Kubeti: Jinamizi linalotafuna vyeti, ndoa, pesa, ubongo, na uhai

– Dar es Salaam yatia fora kwa watoto kucheza kamari
– Serikali, wazazi, viongozi wa dini wabebeshwa mzigo
– Sheria inasema kamari ni mchezo wa burudani, si ajira

NI asubuhi, saa  moja na nusu. Huko Kisukuru, Tabata, Jijini Dar es Salaam, katika familia ya Mzee Alphonce Shirima (67), inaandaliwa sherehe kwa ajili ya kumpongeza kijana wake, Meki (26), anayehitimu shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Viti vimekusanywa, meza zimepangwa, maturubai yameandaliwa, mbuzi wa kususio amechinjwa, na maandalizi ya mapishi yameanza. Ndugu, jamaa na marafiki wanajiandaa kwa sherehe. 

Mzee Shirima ameshavaa suti yake maridadi, huku mkewe anaendelea kujiweka vizuri. Ghafla, kabla hawajaanza safari kuelekea sehemu ya mahafali, anaingia Meki, mhitimu mtarajiwa. Jina lake halisi ni Melchizedeki. Usoni anaonyesha simanzi. Hana furaha.

Vijana wakiwa nje ya kituo cha kubeti Mwananyamala

Anamkaribia baba yake na kumnongoneza kuwa ana jambo muhimu la kumweleza yeye na mama yake. Mbele ya wazazi wake sebuleni, anapiga magoti, huku machozi yakimlengalenga, anawaeleza ukweli mchungu:

“Baba, samahani! Hakuna mahafali.” Mzee Shirima anashtuka kwa mshangao, na kuhoji: “Kwani vipi? Yameahirishwa?” Meki anajibu kwa unyonge: “Hapana, hayajaahirishwa. Wanafunzi wengine wote wanahitimu leo, lakini mimi si mmoja wao.” Mzee anabaki amemkodolea macho kijana wake, akisikiliza ujumbe wenye utata. Meki anaendelea: “Samahani baba, kwa kukukwaza wewe na familia, lakini hii ni siri ambayo nimeitunza kwa muda mrefu nikiogopa jinsi ya kukuelezeni. Ukweli ni kwamba nilishaacha masomo chuoni muda mrefu. Sikulipa karo yote, hivyo nilishindwa kuendelea na masomo. ….” 

Mzee Shirima anamkatiza Meki,“ lakini mbona nilikupatia fedha ya kulipia karo yote kila mwaka?” Kwa aibu na upole, huku ameinamisha kichwa, Meki anasema: “Baba, niliacha chuo nikiwa katikati ya mwaka wa pili. Pesa ya mwaka huo niliichezea kamari nikitarajia izae faida niitumie kwa ada na matumizi mengine ya chuo. Bahati mbaya, ililiwa… na niliogopa kusema. Leo ndo nimekusanya ujasiri wa kusema baada ya kuona mnajiandaa kwenda kwenye mahafali ambayo, kusema kweli, hayapo. Samahani sana…”

Simulizi la Meki na mahafali yaliyoshindikana linafanana na tamthiliya. Ni tukio lililogeuka mkuki moyoni mwa Mzee Shirima. Hata nilipokwenda nyumbani kwake Kisukuru, nilipooomba anisimulie kwa kina mkasa huu, alilengwa lengwa na machozi. Akaniomba nisimpige picha. Akavuta kiti chake na kukiweka vizuri jirani na mti wa kivuli katikati ya bustani ndogo pembezoni mwa nyumba yake.

Mara akamwita mkewe, Eufrasia, akamtambulisha kwangu. Mkewe akaondoka. Dakika chache baadaye, mkewe akaleta trei lenye vikombe viwili vya maziwa. Tukanywa na kuendelea na mazungumzo. 

