Picha hii inazungumza maneno 5,000

INASEMEKANA kuwa picha moja ni sawa na maneno 1,000. Hii hapa inazungumza maneno yapatayo 5,000.

Kushoto ni John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania tangu 2015.

Tangu Juni 2020 hadi Februari 2021, Magufuli amekuwa anasema kuwa Corona haipo Tanzania, kwa maelezo kuwa Mungu aliiondoa baada ya siku tatu za sala kitaifa.

Wenzake katika picha hii wote wamefariki dunia baada ya kuambukizwa Corona kwa nyakati tofauti.

Anayefuata ni Balozi John William Kijazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa rais. Alifariki dunia Februari 17, 2021.

Anayefuata ni Oswald Simon Majuva, aliyekuwa mmoja wa wasaidizi wa rais, Ikulu, ambaye baadaye alihamishiwa Mkoani Mara kuwa msaidizi wa Ofisa Tawala wa mkoa. Amefariki leo Machi 12, 2021 baada ya kuambukizwa Corona.

Wa nne ni Balozi Augustine Phillip Mahiga, akiapishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Alifariki dunia Mei 1, 2020 kwa ugonjwa huo huo.

Wakati wa kuchapisha andiko hili, Magufuli amekuwa kitandani kwa siku 10 mfululizo baada ya kuambukizwa Corona. Jitihada za kuokoa maisha yake zimekuwa zinaendelea, na tunasubiri taarifa rasmi ya serikali juu ya maendeleo ya matibabu yake.

Serikali imekuwa inahaha kuficha taarifa hizo, na hivyo kukazuka uvumi mitandaoni kuhusu hali ya afya ya rais, hadi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo akajitokeza kudai kuwa “rais yu mzima salama salimini.”

Bado Watanzania wanataka kumwona yeye mwenyewe, vyovyote alivyo. Wanasubiri!

Like