Mbowe: CCM Imeishiwa Pumzi

– Umeme, Maji, Biashara, vyatawala Uzinduzi Oparesheni +255, Tunduma

FREEMAN MBOWE, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeishiwa pumzi ya kushawishi wananchi wakiunge mkono.

Kwamba, bado wapo viongozi ndani ya Serikali ya CCM, wanaowaza kufanya “siasa za kishamba” za kujaribu kuidhibiti Chadema, badala ya kupambana na umaskini na matatizo ya msingi yanayowasibu wananchi, kama umeme, maji, barabara na vikwazo vinavyoathiri biashara ya mpakani baina ya Tanzania na nchi jirani.

Mbowe ameyasema hayo katika mkutano wa uzinduzi wa Oparesheni +255 ya Chadema katika Kanda ya Nyasa, uliofanyika leo mjini Tunduma.

“Tunduma (mpaka wa Tanzania na Zambia) ni lango la uchumi wa nchi. Kiongozi yeyote wa Serikali anayeongoza Tunduma anapaswa kuwa na akili yenye ya kukuza biashara na kulinda lango la uchumi wa nchi. Nimesikitishwa sana na mambo yaliyotendeka Tunduma ya kujaribu kuharibu mkutano huu. Huyu aliyejaribu kufanya hivyo ni mshamba. Hizo ni dalili za mtu anayekata roho. CCM wameishiwa pumnzi. Siku Chadema ikiingia madarakani tutahakikisha Tunduma inaishi kwa hadhi yake kama lango la uchumi wa nchi”, alisema Mbowe na kushangiliwa.

Licha ya Mkuu wa wilaya ya Momba, Kenan Kihongosi, kudaiwa kuhujumu mkutano huo wa Chadema, kuandaa mkutano wa ghafla na wafanyabiashara kwa lengo la kuifanya Chadema ikose uwanja ulio zoeleka kwa mikutano ya hadhara, bado wananchi wa Tunduma walijitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa Chadema.

Akizungumzia matatizo ya maji na umeme, Mbowe alisema:

“Tunduma, mji ambao ni lango la uchumi la nchi yetu unakosaje maji? Zambia hawana bandari. Zaidi ya nusu ya mizigo yao inapitia Tanzania. Zambia wana umeme, sisi hatuna umeme. Zambia hawana gesi asilia inayofaa kuzalisha umeme wa kutosha, sisi tunayo lakini hatuna umeme. Makambako kuna bonde la upepo unaotosha kuzalisha megawatts nyingi, lakini hatuna umeme. Tuna serikali au matope?”, alihoji Mbowe na wananchi wakajibu “matope”

Alisema Tanzania ina shirika moja tu, lisilo na mshindani (TANESCO), linalozalisha na kuuza umeme, lakini pamoja na kuuza umeme wa bei ya juu bado Serikali ya CCM imeshindwa kuzalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya nchi na wananchi.

Sera ya Chadema ni kuvutia uwekezaji wa kutosha na wenye ushindani wa makampuni mengi binafsi katika kuzalisha, kusambaza na kuuza umeme wa uhakika, ulio nafuu na unaofaa kwa matumizi endelevu ya shughuli za kiuchumi na matumizi ya kawaida.

“Shida ya umeme na mafuta zimesababisha gharama za uzalishaji ziwe juu na hivyo kupandisha gharama za maisha. Siasa si kazi ya Mbowe na Chadema. Msije kwenye mikutano ya siasa kama vile mnakuja kutazama show ya Diamond. Siasa ni maisha yenu. Wajibu wa kuikomboa nchi hii ni wa wananchi wote. Usivae nguo ya Chadema kama huwezi hata kumshawishi mkeo kujiunga na Chadema”, alisema Mbowe.

Katika hatua nyingine, Mwanasiasa huyo aliendeleza utaratibu wake wa kuwapigisha wananchi kura ya wazi kuhusu mkataba wa kuendeleza na kuboresha ufanisi wa bandari na maeneo mengine ya kiuchumi, ulioingiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai.

Katika kura hiyo, wananchi wote waliohudhuria mkutano huo, wamepinga hatua ya Serikali ya Tanzania kuingia mkataba huo na Dubai.

Mkataba huo, pamoja na mambo mengine, umekabidhi bandari zote za upande wa Tanganyika chini ya uendeshaji wa kampuni ya Dubai ya DP World.

Like