Mzee Shirima, baada ya kunukuu maneno hayo ya kijana wake siku ya tukio, akasema: 

“Kauli hii ya kijana wetu haikuwa rahisi kwetu sisi wazazi kuielewa, tulipigwa ganzi, mimi na mama yake. Tulikaa kimya kama dakika 10. Nilihisi kuishiwa nguvu, nikahisi usingizi wa ghafla.  Kumbe ni presha ilishuka. Hakika ni jambo lililotukatisha tamaa.

“Hizi taarifa sikuwahi kuziweka hadharani. Zinajulikana kwa wana familia tu. Mimi na mke wangu tulikubaliana kukaa kimya na kumwachia Mungu kwa sababu zinatuumiza sana. Lakini kwa faida ya wengine, sina budi kuziweka wazi ili jamii ijue na ichukue hatua, ikibidi.

“Kinachoniumiza ni kwamba kijana wangu Meki alishindwa kufikia ndoto yake. Hiyo si kwa sababu alifeli mitihani ya kidato cha sita au chuo, bali alitumia fedha za ada na kuchezea kamari, wengine wanasema kubeti. Awali sikuelewa hili jambo kabisa.

“Meki ni mtoto wangu wa tatu kuzaliwa, akitanguliwa na kaka zake wawili Jordan na Anselm, na hawa wote walisoma na kuhitimu vizuri bila matatizo. Binti yangu wa mwisho, Salome, anasomea udaktari India. Nilijiona mwenye bahati watoto wangu wote kufika ngazi ya chuo kikuu, lakini Meki amekuwa tofauti. Ukiwa na roho ndogo utasema kuna shida nyingine.

“Sikuwahi kuwa na wasiwasi na kijana wangu. Meki havuti sigara, havuti bangi wala si mlevi wa pombe. Sijui ni shetani gani alimwingia akaingia kwenye ulevi huo wa kamari hadi akasahau masomo.

“Nakumbuka Meki alipofika katikati ya mwaka wa mwisho wa kumaliza masomo alikuja nyumbani akatueleza kuwa alikuwa ameamua kuondoka hosteli na kwamba sasa angekuwa anasoma akitokea nyumbani kwenda chuoni.

“Mimi na mama yake hatukuwa na wasiwasi wowote. Tuliendelea kumpatia fedha za kujikimu kama kawaida, na yeye alikuwa akiondoka nyumbani asubuhi na mapema akisema anakwenda chuoni. Kumbe hakuwa anakwenda chuoni bali kwenye vijiwe vya kubeti maeneo ya Mwenge na Ubungo, anarudi nyumbani jioni au usiku.

“Unajua huyu kijana wangu alikuwa amepata mkopo wa asilimia 60 kutoka Bodi ya Mikopo (HESLB) ambayo tulikubaliana aitumie kulipia ada na sisi wazazi tugharamie matumizi mengine. Hii pesa tulikuwa tunamuongezea ni kutoka kwenye bili ya maziwa ya ng’ombe wetu mmoja tuliye naye pale (anaonyesha kwa kidole zizi la ng’ombe kando ya nyumba yake)

“Sikuwahi kufika kwenye makazi yake (hosteli) isipokuwa mama yake na kaka zake ndio walikuwa wakienda siku moja moja kumtembelea na kumpelekea mahitaji mbalimbali.

Taharuki ya familia

Katikati ya simulizi, Mzee Shirima ananyamaza. Baadaye anasema hawezi kuendelea, maana moyo unauma. Anashauri kaka wa Meki, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aendelee na simulizi hili. Naye anasimulia: 

“Nilianza kupata wasiwasi baada ya kuona mdogo wangu hana furaha usiku wa kuamkia siku ya mahafali yake. Nikiwa pale nyumbani kwa mzee, nilikamilisha maandalizi, lakini usiku nilishtuka kuona mdogo wangu hana furaha. Hakuwa kama tunavyojua mtu ukiwa unakaribia kupata shahada ya kwanza, jinsi unavyokuwa ‘bize’ na maandalizi. Kwa Meki hali ilikuwa tofauti.

