Kesi ya Mbowe yashindikana kusikilizwa kwa masafa. Polisi wadhulumu wafuasi wa Chadema mahakamani

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo limelazimika kutumia nguvu kutawanya wafuasi na mashabiki wa Chadema waliokuwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuatilia mwenendo wa kesi inayomkabili mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Mbowe, ambaye leo ametimiza siku 16 akiwa ameshikiliwa na Polisi na baadaye Jeshi la Magereza, gerezani Ukonga, Dar es Salaam, anakabiliwa na  mashtaka mawili – kula njama za kutenda kosa na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

SAUTI KUBWA ilikuwepo katika maeneo ya mahakama hiyo. Ilishuhudia baadhi ya askari wakiwa na silaha za kivita wakisubiri amri kuwatawanya watu wasiokuwa na silaha au kuwa na dalili za kufanya fujo, waliobeba mabango, mengi yakiandikwa – “Mbowe si Gaidi” na mengine yakiwa na ujumbe “tunataka Katiba mpya.”

Ilipotimu saa 5.12 asubuhi, askari wa kikosi cha FFU walianza kukamata wafuasi na wanachama hao na kuwaingiza kwenye magari yao, huku baadhi wakiwapiga kwa mateke, marungu na vitako vya bunduki.

Askari hao waliendelea na kuwafukuza na kukamata wananchi hao kwa zaidi ya saa moja. Baadhi ya wananchi walikimbia, huku wengine wakikamatwa na kupakizwa ndani ya magari ya jeshi hilo. Haikufahamika walipelekwa kituo gani cha Polisi.

Kesi ya Mbowe pamoja na wenzake watatu ilipangwa kuitwa leo katika mahakama hiyo, lakini ilishindwa kuendelea kutokana na kile kilichoelezwa na mahakama hiyo kuwa ni “hitilafu ya kimtandao.”

Kufanyika kwa kesi hiyo kwa njia ya mtandao kumeelezwa na ofisa mmoja wa mahakama hiyo kwamba ni kuepusha maambukizi zaidi ya Corona, kutokana na kushamiri kwa janga la ugonjwa wa COVID-19 nchini.

“Mahakama haitaki kuwa chanzo cha maambukizi zaidi ya Corona, nyie waandishi ni mashuhuda wa ongezeko la ugonjwa huo na watu wanakufa, sasa kwanini sisi tuendeleze mikusanyiko na unajua kesi ya Mbowe ni kubwa, hivyo inavuta watu wengi,” alisema ofisa huyo bila kukubali kutajwa jina.

Wakili kingozi katika jopo la mawakili wanaomtetea Mbowe, Peter Kibatala alisema kwamba utaratibu wa kuendesha mashtaka kwa njia ya masafa, unakubalika kisheria, ingawa akaeleza kwamba kesho – Agosti 6, Mbowe na wenzake watakuwepo mahakamani. Kesi hiyo iliahirishwa leo kwa sababu ya changamoto za mfumo huo wa mawasiliano kutokuwa imara.

Mfumo huo ungetoa mwanya kwa Mbowe na wenzake kuendelea na kesi wakiwa gerezani Ukonga, huku hakimu, mawakili na watu wengine wakiwa Mahakama ya Kisutu, eneo la Upanga.

Katika kesi hiyo Mbowe anashitakiwa pamoja na watu wengine watatu ambao wanakabiliwa na makosa saba, yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Taarifa za awali zinasema kuwa wanachama wa Chadema wapatao 15 walikamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam. Waliotambuliwa hadi sasa ni Digna Daudi, Lazaro Sawe, Robert Moses, Musa Uswege, Margaret Kyai, Rose Mtwange, Ryoba Mzinga, Lazaro Simon, John Mbwana, Godwin Theobald, Shaban Noah, Gerald Shoo,Charles Kimaro, Joseph Muniko na mmoja aliyetambulika kwa jina moja, Norbert.

Matukio ya ukamataji raia, hasa wafuasi na wanachama wa Chadema, yameripotiwa katika mikoa kadhaa nchini. Kutoka Kagera, wajumbe wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) walivamiwa waiwa katika kikao cha ndani Bukoba mjini.

Waliokamatwa ni Dorice Herman, Arodia Projest, Specioza Kamala, Odeta Gaspar, Paulina Bilenge na Madina Ibrahim. Taarifa zinasema baadaye waliachiwa kwa dhamana.

Matukio mengine ya ukamataji hovyo yameripotiwa Tarime mkoani Mara, na Dodoma. Mkoani Dodoma, polisi wamevamia ofisi ya kanda ya kati wakakamata wanachama na kuchukua baadhi ya vifaa vya ofisi.

SAUTI KUBWA inaendelea kufuatilia matukio hayo.

Katika maeneo mengi nchini wananchi wamekuwa wanajitokeza kwa njia mbalimbali kupata sauti wakitaka Mbowe aachiwe huru. Maneno yanayotamba ambayo yamepamba kuta za nyumba, barabara, vyombo vya usafiri, miamba na kadhalika, ni “Mbowe si Gaidi!”

Yanatumiwa pia katika mitandao ya kijamii kama ujumbe maalumu wa kampeni ya kupinga dhuluma dhidi ya Mbowe na wapenda haki wengine Tanzania.

Like