“Usalama” wafanikiwa kuhadaa umma na kukuza uvumi wa afya ya Magufuli

KWA sehemu kubwa, Idara ya Usalama Taifa (TISS) imefanikiwa kuhadaa Watanzania na dunia kuhusu hali ya kiafya ya Rais John Magufuli huku ikivuta muda apone na aonekane hadharani.

Taarifa ambazo SAUTI KUBWA imezipata kwenye vyanzo vya kiusalama zinasema idara imefurahia uvumi ulioenea kuwa Rais Magufuli amepelekwa Nairobi Kenya na baadaye kuhamishiwa India kwa ajili ya matibabu.

“Rais hajapelekwa popote nje ya nchi. Mazingira ya sasa ya uhusiano wa Kenya na Tanzania si mazuri kiasi cha kumpeleka huko. Yupo anatibiwa hapa hapa Dar es Salaam. Uvumi wa Nairobi na India umetengenezwa, na umewanasa washindani na wakosoaji kupitia mitandao ya kijamii, ukadakwa na vyombo vya habari vya kimataifa. Katika hili, TISS imefanikiwa,” kimesema chanzo cha habari hicho ambacho hatuwezi kukitaja kwa sababu za kiusalama.

Hata hivyo, SAUTI KUBWA ina taarifa zisizokuwa na shaka kwamba Rais Magufuli ni mgonjwa tangu tarehe 3 Machi 2021. Amekuwa chini ya uangalizi wa madaktari wake Ikulu, Dar es Salaam, na baadaye akahamishiwa hospitali maalum kwa viongozi iliyomo ndani ya eneo la TISS Kijitonyama – maarufu, Hospitali ya Mzena. Alilazwa hapo tangu tarehe 6 Machi 2021.

Kwa muda wote ambao Magufuli amelazwa, shughuli za rais zimekuwa chini ya Makamu wa Rais Samia Suluhu ambaye, afya ya rais ilipokuwa mbaya, aliombwa arejee Dar es Salaam kwa haraka kutoka Zanzibar akiwa na ulinzi wa ziada.

Jumanne wiki hii, Samia aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza tangu serikali ya awamu ya tano indie madarakani. Katika kikao hicho, suala la afya Rais Magufuli halikugusiwa wala halikuuliziwa, bali mawaziri walijadili mpango wa serikali wa mwaka 2021/2022 ambao umepelekwa bungeni.

Hata hivyo, kutokuwepo kwa rais katika mazingira yenye uvumi juu ya afya yake kulizusha minong’ono miongoni mwa mawaziri.

Mawaziri wamefichwa taarifa za afya ya rais. Masuala yote yanayohusu matibabu ya rais na mawasiliano kuhusu ugonjwa wake na matibabu hayo vipo mikononi mwa TISS.

Taarifa zilizopo ni kuwa Rais Magufuli aliambukizwa Corona, ambayo ilileta madhara pia katika moyo wake. Rais Magufuli ana tatizo la moyo kwa muda mrefu, na amekuwa anatibiwa hapa hapa nchini na madaktari wa ndani na wa nje, hasa Ujerumani. Zamu hii, vyanzo vinasema serikali imeagiza madaktari kutoka India washirikiane na wenyeji kumpatia matibabu makubwa ili kunusuru maisha yake.

Wasaidizi kadhaa wa rais wameugua Corona; baadhi yao wamepoteza maisha, na rais mwenyewe amekuwa anapuuza ushauri wa kitaalamu wa kuepuka au kupunguza maambukizi ya Corona.

Kuna taarifa mkanganyiko kuhusu maendeleo ya afya ya rais. Baadhi ya vyanzo vinasema ameanza kupata nafuu, na akiimarika ataandaliwa tukio aonekane hadharani ili kusitisha uvumi unaoendelea.

Vyanzo vingine vinasema bado yupo hoi, na kuna uwezekano ikamchukua muda mrefu kurejea hali ya kawaida. Wapo ambao tayari wanazungumzia uwezekano wa makamu wa rais kuongoza nchi kwa kipindi chote kilichobaki iwapo itathibitika kuwa rais hana uwezo tena wa kumudu majukumu yake. Itabidi makamu wa rais aapishwe kuwa rais na utaratibu wa kikatiba utumike kupata makamu wa rais mpya.

Katika hali ya kusafisha upepo, tayari TISS imeanza mkakati wa kuingilia baadhi ya vyumba vya habari na kutumia “kasoro ya Nairobi na India” kushambulia watumiaji wa mitandao na vyombo vya habari vya kimataifa vilivyolivalia njuga suala hili. Hilo litafanyika wakati wowote kuanzia sasa iwapo serikali itajiridhisha na kuimarika kwa afya ya rais.

Vyanzo rasmi vya serikali vimegoma kuzungumzia suala hili. Hadi habari hii inachapishwa, Dk. Hassan Abbas (aliyepewa jukumu la kuwa msemaji mkuu wa serikali kinyume cha sheria) na mwandishi wa habari wa rais, Gerson Msigwa, wamegoma kujibu maswali ya SAUTI KUBWA yaliyowasilishwa kwao kwa zaidi ya siku nne sasa.

Juzi, Dk. Abbas alipoulizwa na vyombo vya habari vya kimataifa, alipokea maswali kupitia simu – kwa WhatsApp na hakujibu kwa maandishi zaidi ya kuweka kibonzo cha kuonyesha mshangao (emoji).

Ni kawaida kwa idara ya usalama kuficha taarifa za ugonjwa wa rais na kutumia mwanya wowote unaopatikana kuonyesha kuwa “rais yu imara.” Mara chache ambapo tarifa za ugonjwa wa rais hutoka hadharani ni kwa idhini yake mwenyewe kwa shabaha maalumu.

Wachambuzi wa kisiasa wanaeleza kuwa iwapo serikali ingekuwa imetoa taarifa hadharani, uvumi wote unaoendelea usingekuwepo kwa sababu rais ni binadamu naye “ana haki ya kuumwa.”

“Pamoja na kazi nzuri waliyofanya TISS kudhibiti uvumi huu wao ndio waliousababisha kwa kujaribu kuficha ugonjwa wa rais,” kimesema chanzo chetu kutoka ndani ya chama tawala, CCM.

Like
18