“Nakumbuka ilikuwa usiku wa kuamkia tarehe ambayo mdogo wangu angepokea shahada yake ya sheria. Alionekana mwenye mawazo na hata wasiwasi, muda mwingi aliutumia chumbani peke yake.

“Nilihisi kuna kitu hakipo sawa. Mawazo ya haraka yalinijia kwamba huenda mdogo wangu hakuwa na mavazi mazuri anayotaka ili apendeze. Nikamuomba anionyeshe suti aliyoiandaa..

“Alinambia suti anayo lakini ipo kwa rafiki yake Mwenge, na kwamba waliahidiana amletee asubuhi. Sikufurahishwa na kauli hiyo. Nilimfokea mdogo wangu. Nilimwambia,  ‘inawezekanaje suti ya kuvaa siku ya graduation iwe kwa rafiki yako na si nyumbani?’

“Wakati namfokea, baba alikuwa anatusikia. Alikuja chumbani kwa mdogo wangu. Alipoelezwa suala la suti, naye alihamaki. Hata hivyo, baba, kwa utu uzima, aliniita pembeni akaniambia Meki ni kijana wa kiume huenda pesa ya suti aliyompatia awali aliifanyia matumizi mengine ya anasa.

“Mzee alinipatia fedha nyingine, shilingi laki mbili, tufanye mpango Meki apate suti nyingine mpya ili turejeshe furaha yake. Usiku ule nilimpigia rafiki yangu mmoja ana duka la suti Kariakoo na Mwenge ili usiku ule tupate suti nyingine kwa ajili ya mdogo wangu. 

“Nilimwambia Meki anitajie vipimo vyake ili suti iletwe na bodaboda usiku ule. Hata hivyo, Meki alinisihi sana kwamba suala la suti halina tatizo, kwamba ana uhakika asubuhi rafiki yake angemletea, kwani walikuwa wamepanga kuvaa sare.

“Tuliachana na mambo ya kuagiza suti nyingine, na kilichotokea asubuhi yake naamini mzee amekueleza kwa kina.

“Niseme tu, nyumbani kwa mzee ilikuwa vilio. Baba na mama walipata msongo wa mawazo na mpaka leo mzee ana tatizo la moyo.

“Hata hivyo, baadaye kama familia tulikubaliana Meki ahamie Zanzibar kwa baba yetu mdogo ambaye ni daktari ili pamoja na mambo mengine aweze kupata ushauri wa kitabibu hususan upande wa saikolojia, kwa sababu alikuwa anashinda ndani bila kuonana na watu.

Mmoja wa wana familia amelieleza SAUTI KUBWA kuwa baada ya kupata tiba ya kisaikolojia kwa miaka miwili, sasa Meki anajiandaa kujiunga na moja ya vyuo vikuu vya Zanzibar kusoma tena sheria baadaye mwaka huu.

Watoto watumbukia katika kamari: Tunawanusuru vipi?

Meki hayuko peke yake. Wapo vijana wengi ambao wameathiriwa na kamari kwa namna mbalimbali. Kibaya zaidi, si vijana wakubwa tu, bali hata watoto nao wametumbukia katika janga hili.

Watoto wakishiriki kamari katika kituo kimojawapo cha mchezo huo.

Katika uchunguzi uliofanywa na SAUTI KUBWA katika baadhi ya mitaa ya Wilaya za Kinondoni na Ilala jijini Dar es Salaam, tumebaini pasipo shaka kwamba watoto chini ya miaka 18 nao wanashiriki michezo hii ya kubahatisha.

Uchunguzi wetu katika mitaa ya Mwananyamala, Kijitonyama na Makumbusho, Manzese Tip Top, wilayani Kinondoni, umebaini baadhi ya vituo vya kamari vinaruhusu watoto kucheza kamari kwa kigezo kimoja tu – wawe na pesa.

