Kutoka rumande Ukonga, Mbowe atuma ujumbe kwa Watanzania

FREEMAN Mbowe, mwenyekiti wa Chadema ambaye yupo rumande katika gereza la Ukonga, Dar es Salaam, ametuma ujumbe wa maandishi kwa Watanzania na kuwapa ujumbe maalumu. Huu hapa chini:

“Hali yangu ya kiafya ni nzuri na hakika sina tatizo lolote na wenyeji wangu (askari magereza-UKONGA) hapa. Lakini nasikitishwa na jinsi hawa vijana 3 (washtakiwa wenzangu) ambao niliwakuta gerezani lakini wamepigwa na kuumizwa sana, wamepitia mateso makali ndani ya mwaka mmoja (tangu wakamatwe August 2020 kule Moshi, Kilimanjaro).

“Wakiwa kwenye mikono ya jeshi la Polisi na mara zote wakishinikizwa kukiri kwenye camera kwamba wanafadhiliwa na mimi kufanya vitendo vya ugaidi walivyotuhumiwa na wao.

“Niliamua kuwa na walinzi hawa (waliowahi kuwa watumishi wa JWTZ) ili kuimarisha ulinzi wangu baada ya kushambuliwa na (watu wasiojulikana), Dodoma na kuvunjika mguu wangu.

“Lakini pia siridhishwi na vitendo vya Jeshi la Polisi kuendelea kuwakamata na kuwaweka mahabusu viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wanaojitokeza kusikiliza kesi yangu Mahakamani.

“Hata hivyo, nawashukuru Watanzania wote wanaoendelea kuniombea na kuliombea taifa letu, nchi nzima.

“Nawaomba sana, Watanzania wenzangu popote walipo, waungane na wasichoke katika kuendelea kuidai, kuitafuta na hatimaye kuandikwa kwa Katiba Mpya! Mungu awabariki, nawapenda sana.”

Freeman Aikaeli Mbowe
Gereza la UKONGA, DSM
08.8.2021

Like