Mbowe aungurumia Misenyi, Karagwe

– Anadi Sera ya Uchumi wa Mipakani
– Akuta vilio vya Afya, Ardhi, Maji na NIDA
– Asaidia Mzee wa miaka 101 aliyevunjiwa nyumba

MAMIA ya wananchi wa Mutukula, Kanyigo na Bunazi, wilayani Misenyi, na Rwambaizi, Nyaishozi na Kayanga, wilayani Karagwe, mkoani Kagera, wamejitokeza kwa wingi katika mikutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), iliyohutubiwa leo na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Katika mikutano hiyo, Mbowe, alinadi zaidi sera ya Chadema, ya kuufanyia mageuzi makubwa uchumi unaotegemea biashara ya mipakani baina ya Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki.

Akifafanua sera hiyo, alisema Chadema ikichukua dola itarekebisha mifumo ya kodi, tozo, ushuru na kuondoa vikwazo vyote vinavyorudisha nyuma biashara na uchumi wa mipakani.

Kwamba, sera hiyo ya Chadema, itawapatia wananchi fursa pana ya kutengeneza vipato vyao na wakati huo huo itaongeza mapato ya serikali na maendeleo ya nchi, kwani motisha ya kuondoa vikwazo, itaongeza maradufu wingi wa mizigo na biashara inayopita mipakani tofauti na ilivyo sasa.

*”Duniani kote, mipaka ya nchi ni fursa ya kuwatajirisha wananchi kibiashara, lakini kwa Tanzania, mipaka ni laana. Hapa Mutukula, Waganda wanauza zaidi kwetu kuliko sisi tunavyouza kwao, kwasababu serikali ya CCM imewazuia msiuze Kahawa, mchele na mazao mengine Uganda, wakati Uganda kuna bei nzuri zaidi. Akili gani hii?”*, alihoji Mbowe.

*”Kwasababu ya kodi kubwa, tozo na ushuru, bidhaa nyingi kama mafuta ya kupikia, sukari na sabuni zinauzwa bei ghali Tanzania, lakini ni nafuu sana Uganda*

*Kila mahali mmewekewa barriers (vizuizi) vya kutozwa ushuru wa mazao. Mzigo mmoja unatozwa ushuru mara nyingi bila sababu za msingi. Chadema tutarekebisha kodi, ushuru na tozo. Chadema tutafuta vikwazo vyote ili mfanye biashara zenu kwa uhuru”* alisema Mbowe na kushangiliwa na wananchi wa Mutukula.

Katika hatua nyingine, wananchi wa Misenyi na Karagwe walilalamikia kutopewa vitambulisho vya taifa (NIDA) licha ya kutimiza taratibu zote, huku wengine wakidai kunyimwa vitambulisho hivyo kwa kudaiwa kuwa si raia wa Tanzania.

Pia, wananchi wa Mtukula waliokuwa wakazi kwenye vitongoji vitatu vya Mabalagera, Kyarukaya na Kachumbi vya Mutukula walilalamikia kuondolewa kwenye maeneo yao na serikali bila kupewa fidia na maeneo hayo kupewa mwekezaji wa mifugo.

Miongoni mwa wahanga hao, ni mzee Terestori Ludovick, mwenye miaka 101, aliyevunjiwa nyumba yake kwa madai kuwa alivamia eneo hilo alilopewa mwekezaji.

Akionesha kuguswa na sakata hilo, Mbowe alitoa msaada wa shilingi milioni mbili kwaajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya mzee huyo, huku akisisitiza kuwa ni sharti wananchi waachane na CCM, ndipo ubaguzi wa uraia na mateso ya kuporwa ardhi zao yatakapokwisha.

Aidha, Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, na Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje, waliahidi kuwa Chadema itaboresha afya na maji ambazo zililalamikiwa sana na wananchi wa Kanyigo, Bunazi, Rwambizi, Nyaishozi na Kayanga.

Wananchi wa Mtukula walieleza kuwa huduma za afya ni duni, lakini zinatolewa kwa gharama kubwa, hali inayowalazimu kuvuka mpaka na kwenda kufuata matibabu bora na nafuu nchini Uganda.

Akiwa Kayanga, Mbowe pamoja na mambo mengine, alitoa rai kwa askari wa jeshi la polisi kutokubali kutumiwa vibaya na CCM kwa kuisaidia kufanya kile alichokiita wizi wa kura, kwani kufanya hivyo kunawanyima wao wenyewe polisi pamoja na wananchi wote fursa ya kuongozwa na serikali bora.

Like