Baada ya Lissu, sasa Magufuli “amtaka” Heche

  • KIKUNDI cha maofisa wa vyombo vya dola kinachomzunguka Rais John Magufuli kimemshauri vibaya, naye ameridhia, na sasa kipo katika harakati za “kumwangamiza” Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, ili aache “kumsumbua rais.”

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika kutoka serikalini, rais na wapambe wake wanasema, “Heche ameanza kuota mapembe kama Tundu Lissu,” na sasa kikosi hicho kimeamriwa kumnyamazisha.

SAUTI KUBWA linaandika kwa uhakika kuwa mipango hii michafu dhidi ya Heche ilianza kuratibiwa mara baada ya ziara ya Rais Magufuli katika mkoa Mara takribani wiki mbili zilizopita.

Vyanzo vyetu vinasema kauli ya kujiamini iliyotolewa na Heche mbele ya rais, akikataa kuburuzwa, ilimkera mkuu wa nchi na wasaidizi wake hao.

Inapochanganywa na ujasiri wake, kukubalika jimboni mwake, na hoja nzito za ufisadi wa serikali anazoibua bungeni mara kwa mara, Heche anatajwa kama mtu ambaye amefikisha ukingoni uvumilivu wa Rais Magufuli.

SAUTI KUBWA inatambua kuwa wanaoratibu mikakati, vikao na maelekezo mahsusi wanatenda kwa agizo toka juu. Vikao vimefanyika Dar es Salaam na Mwanza katika wiki mbili hizi.

Kikosi maalumu kimeundwa kuchunguza nyendo za Heche kuanzia nyumbani hadi kazini. Shabaha yao ni kumshambulia akiwa nje ya Bunge, hasa akiwa Mwanza, Dar es Salaam au Mara.

Hata juzi katika mikutano ya hadhara aliyofanya katika jimbo lake, serikali ilituma baadhi ya mashushushu kupeleleza taarifa ina nyendo zake, kuchunguza kauli zake, na mazingira yake kiusalama.

Katika hali isiyotarajiwa, Heche naye alieleza wananchi wa Tarime, katika mikutano yake ya hadhara juzi, kwamba ana fununu za watu wanaotaka kuondoa uhai wake kwa ajili ya kumfurahisha Rais Magufuli.

Alijiapiza kwamba yeye hatakubali kufa kibudu, na kwamba iwapo watathubutu, basi wajue kuwa ndio utakuwa mwisho wa uvumilivu wa Watanzania; na kwamba ndio utakuwa mwisho wa watawala hawa wanaoshabikia umwagaji damu.

Vyanzo kadhaa vilivyozungumza na SAUTI KUBWA kutoka “jikoni,” vinasema, “wakubwa wamekuwa wanahoji, ‘huyu Heche anajiamini nini?'”

Mvujishaji mmoja wa taarifa ameiambia SAUTI KUBWA kuwa, “hata kwa Tundu Lissu, ilianza hivi hivi. Jioni moja wakati mkuu na timu yake wanatazama taarifa ya habari ya saa mbili, kituo kimoja kilimweka Lissu akiwa anahoji masuala mazito dhidi ya serikali; mkuu akakasirika, na kusema: ‘hivi huyu mtu atatusumbua hadi lini? Nimechoka sasa!’ Akanyanyuka ghafla na kwenda chumbani.

“Hapo hapo wapambe wake wakaanza kupanga jinsi ya kumsaidia kuondokana na Lissu. Aliporejea wakampa wazo, naye akaridhia. Ndivyo mpango dhidi ya Lissu ulivyoanza,” anasema mtoa taarifa wetu. Baada ya ujangili wao dhidi ya Lissu, kulifanyika mabadiliko kadhaa ndani na nje ya kitengo yaliyogusa hata baadhi ya wakuu wa vyombo vikuu vya usalama.

Kikosi maalumu kinachopangwa kushughulika na Heche kinaundwa na watu mchanganyiko, wakiwemo baadhi ya vijana “walioingizwa kitengoni na rais mwenyewe,” bila kufuata taratibu za kisera. Baadhi yao ni maofisa wa polisi. Wengine ni wageni, na wengine hawafahamiki hata taaluma zao.

Kwa sababu hiyo, mmoja wa wavujisha taarifa anasema: “Unajua mambo haya yametufanya hata sisi wenyewe tugawanyike, hatuaminiani, na hatukubaliani. Kwa sababu hiyo operesheni hizi zinafanywa lakini haziungwi mkono na baadhi ya maafande wetu, nadhani hata mkuu hatuamini sawa sawa. Ndiyo maana naye anaajiri wa kwake kwa njia zake.”

Baadhi ya watu walio karibu na Heche wameiambia SAUTI KUBWA kuwa katika mikutano yao ya hadhara iliyomalizika Jumapili hii, walitilia shaka baadhi ya watu waliokuwa wanafuatilia nyendo za Heche, na kwamba hata yeye alipokuwa anazungumza aliona baadhi ya sura alizozitilia shaka.

Wanasema watasimama na mbunge wao na kumlinda kwa nguvu zote hata zile ambazo dola haidhani kuwa wanazo.

Katika siku za hivi karibuni, Heche amekuwa katika malumbano ya hoja na serikali kiasi kwamba katika mmoja wa mikutano ya rais wilayani Tarime, mbunge huyo alinyang’anywa kipaza sauti na wana usalama kwa amri ya rais, pale alipomtaka rais asikilize maelezo viongozi badala ya kuwaamuru wajibu maswali kwa mkato, na asigeuze mkutano wake kuwa wa CCM.

Aidha, Heche kwa nyakati mbalimbali bungeni ameibua kashfa nzito dhidi ya serikali, hasa rais na wasaidizi wake wa karibu, katika miradi ya e- passport na vitambulisho vya taifa.

Shinikizo la kumshughulikia Heche, pamoja na kutoka kwa rais, linashadidiwa pia na baadhi ya maofisa wakubwa serikalini wenye “madudu” ambayo Heche amekuwa anaibua.

Taarifa za uhakika zilizoifikia SAUTI KUBWA zinasema mipango hii michafu imeshavuja hata nje ya mipaka ya nchi. “Katika mazingira tuliyomo, si wewe tu unayejua mambo haya. Jamii ya kimataifa nayo inamulika mienendo yetu, na mambo mengi tunayofanya hata sirini, maana, kama ujuavyo, nao wana watu wao humu,” kimesema chanzo chetu.

Like
23

Leave a Comment

Your email address will not be published.