Sabaya, Makonda, Musiba: Kapu moja la “wahalifu”

LEO baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, kufikishwa mahakamani Arusha kujibu tuhuma za uhalifu zinazomkabili, mwandishi wa habari na mchambuzi Bollen Ngetti ameandika uchambuzi mfupi ufuatao kuhusu vinara wa genge la uhalifu lililosumbua jamii katika miaka mitano iliyopita. Endelea.

WAKATI mwingine unaweza kudhani ni shetani anaongoza binadamu. Lakini ukweli ni kwamba madaraka mikononi mwa mtu asiyestahili humlevya kama bangi au gongo.

Kilichotokea kwa vijana Sabaya na Paul Makonda ni ulevi wa kupindukia wa madaraka ambayo kwa namna yoyote Mungu asingeweza kufumbia macho. Ni matendo machafu na ya kishenzi yanayoweza kutendwa na tawala za kifashisti maana hata shetani anawashangaa.

Walikithiri katika kukamata watu, kutesa watu, kuteka watu, kudhulumu mali za watu kwa ubabe na kibri cha cheo. Hakika malipo huwa ni hapa hapa. Sasa wameanza kuonja joto la ujinga wa kumtegemea mwanadamu.

Labda niwaambia jambo ambalo lilitokea lakini halikuwahi kuandikwa. Kuna wakati aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alienda Afrika Kusini kukutana na wawekezaji waliokuwa na hamu ya kuwekeza Tanzania kipindi cha sakata la korosho.

Kwa kifupi, alipokutana nao katika Hoteli moja Jijini Johannesburg, pamoja na Balozi wetu (nimemsahau jina), katikati ya mkutano aliinuka mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Canada akasema:

“Mhe Waziri, tunatamani kuja Tanziania lakini kuna watu serikalini na wastaafu wanatuambia ‘kwa sasa sera za biashara Tanziania si rafiki msije.” Akaulizwa ushahidi.

Akatoa “chip” iliyowekwa kwenye projector na kuonesha kikao cha watu hao. Ni majina makubwa. Baadaye Mwijage alimpigia simu Rais John Magufuli kumjulisha habari hiyo.

Rais akamwambia, “umekuja uko na TBC1 wataje laivu.” Mwijage akamjibu, “Mhe majina haya ni mazito ngoja nikuletee uwataje mwenyewe.” Bosi akasema, “mbona Makonda tukimpa majina ya drug dealers anawataja?”

Mwijage akamjibu, “bosi nina familia, Makonda hana familia.” Hili lilitosha kumfukuzisha Mwijage kazi. Lakini hoja hapo si Mwijage bali ni “ujasiri wa kijinga wa Makonda;” kwamba alikuwa tayari kutenda jambo lolote hata kama ni baya.

Huu ndio ujasiri wa kijinga aliokuwa nao Sabaya, Makonda mwenyewe bila kumsahau Cyprian Musiba aliyejitwika ujasiri huo huo kutukana watu tena waliomzidi uadilifu, heshima na umri.

Nitashangaa kama Makonda naye atakwepa mkono wa PCCB pamoja na kukingiwa kifua na “Sukuma Gang” walioanza kupotezana dozedoze, lakini kwa hakika inabidi kikombe walichotumia kunywesha watu shubiri nao wakinywee.

Like
2