Mwanajeshi, mwandishi watuhumiwa kuua mtu na kuficha mwili Mtwara. Ndugu wataka Sirro, Mabeyo wachukue hatua

IMETIMIA miezi miwili tangu Azizi Juma (40), mkazi wa Ligula katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Wilaya ya Mtwara, apotezwe akiwa mikononi mwa maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Jitihada za ndugu zake kumpata zimegonga mwamba, huku zikiwepo tuhuma kuwa aliuawa na kuzikwa kisirisiri tarehe 21 Novemba 2021.

Tuhuma zinaelekezwa kwa watu wawili – mwandishi wa habari anayemiliki TV ya mtandaoni na mwanajeshi wa JWTZ. Watuhumiwa hao ni wapangaji katika nyumba moja, na walikuwa wanamtuhumu Azizi kuwa aliiba Oven ya mmoja wao.

Ingawa majina ya watuhumiwa yanatajwa mitaani, katika hatua ya sasa SAUTI KUBWA haitayataja hadharani, kwa sababu za kimaadili, hadi wakati sahihi utakapowadia. Inaendelea kufuatilia suala hili katika ngazi za juu za JWTZ na Polisi baada ya maofisa wa chini mkoani humo kutoa ushirikiano hafifu.

Walikomzika Azizi bado hakujafahamika lakini vyanzo vyetu vinaeleza kuwa mauaji hayo yalifanyikia ndani ya Kambi ya Jeshi ya Neliendele, iliyopo wilayani humo..

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, mwandishi wa habari huyo na mwanajeshi walimtoa Azizi nyumbani kwake, wakaondoka naye kwa gari lenye namba za usajili T816 DNE aina ya Toyota Voltz

Kabla ya kumchukua Azizi, watu hao walikuwa wamemchukua rafiki yake anayejulikana kwa jina Geoffrey Kasembe, ambaye hushirikiana naye katika kutafuta na kufanya vibarua. Alikuwepo rafiki yao mwingine aitwaye Abdallah, ambaye naye alichukuliwa lakini hakuwa mtuhumiwa, lakini anadai alilazimisha achukuliwe ili kujua walikokuwa wanapelekwa.

Wanajeshi wapatao saba, wanaume, ndio walishiriki kuwapiga na kuwatesa Azizi na Geoffrey mara walipofikishwa kambini. Wakati wanajeshi hao wanapiga vijana hao, alikuwepo mwingine wa kike aliyekuwa ameshikilia bunduki, huku akizunguka zunguka katika eneo la tukio, akishuhudia kipigo hicho.

Inaelezwa kuwa yote haya yalianza tarehe 23 Oktoba 2021 mwandishi wa habari huyo alipowapa vijana hao kazi ya kusafisha makazi yake na mwanajeshi huyo, lakini baada ya kazi hakuwalipa.  

Kila walipoenda kumdai malipo aligoma kuwapatia. Baadaye, ikasikika kuwa vijana hao walikuwa wameondoka na Oven iliyokutwa nje ya nyumba hiyo, ili waiuze chuma chakavu wajilipe. Lakini wao hawakuwahi kukiri wizi huo, na waliendelea kudai malipo yao. 

Taarifa kutoka ndani ya JWTZ zinaeleza kuwa kipigo kizito kilielekezwa kwa Azizi aliyelengwa kuwa ndiye mwizi halisi wa Oven hiyo. Zinasema:

Wakati kipigo kikiendelea, Azizi alilalamika kuwa anaona giza, akaomba apewe maji ya kunywa. Mmoja wa wanajeshi waliokuwepo akasema hakuna haja ya kumpa maji, wakaendelea kumpiga.

Baadaye ya kipigo kikali, Azizi alipoteza fahamu, akaanza kutoa povu mdomoni. Wakaacha kumpiga, wakajaribu kumsimamisha, akashindwa kusimama. Wakammwagiua maji. Mara mmoja wa wanajeshi akasema kwa hofu, ‘mmeshatuletea msala!’

