Wawakilishi ACT-Wazalendo wala kiapo Zanzibar

WAJUMBE watano kutoka chama cha ACT-Wazalendo wameapa jana katika mkutano wa pili wa Baraza la Wakilishi la 10 unaoendelea Chukwani Mjini, Zanzibar.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, aliwaapisha baada ya chama cha ACT-Wazalendo kukubali kushiriki Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK) inayoongozwa na Rais Dk Hussein Mwinyi (CCM).

Wajumbe hao ni pamoja na Habib Ali Mohammed kutoka Jimbo Mtambwe, Hassan Omar Hamad kutoka jimbo la Kojani na Kombo Mwinyi Shehe kutoka Jimbo la Wingwi walichaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita mkoa wa Kaskazini Pemba.

Wengine ni Nassor Ahmed Mazrui na Omar Said Shaaban. Waliteliwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mwenezi na Mahusiano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani, alisema haikuwa kazi rahisi kwa chama hicho kufikia makubaliano ya kushirikiana na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa.

“Hii ni hatua kubwa kwa watu wetu kuingia ndani ya Baraza la Wawakilishi katika kipindi hiki kigumu cha makovu ya Uchaguzi Mkuu ambao uligubikwa na kila aina ya hujuma na unyama mkubwa. Lakini tumefanya yote haya kwa maslahi ya Zanzibar,” alisema Bimani.

Wawakilishi hao waliapa jana ikiwa ni siku 100 za Rais Mwinyi kuingia madarakani tangu Septemba mwaka jana.

Nassor Mazrui akila kiapo cha kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi

Like