Shabaha ya Magufuli kufunga mitandao ni kulea ufisadi

HOFU ya kiza cha ujinga inazingira serikali ya Tanzania, na sasa watawala wanapanga kufunga – Facebook, WhatsApp, Twitter na hata Instagram.

Kupitia mitandao hiyo, si wanafunzi tu wanaopata uelewa wa masuala mengi, bali jamii pana imekuwa inaelimika na kuondokana na ujinga wa wa masuala madogomadogo kuhusu sayansi, afya, elimu yenyewe na mazingira.

Wanaotumia vyema mitandao hiyo wamekuwa wakipata elimu kuhusu masuala wanayotaka kufahamu. Wamejua nini kinatokea wapi na lini, pamoja na kuwasiliana kwa njia rahisi na watu wanaowataka.

Kimsingi, faida kubwa ya mitandao hiyo ni kuondoa ujinga. Mtu hahitaji kwenda darasani na kulipa fedha nyingi kujua somo au kitu fulani. Akiingia kwenye mitandao hiyo anaweza kujifunza na kujua mengi kwa muda mfupi na gharama nafuu.

Hata hivyo, elimu hii sasa inatishwa. Eti inakwaza watawala, na wanaona haina maana kwa kuwa inatoa uhuru mpana kwa wananchi kuwakosoa. Sasa wanaona heri ifungwe, watawale bila “kelele.”

Watawala hawa wanaona heri kuendelea kuwa na idadi kubwa ya watu wajinga, ili wasipate watu wengi wa kuwasumbua. Wanaficha nini?

Tayari kuna watu wanakamatwa, wanashitakiwa na kuhukumiwa kwa kuwa tu wametoa maoni yasiyopendwa na “wakubwa.” Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inaongoza kwa idadi ya watu wanaokamatwa na “kutiwa kashkash.”

Ili kuendelea kudhibiti watumiaji wa mitandao hiyo ya kijamii, Tanzania imetunga sheria kali “kuwazuia” watumiaji hao. Kimsingi, sheria hizi ni kikwazo kwa jitihada za kusambaa uhuru wa maoni na kuendelea kuwepo kwa shule-pendwa.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Desemba 2017 inaonesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti (njia ya kupata mitandao ya kijamii) imeongezeka kufikia watu milioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 45 ya Watanzania wote. Tanzania ina zaidi ya watu milioni 50 kwa sasa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema udhibiti huo wa mitandao una shabaha ya kunyamazisha wananchi ambao wamekuwa na ari ya kujisomea, kuwa na mwamko wa kuhoji, na kukosoa mwenendo wa viongozi na serikali.

Rais John Pombe Magufuli amwkuwa akitoa matamko na kauli mbalimbali dhidi ya “uhuru wa watumiaji wa mitandao uliovuka mipaka.”

Aprili 21, mwaka huu, Rais Magufuli alionekana na alisikika kwenye runinga, wakati akiapisha majaji 10 wa mahakama kuu, akisema uhuru wa watumiaji wa mitandao ya kijamii umevuka mipaka na watu wanatumia uhuru huo kupotosha baadhi ya mambo yanayofanywa na serikali yake.

Alisema: “Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sasa sifahamu huu ugonjwa umetoka wapi? Lakini ni kwa sababu hii mitandao hatui-control (hatuidhibiti) sisi, wako huko wenye mitandao yao, wao interest (maslahi) yao ni kutengeneza biashara, hawajali madhara mtakayoyapata.”

Licha ya watawala kukerwa na mitandao ya kijamii na uhuru wa wananchi kuhoji, kuchangia mawazo yao katika uendeshaji wa nchi, Katiba ya Tanzania inaruhusu uhuru huo, ingawa sasa kumeanza kutungwa sheria zinazokinzana na matakwa hayo ya kikatiba.

Tanzania imepitisha Sheria ya Maudhui ya Mtandaoni ya Mwaka 2015 ambayo imewatia hatiani baadhi ya watu kwa makosa mbalimbali ikiwemo ‘uchochezi’.

Ili kuipa nguvu sheria hiyo, mapema mwaka huu serikali ilipitisha kanuni mpya za maudhui ya mitandaoni za mwaka 2018. Kifungu cha 4 kinataka wamiliki wa blogu, tovuti, majukwaa, radio na runinga za mtandaoni kujisajili ili wapate leseni za kuendesha shughuli zao.

Waliopewa mamlaka ya kusimamia maudhui ya mtandaoni ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Hawa watakuwa na uwezo wa kulazimisha wamiliki wa blogu au tovuti kuondoa maudhui yanayodhaniwa kuwa hayafai ndani ya saa 12, na kama hawajatimiza maagizo hayo, wanaweza kulipa faini isiyopungua Sh. 5,000,000 au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela.

Ikumbukwe kuwa Septemba 28, 2016 Rais Magufuli alinukuliwa akisema: “natamani siku moja malaika washuke wazime hii mitandao yote, ili baadaye itakapofunguliwa wakute sisi tumeisha tengeneza Tanzania yetu mpya.”

Kimsingi, kulipiza wananchi usajili wa blogu ni wizi wa wazi unaofanywa na serikali ya Tanzania kwa kuwa haimiliki intaneti. Lakini kwa kuwa teknolojia imekua kuliko uwezo wa serikali kuidhibiti, watamzunguka. Atafunga pale, watafungua kwingine.

Kwa maana yeyote, kauli ya rais kufunga mitandao inaeleza dhamira yake halisi ya kunyamazisha wananchi. Anaogopa maarifa na taarifa wanazochota mitandaoni,

Anachotaka ni kimoja – wasimseme. Kwa vyovote vile, kuna jambo ovu anataka kufanya au ameshafanya, na hataki wananchi walijue. Kama si ufisadi, mtu huyu anaficha nini?

Like
5
3 Comments
  1. James 6 years ago
    Reply

    Ataweza kuifungia hiyo mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook n.k. lakini hiyo ndio itazidi kuongeza chuki kwa serikali yake.
    Kitu kingine atakuwa anazidi kujitangaza kwamba yeye ni dikteta kwa raia wa nje wanayoitembelea Tanzania. Hebu fikiria raia wa nje anaingia Tanzania halafu anagundua hawezi kutumia WhatsApp au Facebook. Kitu kitakachofuata ataingia udadisi wa kutafuta kwanini hawezi kutumia huduma hizo. Mwisho atagundua anaishi nchi ya kidikteta.

    2

    0
  2. Edmund Costantine 6 years ago
    Reply

    Hakika umenifumbua macho
    kwa haya uliyoelezea

    0

    0
  3. KATALA 6 years ago
    Reply

    Wengi tumefunguka macho na kupata picha kamili hongera ?????

    1

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.