Wizi wa kura wa CCM, NEC 2020 waanza kuibuliwa

NJAMA za “utatu wa kishetani” kuiba kura na kuvuruga uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2020, zimeendelea kudhihirisha namna zilivyominya haki za Watanzania kuchagua madiwani, wabunge na rais wanayemtaka.

Ushirika wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), maarufu – utatu wa kishetani umeendelea kuumbuka kwamba ulipanga matokeo ya kura katika uchaguzi huo uliogubikwa na kila aina ya mbinu chafu na wazi za kukataa matakwa ya Watanzania.

Katika utafiti uliofanyika hivi karibuni, imebainika kuwepo kwa ukweli kwamba ushirika huo ulipanga wagombea wote wa CCM wapate ushindi walioutaka na kwamba kila mkoa ulipangiwa idadi na asilimia ya ushindi.

Sampuli za utafiti huo zinaonyesha kuwa ushirika huo ulipanga washindi wa ubunge Mkoa wa Mbeya, katika wilaya za Mbarali na Mbeya Mjini, ushindi kwa CCM uwe ni kati ya asilimia 66 na 70. Matokeo yaliyotangazwa yalionyesha kwamba CCM ilishinda kwa kura 55,737 (asilimia 66.47) huku mgombea wa Chadema akipata kura 28,104 (asilimia 33.52). Jimbo la Mbeya Mjini CCM ilipata kura 75,225 (66.67%), huku mgombea wa Chadema akipewa kura 37,591 (33.32%).

Mkoa wa Njombe ulipangiwa kupata kati ya asilimia 80 na 85 na matokeo yaliyotangazwa yaliashiria kuwepo kwa mpango wa awali uliosukwa kwa ushirika wa NEC, TISS na CCM. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Makambako alipata kura 24,766 (asilimia 82.89) huku mpinzani wake kutoka Chadema akiambulia kura 5,106 (17.11%).  Jimbo la Makete mgombea wa CCM alipata kura 24,237 (82.68%) na Chadema ikipewa kura 5,077 (17.31%).

Katika Mkoa wa Songwe ushirika huo ulipanga washindi wa CCM wasizidi asilimia 70 ya ushindi na matokeo yaliyotangazwa yalikuwa hivi; Jimbo la Vwawa, mgombea wa CCM alipata kura 38,226 (69.02%) na mgombea wa Chadema akipewa kura 17,157 (30.67%) wakati Jimbo la Mbozi, mgombea wa CCM akipata kura 40,834 (69.34%), mgombea wa Chadema alipewa kura 18,054 (30.65%).

Uchaguzi huo uliofanyika katika mazingira magumu kwa wapinzani, hasa chama kikuu cha upinzani, Chadema, ulishuhudia vyama vya upinzani vikiambulia kiti kimoja tu bungeni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ikipata viti vinne pekee. NEC ilimtagaza mgombea urais wa CCM, John Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha urais.

Like