Polisi Dar wakamata Wanachadema 40, wawanyima dhamana

NDANI ya siku tatu, Jeshi la Polisi limekamata na kunyima dhamana wanachama wa Chadema zaidi ya 40 katika Jiji la Dar es Salaam, SAUTI KUBWA imeelezwa.

Leo pekee, polisi wamekamata wanachama 15, baada ya wengine 15 waliokamatwa jana katika mazingira ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walikokuwa wamekusanyika kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Juzi, polisi walikamata wengine 10 wakiwa katika kikao cha ndani kwenye Jimbo la Segerea.

Watu wote waliokamatwa wametawanywa katika vituo mbalimbali vya polisi, na wamezuiwa kuonwa na ndugu zao au mawakili wao.

Taarifa kutoka Kituo cha Polisi Mburahati zinasema kuwa mmoja wa waliokamatwa juzi Segerea, Julius Mwita, amekuwa na matatizo ya kiafya akiwa kituoni hapo lakini polisi wamegoma kumpeleka hospitali.

Mmoja wa mawakili wa Chadema ameiambia SAUTI KUBWA kuwa miongoni mwa waliokamatwa leo, mmoja aliachiwa. Hakumtaja jina.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wanachama waliopeleka chakula cha mchana kwa wenzao walikataliwa, na wengine walikamatwa.

Pamoja na kuandika maelezo polisi, watuhumiwa wote wamenyimwa dhamana. Wamesombwa kwa magari matatu tofauti na kupelekwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi ambako watakuwa hadi watakapodhaminiwa au kufikishwa mahakamani.

Waliokamatwa leo ni pamoja na Sharifa Suleman ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Catherine Ruge ambaye ni katibu mkuu wa BAWACHA, na Susan Kiwanga, aliyekuwa mbunge wa Mlimba.

Wengine ni Remina Peter, Bwire Nyangero Bwire, Neema Abdallah, Lambart Filbert, Sado Msomali, Ramla John, Mussa Bwashari, Christian Paul, Yusuph Manji, Raymond Baltazar na Rashid Rashid Jogaya.

Katika hali ya kushangaza, Waziri wa Mambo ya Ndani, Simbachawene, ametoa tamko kwa vyombo vya habari akizungumzia suala la fumanizi la kimapenzi badala ya mambo ya msingi yanayosumbua taifa.

Baadhi ya wasomaji wa SAUTI KUBWA wamesema kuwa wameshangazwa na tamko hilo la waziri ambalo limepuuza kabisa kauli juu ya polisi wanaonyanyasa, kuwatisha, kuwafunga na kuwanyima Watanzania haki ya kusikiliza kesi ambayo ina maslahi ya kitaifa.

Mmoja wao, ambaye hakupenda jina lake litajwe, amesema: “Ya Mbowe kimya, hili la ufuska ndio analitolea mwongozo? Tutaendelea na viongozi hawa wasiojali hadi lini?”

Like
2