Fedha zilizopotea ni zaidi ya Trilioni 1.5, ni 2.6. Zipo wapi?

 

NILISIKILIZA kauli ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, wakati alipokuwa akieleza Bungeni “zilipo Shs. trilioni 1.5,” nikajiuliza, kwanini serikali hii inataka kutuchanganya kwa hesabu za kutengeneza kama vile huku nje ya serikali hakuna wahasibu wanaojua mambo haya au hakuna watu wanaojua hesabu?

Serikali kupitia kwa naibu waziri wa fedha inasema tofauti hiyo ya 1.5 trilioni imetokana na serikali kutumia mfumo wa IPSAS Accrual wa kutambua mapato na matumizi pale miamala inapokamilika na siyo pale mapato taslimu yanapopokelewa au matumizi yanapolipwa.

Naibu waziri, katika kauli yake Bungeni, anasema baada ya miaka mitano ya majaribio, serikali ilianza kutumia mfumo huo wa IPSAS Accrual kuanzia 2016/17.

Maswali ya kumwuliza naibu waziri na serikali yake hii ya CCM ya awamu ya tano ni haya yafuatayo:

Kwanza, kama mwaka 2016/17 Serikali ilianza kutumia IPSAS Accrual, hesabu zilizopelekwa kwa CAG kwa ukaguzi zingeonyesha  hesabu zilizokokotoa naibu waziri Bungeni zinazoonyesha mapato ya trilioni 24.41 (pamoja na overdraft ya bil. 79) na matumizi ya trilioni 24.49.

Sasa kwanini CAG hakupewa hesabu hizo zenye kutumia IPSAS Accrual hadi CAG akakuta hiyo tofauti ya trilioni 1.5?

Pili, kma yanayosemwa na serikali kupitia saibu waziri yangekuwa kweli, utata huu wa 1.5 trilioni ungemalizwa kwenye exit meeting kati ya CAG na Hazina kabla taarifa ya mwisho ya CAG haijatolewa.

Kwanini Hazina hawakufanya hivyo hadi Mhe. Zitto Kabwe alipoibua sakata hilo?

 

Tatu, kama maelezo ya naibu waziri ndiyo sahihi, je, ina maana CAG ndiye hazingatii mfumo wa IPSAS Accrual kwenye ukaguzi wake hadi atoe hesabu ambazo hazizingatii mfumo huo?

Jambo hili haliwezi kuwa kweli kwa sababu ni huyo huyo CAG ambaye kwa miaka kadhaa amekuwa akiitaka serikali kukamilisha na kuanza kutumia mfumo wa IPSAS Accrual. Maana yangu ni kwamba kama serikali inatuambia kuanzia mwaka 2016/17 walianza kutumia mfumo wa IPSAS Accrual na CAG pia angetumia mfumo huo katika kukokotoa mahesabu kwenye ukaguzi wake na kusingejitokeza tofauti hiyo ya trilioni 1.5.

Nne, naibu waziri anasema serikali ilianza kutumia mfumo huo mwaka wa fedha wa 2016/17. Maana yake ni kwamba kabla ya hapo mfumo huo haukutumika kwenye kutambua mapato na matumizi.

Sasa je, serikali inaweza kutueleza ile tofauti kama hiyo ya shs. trilioni 1.088 ya mwaka 2015/16 kati ya mapato na matumizi ilitokana na nini?

Kwa taarifa tu ni kwamba mwaka 2015/2016 mapato ya serikali kwa mujibu wa CAG yalikuwa trilioni 21.109 na matumizi yalikuwa trilioni 20.021.

Serikali ije tena itudanganye kwamba katika tofauti hii ya trilioni 1.088 ya mwaka 2015/16, mapato “tarajiwa” yalikuwa kiasi gani. Kumbuka wamesema IPSAS accrual ilianza kutumika 2016/17 na siyo 2015/16).

