Tanzania yazidi kujichafua duniani kwa hila, ubabe wa madaraka

TANZANIA imeingia katika orodha ya nchi zinazotumia ubabe na hila kubaki madarakani ikiwa ni pamoja na kuminya uhuru wa kupashana habari kwa kuzima mtandao wa mawasiliano wa intaneti.

Ripoti ya taasisi ya Accessnow ya New York, Marekani iliyotangazwa jana, imesema Tanzania imeungana na nchi zingine 11 za Afrika ambazo zilizima intaneti mwaka jana, bila kujali kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaoendesha maisha yao kwa kutegemea mawasiliano hayo.

Tanzania inatajwa na ripoti hiyo kwamba ilizima intaneti kwa sababu ya “kusaidia watawala kubaki madarakani,” ingawa serikali ilieleza vinginevyo- kwamba ni kuepusha vurugu wakati wa uchaguzi mkuu. Tanzania ilifanya uchaguzi wake Oktoba, mwaka jana- 2020.

Mawasiliano yaliyozimwa kabisa wakati wa uchaguzi na hadi sasa bado uimara wake unasuasua ni mitandao ya kijamii, hasa Twitter. Ni katika kipindi hicho na hata wakati huu, watu wengi wanalazimika kutumia njia ya VPN ili kuwasiliana kwa urahisi.

Taasisi hiyo ya Accessnow inaeleza kuwa India inaongoza duniani kwa kuzima intaneti, ikiwa imefanya hivyo mara 109 kwa mwaka jana pekee. Katika Afrika – Ethiopia inaongoza kwa kuzima mara 4. Nchi zingine za Afrika ni Guinea, Togo, Sudan – zilizozima mara 2, huku Algeria, Mali, Misri, Burundi, Chad, Uganda na Kenya – zilizima mawasilian hayo mara moja kama ilivyo kwa Tanzania.

Ripoti hiyo inayojumuisha taasisi 243 kutoka nchi 105, hutolewa kila mwaka kutathmini athari za kuzima kwa mawasiliano hiyo, huku ikisisitiza serikali kuacha kuminya uhuru wa kuwasiliana, kuzuia biashara zinazotegemea mitandao na zaidi sana kuonya na kukemea kukwamisha ustawi wa maisha yanayotegemea uwepo wa huduma hiyo.

Accessnow inaonyesha kuwa mwaka 2018, huduma ya intaneti ilizimwa mara 196, wakati mwaka 2019, intaneti ilizimwa mara 213.

Like
1