Katika mitaa ya Manzese, Tandale, Kigogo, na Mwananyamala, michezo ya kubahatisha au ‘kubeti’ ipo kwa wingi. Kila baada ya mita 20 hadi 30 kuna mashine za kubeti zilizofungwa kwenye maduka maalumu.

Mbali na vituo vya kuchezesha kamari, pia matangazo mbalimbali yanayohamasisha na kushawishi watu kushiriki michezo hiyo yamekithiri kwenye vyombo vya habari, mitaani na hata kwenye mazingira yanayozunguka baadhi ya shule za sekondari na msingi. 

Mfano mzuri ni shule za msingi na sekondari Makumbusho katika Wilaya ya  Kinondoni. Zimezungukwa na matangazo ya bahati nasibu ya BIKO yaliyotapakaa kwenye nguzo za simu, taa za barabarani, na kuta zinazozunguka eneo hilo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Minazini, Kata ya Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Zunda Deogratius, katika mahojiano na SAUTI  KUBWA alikiri kuwa mtaani kwake kuna mashine nyingi za kuchezesha kamari ambazo pia huwahusisha watoto chini ya miaka 18.

Alisema ofisi yake ina taarifa hizo, na tayari imechukua uamuzi wa kufunga baadhi ya vituo hivyo kutokana na ongezeko la watoto wa mtaa huo wanaobeti licha ya makatazo ya kisheria.

“Kituo kimojawapo tulikifunga kwa sababu ya kuchezesha kamari kwa watoto licha ya kuonywa mara kadhaa. Kipo Mtaa mdogo wa Sokoni hapa Mwananyamala. Kile tumekifunga baada ya kuona kinaendelea kuwatumia watoto, jambo ambalo ni hatari na ni kinyume cha sheria ya michezo ya kubahatisha.

“Mbali na watoto kujiingiza katika kamari kwa kujificha, imegundulika pia kuwa baadhi ya watu wazima kwenye familia wamekuwa wanawatuma watoto wao kupeleka vikaratasi walivyobashiri mpira, vijulikanavyo kama ‘mkeka,’ wavipeleke kwenye vituo vinavyochezesha kamari. Hili nalo ni kosa,” alisema Nzunda.

SAUTI KUBWA ina taarifa za uhakika kwamba kiwango ‘kinachochezwa’ na watoto ni kati ya Sh 500 hadi 1000 kwa mtu mmoja. Jumamosi na Jumapili ndizo hutumiwa zaidi na watoto kucheza kamari.

Mmoja wa wajumbe wa Serikali ya Mtaa Manzese, Hanzuruni Hassan Mshamu, alisema watoto kujiingiza kwenye michezo ya kamari kunachangiwa na wazazi kutokufuatilia watoto wao kwa kila hatua ya makuzi yao.

Alisema: “Hii michezo huwezi kuikuta sana vijijini. Hapa mjini wazazi wanahangaka kutafuta pesa na wajibu wa malezi wameiachia serikali. Wazazi wengi akishampatia mtoto shilingi 500 ya kula shuleni wamemaliza. Watoto wengine wanaamua hata kushinda njaa ili baadaye waweze kucheza kamari wapate pesa zaidi, na wengine wanachangishana fedha na wakipata faida wanagawana.”

Kwa mujibu wa vifungu Na. 47 na 70 vya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, ni kosa kisheria na ni kinyume na maadili kwa mtu yeyote aliye juu ya miaka 18 kuruhusu au kusababisha mtoto wa miaka chini ya 18 ashiriki kwenye michezo ya kubahatisha.

Mapato ya halmashauri

Mmoja wa watendaji wa kata ambaye alikataa kutajwa jina kwa maelezo kuwa hajaruhusiwa na mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, alisema sheria za Serikali za mitaa hazitambui michezo ya kubahatisha kama chanzo cha mapato kwenye halmashauri zao.

