchi wakati wa mchakato wa katiba mpya, sasa wamegeuka wasaliti wanaostahili ghadhabu ya watu wanyonge wa taifa hili, kwa sababu tu wanataka kupendwa na rais.

Wanatetea usaliti na ufisadi walioupinga wakati ule, kwa vile tu anayeufanya ni bosi wao. Laana inawahusu.

Like
4
1 Comment
  1. Bichwa kubwa 6 years ago
    Reply

    Dah kaka tunakusupport waelimishe watanzania wajui nchi yao inakoelekea

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.