Rudisheni bungeni ‘Sauti ya Tarime’ – Mwalimu

NAIBU Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano limepwaya, kwa kukosa wabunge mahiri kutoka Chadema.

Amewaomba wananchi wa majimbo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini kurejesha ngome za chama hicho kwenye wilaya ya Tarime, pamoja na wabunge mahiri kama John Heche.

Heche, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aligombea ubunge Tarime Vijijini mwaka 2020, katika uchaguzi uliovurugwa na nguvu za dola, kwa kutumia majeshi kukibeba Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika hotuba yake aliyoitoa jana kwenye mkutano uliofanyika Tarime Mjini kwenye uwanja wa Shamba la Bibi na kuongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, mwanasiasa huyo wa Chadema Zanzibar, alisema historia ya watu wa Tarime ya kuipigania na kuiheshimisha Chadema ni ya muda mrefu kiasi cha kuwa chachu iliyoamsha vuguvugu la mabadiliko katika maeneo mengine nchini.

Majimbo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini yamewahi kuongozwa na wabunge na madiwani wa Chadema kwa muda mrefu, huku Chama cha Mapinduzi (CCM), kikiwa chama cha upinzani mara kadhaa katika wilaya hiyo.

Baadhi ya wanasiasa wa Chadema waliowahi kuwa wabunge wilayani Tarime ni Chacha Wangwe, Charles Mwera, Esther Matiko na John Heche.

“Bila shaka nyie sio watu wa kuhutubiwa sana kuhusu mageuzi. Mmeshaipokea Chadema na kuisimika hapa tangu miaka ya 2000, nakumbuka kishindo cha mwaka 2005 nilipokuja Tarime kama mwandishi wa habari wakati wa uchaguzi mkuu enzi hizo za Marehemu Chacha Zakayo Wangwe, tangu wakati huo hamjaruhusu Chadema ishuke, simameni hapohapo, ngome zetu zirudi,” alisema Mwalimu na kuongeza:

“Msikubali kuyumbishwa, Chadema ndio chama chenu. Mmekuwa wa mfano huko kwengine, hadi kufikia kuibuka kwa kauli mbiu ya “mambo kama Tarime.”

Aliwataka wakazi wa Tarime Vijijini kuirejesha Sauti ya John Heche ndani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani ndiyo tasiwra ya watu wa Tarime na siasa zao ndani ya Bunge hilo na Taifa kwa ujumla.

“Nawaomba watu wa Tarime muda ukifika rudisheni sauti ya John Heche katika siasa za Bunge la Tanzania akaisemee Tarime, sasa hivi kumepwaya kuna kitu kinapungua,” alisema Mwalimu.

Aidha, Mwalimu amewakumbusha wakazi wa Tarime kuendelea kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kuhakikisha wanajisajili kwenye kanzidata ya kidigitali (Chadema Digital) kwa kulipia ada na kupata kadi mpya za kisasa.

Amewahimiza wasiipuuze Chadema Digital kwani ndio inayotumika kuandaa wanachama,wagombea pamoja na kukiwezesha chama hicho kukusanya michango ya wanachama kupitia malipo ya ada zao

Ziara ya Oparesheni +255, ya Chadema, yenye ujumbe wa “Katiba Mpya: Okoa Bandari Zetu”, inayoongozwa na Mbowe, akiambatana na Salum Mwalimu na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Gimbi Masaba, Grace Kihwelu na Patrick Ole Sosopi, nahitimishwa leo Septemba 6, kwenye kanda ya kichama ya Serengeti, inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.

Ziara hiyo imefikia majimbo yote 24 ya mikoa hiyo na kufanya mikutano ya hadhara takribani mia moja ndani ya muda wa siku 13, ikiwa ni wastani wa mikutano kati ya sita hadi tisa kwa siku.

Idadi ya mikutano imefikiwa kutokana na Mbowe kutumia usafiri wa Chopa, akiendeleza rekodi ya kuwa mwanasiasa pekee nchini anaeendelea kufanya siasa zake kwa usafiri huo uliombatiza jina la Kamanda wa Anga.

Mwaka 2005 Mbowe akiwa mgombea wa Urais wa Chadema, alibuni matumizi ya Helikopta katika Kampeni zake na kuweka rekodi ya kuwa mwanasiasa wa kwanza kutumia usafiri huo katika kampeni za uchaguzi, na tangu wakati huo ameendelea kutumia chopa katika oparesheni zake za uimarishaji wa chama hicho.

Like