Alisema kutokana na hilo, wanashindwa kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaochezesha michezo hiyo mitaani hata wanapovunja sheria.

“Hatuna miguu ya kusimamia kisheria sisi kama wawakilishi wa manispaa, labda ikitokea watu wamepigana humo kwenye biashara ndiyo askari wetu (mgambo) wanaweza kuingilia; lakini kuhusu wanaendeshaje biashara, kanuni zinazowaongoza ziko nje ya uwezo wetu.

“Licha kwamba vituo vya kuchezesha kamari vimetapakaa kila mtaa huku kwetu, mimi sina mamlaka navyo kwa maana ya usimamizi. Hapa nina orodha ya biashara ninazoruhusiwa kisheria kuzisimamia hususan zile ambazo wanaotaka kuzianzisha sheria inawaelekeza kuanzia ofisi ya mtendaji wa Serikali za Mitaa.

“Kwa hiyo, ofisi yangu inashughulika na biashara kama vile leseni za vileo, maduka ya bidhaa mbalimbali, mighahawa, gereji na biashara nyingine zilizo orodheshwa kwa mujibu wa sheria, lakini hiyo ya kamari tunaiangalia kwa macho. Hatuna mamlaka nayo. Usajili wao unaishia huko Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) na Brela.”

Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Aquilinus Shiduki, alithibitisha hoja ya watendaji wa mitaa kwamba ni sahihi, kwani kamari ni michezo ambayo inaratibiwa na chombo kingine nje ya mfumo wa manispaa.

“Kamari ni michezo ambayo inaratibiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha na kusajiliwa na Brela. Manispaa hatuna mwongozo wowote uliotolewa na bodi juu ya usimamizi wa michezo hiyo ya kamari kwenye halmashauri zetu,” alisisitiza Shiduki.

Msemaji wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, naye anathibitisha kauli hiyo ya msemaji wa Manispaa ya Kinondoni.

“Kama watendaji wamekwambia hawahusiki na uanzishwaji wa biashara zote za kamari katika mitaa yao, wapo sahihi. Sisi kama manispaa hatuna miongozo ya biashara ya michezo ya kubahatisha kwani wana bodi yao pamoja Brela, hao ndiyo wanahusika,” alisema Tabu.

Katika mitaa ya Tabata Kimanga, baadhi ya biashara ya kamari zinazotumia mashine zijulikanavyo kama ‘dubu’ zimefungwa kutokana na sababu mbalimbali.

Kamari na usalama wa wadau

Mmoja mawakala wa kamari kupitia ‘dubu’ Rukia Hamduni Massabo alisema wamiliki wa mashine hizo ni Wachina, na wanamlazimisha kuendelea na biashara hadi saa 6 usiku. Kwa sababu za kiusalama,  alilazimika kuvunja mkataba na wamiliki hao wa mashine za kamari.

“Nimehofia usalama wangu. Wacheza kamari wa usiku mara nyingi ni wahuni na wanaweza kukubadilikia muda wowote. Nilikuwa nalipwa vizuri lakini sina amani, nimeachana nao,”alisema Rukia.

Mmoja wa wajumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Sophia ibrahimu, alisema kuwa baadhi ya vituo vimefungwa kutokana na ugomvi wa mara kwa mara, kutishiana visu na mapanga miongoni mwa wacheza kamari na wafanyakazi wa kwenye mashine hizo.

“Baadhi ya wenye nyumba,  licha ya kupata kodi kubwa kutoka kwa wenye mashine hizo ambao ni raia wa China, mkataba unapoisha wanaamua kuwafukuza kutokana na vurugu zinazotishia amani. Unakuta mtu amekuja na pesa yake nyingi tu, akishacheza zote zikaliwa anaanzisha vurugu na kutishia uvunjifu wa amani, wanakimbilia serikali ya mtaa,” alisema mjumbe huyo.

Katika sehemu inayofuata tutazungumzia mauaji yasababishwayo na kubeti.

Like
2