Kutokana na hali hiyo, walimuondoa rafiki yao Abdallah eneo la tukio na kumrudisha uraiani. Baada ya kuona hawezi kusimama, wakambeba Azizi na kumweka ndani ya buti ya gari iliyokuwa imemtoa kwake. Wakaelekea kusikojulikana hadi leo.

Wakati hayo yakiendelea walimpa Geoffey Kasembe maji na kumtaka aoge, kisha wakampa chai na kumrudisha uraiani akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo mguu alioumizwa.”

IGP Simon Sirro

Baada ya mateso hayo, ndugu wa Azizi walipewa taarifa za mateso ya ndugu yao ndani ya kambi ya jeshi, wakatoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, na watuhumiwa hao wawili walikamatwa na kufikishwa kituoni hapo.

Vyanzo vya kipolisi vimeieleza SAUTI KUBWA kuwa mwanajeshi huyo aligoma kutoa maelezo, kisha OCD alitoa amri ya kumweka rumande na wenzake ili uchunguzi ufanyike, lakini kesho yake mwanajeshi huyo alichukuliwa na wenzake kwa maelezo kuwa anapelekwa kwenye uongozi wao kwa sababu taratibu zao na za Jeshi na za Polisi zinatofautina.

Hata hivyo, Abdallah na Geoffrey waliachiwa. Geoffrey akapewa  PF3 kwa ajili ya matibabu lakini mwandishi wa habari aliendelea kushikiliwa kwa siku kadhaa kituoni hapo. Baadaye aliachiwa katika mazingira ya kutatanisha. Gari la mwanajeshi huyo liliendelea kuonekana limeegeshwa mbele ya kituo cha polisi hadi tarehe 8 Desemba 2021.

Kutokana na mazingira hayo, ndugu wa Azizi wamekua wakiomba msaada sehemu mbalimbali ili kumpata ndugu yao hata kama amekufa, huku wakitaka watuhumiwa wachukuliwe hatua. Lakini mmoja wa watuhumiwa anaonekana uraiani akiendelea na majukumu yake.

Jitihada za ndugu wa Azizi kuomba msaada wa vyombo vya habari viwasaidie kupiga kelele ili wampate ndugu yao, hazijazaa matunda kwa kile kinachoonekana kama mshikamano wa waandishi wa habari kulinda uhalifu wa mwenzao.

Baada ya kunusa taarifa hizi, SAUTI KUBWA ililazimika kutuma mwandishi maalumu kutoka Dar es Salaam ili kufuatilia mkasa huu. 

Imebainika pia kuwa mwandishi wa habari anayetuhumiwa, ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ana uhusiano wa karibu na viongozi wa serikali mkoani humo, ambao wanamkingia kifua, wamegoma kutoa ushirikiano na wameathiri pia uwajibikaji wa polisi katika sakata hili.

Hata vyanzo vya kipolisi vilivyozungumza na SAUTI KUBWA kuhusu mkasa huu viliomba visitajwe majina wala vyeo vyao. Lakini vimekiri kufahamu tukio hili. Polisi mmoja amesema: “Bila nguvu kutoka juu, hili litafukiwa na kuishia hapa hapa Mtwara.”

Familia ya Azizi, baada ya kukosa msaada juu ya sakata hili la ndugu yao, ilitonywa na watu kadhaa kuwa ndugu yao alifariki dunia siku ile ile ya kipigo. SAUTIKUBWA inafahamu kuwa ndugu zake kadhaa waliitana tarehe 02 Desemba 2021 wakaomba dua maalumu kwa ajili yake.

Ndugu zake Azizi wanataka wakuu wa majeshi – Polisi na JWTZ – waingilie kati ili ufanyike uchunguzi na wahusika wawajibishwe.

“Huu sasa ni mtihani kwa IGP (Simon Sirro) na CDF (Venance Mabeyo) kwani watu wao ndio wanahusika kudhulumu haki ya ndugu yetu. Tunafahamu ndugu yetu ameshauawa, lakini tunataka haki itendeke, ” amesema mmoja wa ndugu wa karibu wa Azizi.

Like
1