Serikali yahaha kuzuia mashirika, taasisi kusema “kuna Corona” Tanzania

VIONGOZI wa taasisi, mashirika ya umma na idara za serikali wamekatazwa kutangaza chochote kuhusu tahadhari juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa Corona – “kwa hofu ya kuleta taharuki.”

Yeyote miongoni mwao atakayetangaza kuwepo kwa ugonjwa huo na kutahadharisha, atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kufunguliwa jinai.

Habari zilizofikia SAUTI KUBWA zinaeleza kuwa serikali kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, zinaeleza kuwa makatibu wakuu wa wizara zote wamepewa maelekezo hayo leo na kutakiwa kuyasambaza kwa wafanyakazi wote wa serikali.

Taarifa zinaeleza kuwa serikali inawataka viongozi wote kufuata msimamo wa serikali katika “kutoa tahadhari kwa umma, bila kuleta taharuki.”

Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli imekuwa ikisambaza taarifa za kuhimiza wananchi kujikinga na magonjwa, bila kueleza kuwepo kwa ugonjwa wa Corona na kuwa huo ndiyo msimamo wa Tanzania.

Pamoja na kuwa taarifa hiyo haielezi kuwagusa taasisi binafsi, dini na mashirika binafsi, lakini inatambulika kuwa huo ndiyo mtazamo wa serikali; kwamba “Tanzania hakuna Corona.”

Tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa taarifa kwa umma ikionya hatua ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda kutoa tahadhari kwa wanachuo na umma kujikinga na janga la Corona.

Katika waraka wake, Prof. Bisanda uliosambazwa juzi- Februari 8, 2020, aliwataka wanafunzi wa chuo hicho, walimu na watendaji wengine kuchukua tahadhari kujikinga na Corona – “kwani ipo.” Alihimiza kusoma kwa kutumia mitandao, kuacha kukutana na kuhakikisha kila mmoja anafuata njia sahihi za kujinga na janga hilo.

Leo, serikali kupitia wizara ya elimu, imeukana waraka huo wa Prof. Bisanda na kuuita ni maoni binafsi, huku ikionya viongozi kutumia nembo ya taifa katika “maoni binafsi.”

Serikali ilisema maelekezo yaliyotolewa na Prof. Bisanda hayakuzingatia mwongozo wa udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika shule, vyuo na taasisi za elimu nchini wa wizara ya afya wa Mei 27.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, leo jioni, Baraza la OUT liliitisha kikao cha dharura na kuazimia kuwa Prof. Bisanda alikosea katika waraka wake na kwamba anatakiwa kuomba radhi serikali na umma. Pia baraza hilo katika taarifa yake limeomba radhi kwa ngazi hizohizo kwa kile ilichoeleza kuwa ni “usumbufu uliojitokeza.” Pia limewataka wanafunzi na wafanyakazi kuendelea na kazi zao kama kawaida.

Mbali na waraka huo wa OUT, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Tanzania (SUA) kilitoa taarifa yake jana – Februari 9, kikiwahimiza wanafunzi, walimu na jumuia nzima kuchukua tahadhari na kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Taasisi za dini, likiwamo Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) zimetoa tahadhari kwa waumini wao na umma juu ya ugonjwa huo, wakitaka kila mmoja kujilinda na Corona.

Gazeti la Jamhuri, katika toleo lake la wiki hii, limeandika habari kuubyenye kichwa cha habari, “Tiba ya kupumua hatari.” Mmoja wa wahariri wa gazeti hilo ameliambia SAUTI KUBWA: “Ni dhahiri kuwa tulidhamiria kuandika, ‘Tiba ya Corona hatari,’ lakini tulisita kwa sababu ya hofu iliyojengwa na serikali. Tunaamini wasomaji wameelewa tulichomaanisha.”

Sambamba na taasisi hizo, leo Februari 10, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari ya ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Katika taarifa yake iliyotumwa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ubalozi huo, umeeleza kuwepo kwa ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona tangu Januari, 2020.

“Hatua za kuzuia maambukizi ya COVID-19 bado zimeeendelea kuwa za kiwango cha chini, Tanzania haijatoa takwimu zozote kuhusu maambukizi au vifo vilivyotokana na ugonjwa huo tangu Aprili 2020’’ inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ubalozi huo kuwa upo uwezekano mkubwa kwa hospitali na vituo vya afya nchini Tanzania kuzidiwa kwa haraka na idadi ya wagonjwa wenye matatizo yanayohusiana na Corona.

‘’Uwezo mdogo wa hospitali nchini kote Tanzania unaweza kusababisha wagonjwa wa dharura kuchelewa kupata huduma, jambo linaloweza kuhatarisha maisha,’’ inaongeza taarifa hiyo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi mbili, nyingine ikiwa ni Korea Kaskazini kukataa kutoa taarifa endelevu za kuwepo kwa Corona, idadi ya wanaoambukizwa, kupona na hata kufariki dunia. Mara ya mwisho kutoa taarifa zke ilikuwa Aprili 29, 2020.

Like