Hati fungani zilikuwa ngapi (hizi ambazo CAG inaonekana haonyeshwi wakati wa ukaguzi? Makusanyo ya Zanzibar yalikuwa kiasi gani (hizi ambazo CAG haonyeshwi na kuzingatia kwenye ukaguzi)?

Lakini kwa upande wa CAG kuna maswali mengi ambayo na yeye anatakiwa atakapokutana na Kamati ya PAC ayajibu bila woga.

Kwa nini CAG hakutolea maelezo (comment) hiyo tofauti ya 1.5T? CAG alitakiwa aeleze nini maana ya hiyo 1.5T. Je, ameona ni mapato yaliyopokelewa mwaka 2016/17 lakini matumizi yake yamekwenda kufanyika 2017/18 (kama mimi nilivyoamini awali)?

Je, ameshindwa kujua tofauti hiyo iko wapi? Kama ni matokeo ya IPSAS Accrual kama Serikali inavyodai, CAG angeiona hiyo na kuitolea maelezo kwenye ripoti yake. Kwa nini hakufanya hivyo? Je, CAG anahisi kuna ubadhirifu wa hiyo 1.5T?

Anatoa ushauri au maagizo gani kuhusu tofauti hiyo? Mimi najiuliza sana kwa nini CAG hakutuweka wazi kuhusu 1.5T. Au aliona ni kiasi kikubwa mno kinachotisha kiasi kwamba aliogopa kukitolea maelezo na kuamua kuwaachia wabunge na wachambuzi wengine wafanye kazi ya kukokotoa na kuhoji wenyewe?

Au CAG alifanya ukokotoaji na akahoji hiyo tofauti lakini akatishwa na hivyo kuacha hoja ikining’inia bila maelezo? Au kweli ripoti ya mwanzo ya CAG kuna aya imenyofolewa kama watu wengine wanavyohisi?

Hiyo trilioni 1.5 ni tofauti ya mapato yaliyokusanywa na matumizi yaliyolipwa kwa mwaka 2016/17. Lakini kama nilivyoeleza hapo juu, kwenye taarifa ya CAG ya mwaka uliotangulia wa 2015/16 utaona pia kulikuwa na tofauti ya trilioni 1.1 (mapato 21.1T na matumizi 20.0T).

Kwa maana hiyo kwa miaka miwili toka Julai 2015 hadi Juni 2017, wananchi wa Tanzania hatujui zilipo shs. 2.6 trilioni. Tunadai kujua wapi zilipo.

Kama CAG anaogopa au ametishwa ili asiulize zilipo hizi fedha, sisi tutaendelea kuihoji Serikali: ZIKO WAPI TRILIONI 2.6?

Tunawasubiri wabunge na wajumbe wa PAC muda wa mjadala utakapofika mtusaidie watanzania. Hazina na CAG waje na majibu yenye ukweli.

Huu ni uchambuzi wa Dk. Milton Mahanga, mtaalamu kwenye masuala ya fedha, ununuzi na uendeshaji wa nyumba mijini. Amekuwa mhadhiri kwenye fani za uhasibu, ununuzi na ugavi, mbunge kwa miaka 15, na naibu waziri kwa miaka 10 katika wizara kadhaa za Tanzania. Ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, na  mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema.

Like
14
4 Comments
  1. Prosper Lazaro 6 years ago
    Reply

    Tusiache kuhoji juu ya huu wizi uliokufuru kwenye taifa letu, miaka miwili tuu tushaibiwa 2.6 tr !? Hakika nchi hii akina mama hawakutakiwa kujifungulia vumbini tena Giza.
    Tuamke kifikra waTz

    0

    0
  2. Ngondo mbwitu 6 years ago
    Reply

    Watanzania tumeibiwa sana. Sasa ni muda wa kusema ni basiiii!!

    0

    0
    • MAKIWERU NKYA 6 years ago
      Reply

      Iko shida kubwa

      0

      0
  3. MAKIWERU NKYA 6 years ago
    Reply

    Iko shida kubwa

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.