Japan, Uingereza zaikamia Tanzania kuhusu Corona

WAKATI Japan ikizuia raia wake kusafiri Tanzania kwa sasa, Uingereza imewataka wasafiri wote wanaotoka au kupitia Tanzania na nchi nyingine zilizowekwa katika “kundi la hatari” kufanya malipo ya awali ya Sh. 5,250,000 kama maandalizi ya kuwekwa kwenye karantini ya siku 10 katika hoteli maalumu wakishawasili Uingereza.

Taarifa iliyopatikana jana kwa SAUTI KUBWA inaeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan imeshauri wananchi wake kuahirisha au kuacha kabisa safari za kwenda Tanzania kutokana na kuwa na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Corona, lakini hasa kwa kuwa dunia haina uhakika wa kiwango cha maambukizi kwa kuwa serikali ya Rais John Magufuli haitoi takwimu.

Wizara hiyo imesema kuwa kusafiri kwenda Tanzania kunahatarisha maisha, kwani maambukizi ya Corona ni makubwa na kuna kila dalili kuwa ugonjwa huo umesambaa zaidi katika miji mikubwa.

Japan inaeleza kuwa pamoja na kuwa Rais John Magufuli amekuwa akidai kwamba hakuna Corona, kwamba umetoweshwa kwa maombi ya siku tatu, ukweli ni kwamba maambukizi ya Corona ni makubwa, hivyo ni “heri kujikinga kwa kutosafiri.”

Taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa kuna Watanzania wengi walidhani Rais Magufuli anasema ukweli, wakajiachia wakidhani hakuna Corona, kumbe ndipo walikuwa wanajenga mazingira ya kuieneza.

Inaelezwa na taarifa hiyo kuwa mwamko wa watu kunawa mikono, kuvaa barakoa, kuepuka misongamano bado ni mdogo kutokana na msimamo wa rais ambao ulitangazwa mno na vyombo vya habari vya Tanzania.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya wa Uingereza, Matt Hancock, alisema jana jijini London kwamba ni hatari kupokea wageni na hata wenyeji kutoka Tanzania kutokana na kuwepo kwa maambuizi makubwa na madhara yatokanayo na Corona.

Hancock alisema kuwa ili kuendelea kudhibiti maambukizi ndani ya Uingereza ni lazima kujilinda, na njia nzuri ni kuhakikisha wageni na wenyeji wanaotoka au wanaopitia Tanzania wanapimwa na baadaye wanawekwa karantini kwa siku 10 katika hoteli maalumu.

Kila anayeingia Uigereza lazima alipe Sh. 5,250,000 kabla hajaanza safari yake, na fedha hizi zitakuwa kwa ajili ya kujiweka karantini kwa siku 10.

Uamuzi huu wa Uingereza unaanza kutekelezwa kuanzia Februari 15, 2021.

Hancock aliongeza kuwa fedha hizo zitalipwa katika hoteli ambazo zimechaguliwa na serikali ya Uingereza na kuwa zimetengwa kutokana na kuwa na uwezo wa kuhudumia wageni bila usumbufu wakati wakijiangalia afya zao.

Alisema hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kutokuwa na maambukizi mapya na kutoka katika nchi ambazo zinaaminika kuwa katika hatari ya Corona.

Mbali na Tanzania, nchi zingine ambazo zimetajwa na Uingereza katika “kundi la hatari” ni pamoja na Angola, Argentina, Bolivia, Botswana, Brazil, Burundi, Cape Verde, Chile, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ecuador Eswatini, Guyana, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Panama, Paraguay, Peru, Ureno, Rwanda, Shelisheli, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Uruguay, Venezuela, Zambia na Zimbawe.

Tanzania iligundua kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza wa Corona Machi 16, mwaka jana na serikali ilianza kutangaza maambukizi mapya, idadi ya waliowekwa karantini na wale waliopona.

Hata hivyo, baada ya siku 45, serikali ilisitisha kutoa taarifa na takwimu za ugonjwa huo baada ya kupokea maelekezo ya Rais Magufuli. Hadi hatua hii inafikiwa, Tanzania ilikuwa imerekodi wagonjwa 519 na vifo 21 pekee.

Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi za kimataifa zimeendelea kuitaka Tanzania kuacha kuficha taarifa za ugonjwa huo na hata kukana kuwepo kwa Corona.

Like