Sabaya kizimbani kwa ujambazi

HATIMAYE aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Mkoa Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya (34) na walinzi wake watano, leo wamepandishwa kizimbani kujibu mashitaka sita yakiwemo ujambazi wa kutumia silaha, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Waendesha mashitaka wa serikali, Tumaini Kweka na Tresla Garvas, mbele ya Hakimu Mfawidhi Martha Mahumbuga na Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha, walisema kuwa Sabaya na wenzake walitenda makosa hayo Januari 20 mwaka huu na Februari 9, 2021 yeye akiwa mtumishi wa umma.

Sabaya anatuhumiwa kuunda genge la uhalifu na kutenda makosa ya uhujumu uchumi na kujipatia fedha kwa njia ya rushwa.

Ilielezwa alijipatia fedha kiasi cha Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Fransis Mroso mkazi eneo la kwa Mrombo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi akimhadaa kuwa angemnusuru asishitakiwe.

Katika kutenda makosa hayo Sabaya alikuwa na walinzi wake hao – John Aweyo maarufu kama Mike One, na Enock Mnkeni

Katika makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Sabaya anashitakiwa pamoja na walinzi wake wawili – Sylivester Nyengu (26) kwa jina maarufu Kicheche na Daniel Mbura (38). Mtuhumiwa mwingine ni Watson Mahomange.

Wanadaiwa kutenda kufanya ujambazi wa kutumia silaha Februari 9, baada kumfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa CCM Kata ya Sombetini, Arusha, na kumwibia Sh 390,000.

Katika tukio hilo lililotokea eneo la Bondeni jijini Arusha, Sabaya na walinzi hao pia wanatuhumiwa kumpiga mateke kumtishia silaha na kumpora simu na fedha Sh 35000 Ramadhani Ayoub

Mahakimu wote wawili walisema makosa hayo hayana dhamana na watuhumiwa hao walipelekwa mahabusu kwenye Gereza Kuu la Kisongo hadi June 18 kesi itakapotajwa tena.

Nje ya mahakama, mamia ya watu waliojitokeza walishangilia kitendo cha Sabaya kutiwa nguvuni na kufikishwa mahakamani.

Like
2