BARUA YA WAZI KWA RAIS SAMIA (2)

Rais Samia Suluhu Hassan

Hii ni sehemu ya pili ya barua hii, ikianzia ilipoishia sehemu ya kwanza kuhusu mkataba wa bandari katika muktadha wa “biashara kama msingi wa uchumi.” Endelea.

SHERIA KAMA NGUZO YA KUENDESHA UCHUMI

Mheshimiwa rais, sheria ni zana ya kuendesha uchumi na zaidi, zana katika kusimamia uchumi mpana. Sheria huwekwa au hutumiwa kulinda maslahi ya uchumi wa nchi kwa kuzingatia malengo ya muda mrefu kwenye yale maswali makuu matano. Kwa hiyo, ni sharti kuanza na fikra za kiuchumi kabla ya kuwa na sheria za kusimamia uchumi huo.

Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa kwenye nchi yetu, tumefanya kinyume na hasa kwenye usimamizi wa sera za uchumi mpana. Tumekuwa na utaratibu wa kuanza na sheria na baadaye kufikiri juu ya malengo mapana ya uchumi wetu. Kwa maana nyingine, ni kuwa, sheria zimekuwa zikiamua malengo mapana ya uchumi wetu.

Changamoto kubwa hapa, imekuwa kwenye maeneo yanayohusu jinsi ya kuvuna rasilimali zetu kupitia uwekezaji na hasa uwekezaji kutoka nje. Tulipoamua kuvuna rasilimali zetu za madini tuliafuata njia hii, tumefuata njia hii kwenye sekta ya uhifadhi, tumefanya hivi kwenye sekta ya mawasiliano, tumefanya hivi kwenye sekta ya nishati na tumefanya hivi hata kwenye sekta ya aridhi kwenye sehemu nyingi.

Mheshimiwa rais, jambo kubwa katika yote haya ni jinsi tunavyoshughulika na mikataba. Mikataba ambayo kwa sababu ya tatizo la kimsingi, tumelazimika kuitetea kwa sababu machoni petu sheria imechukua nafasi ya malengo mapana ya kiuchumi badala ya kuwa zana ya kusimamia uchumi.

Mkataba wa kati ya Tanzania na Dubai ni hatua nyingine “mbele” ya kuendelea ya kuweka sheria kwenye kitovu cha malengo mapana ya kiuchumi badala ya malengo yenyewe.

Mkataba huu hautoi nafasi kwa Tanzania kuwa na umiliki wa haki za kimkakati kwenye rubaa za myororo ugavi duniani. Baada ya mafunzo tuliyoyapata kutokana na UVIKO-19 ni kuwa; bandari ni maeneo ya kimkakati kuliko ilivyowahi kuwa kiuchumi kabla ya hapo. Kuwa na mkataba ambao unajaribu kupokonya nchi umiliki wa mkakati huo kwa hoja za kisheria ni dhahama kwa muono wa siku za usoni.

Aidha, mkataba huu ambao unakanyaga malengo ya kiuchumi ya muda mrefu, unatumia mwanya huo kuzitumia sheria za ndani ili kurahisisha shughuli za muwekezaji mathalani Ibara ya ishirini na saba(27) ya mkataba wenyewe.

Ni kwa njia hii sheria zetu za ndani hata zile ambazo zilibuniwa ili kulinda maslahi ya uchumi wetu, zitatakiwa kukarabatiwa ili kukidhi matakwa ya mkataba. Ikumbukwe kuwa ukarabati huo, unaweza kuwa unalenga kurahisisha shughuli za mwekezaji wa sasa wa kwenye bandari lakini athari zake zikawa kwenye sekta nyingi zaidi.

KIINI KATI YA RASILIMALI ZA ASILI NA RASILIMALI ZA KIUCHUMI

Mh Rais, ili nchi yetu kuwa na ustawi wa kiuchumi ni sharti iwe na uwezo wa kuzibadili rasilimali zetu za asili kuwa rasilimali za kiuchumi. Hii maana yake ni kuzifanya rasilimali zetu kama bahari na mito kuwa na thamani zaidi na inayotumiwa na watu.

Hii ni pamoja na kuongeza tija kwenye rasilimali hizo ili kutengeneza mazingira ya kuimarisha sekta nyinginezo kwenye uchumi. Kuifanya kazi hiyo kunahitaji maarifa ya kutosha na usimamizi wa uchumi usiokuwa na mawaa. Maarifa na usimamizi huo, unahitaji masuala makuu matatu.

  1. Rasilimali watu. Hapa swali la kwanza ni; Watu wangu wako wapi? na siyo Wawekezaji wangu wako wapi?. Swali la wawekezaji linajibiwa na swali la watu wangu na siyo swali la watu wangu kujibiwa na swali wawekezaji wangu.
  2. Taasisi Imara. Hapa swali kuu ni; Taasisi zetu ziko wapi? na siyo Fedha zao ziko wapi?
  3. Muhimu hapa ni kuwa, taasisi imara na zenye uwezo kimuundo na kimaarifa zinakuwa na uwezo wa kubuni mikakati ya kupata fedha kwenye uchumi bila kuondoa hali ya kumiliki nguzo kuu za uchumi wenyewe.
  4. Siasa safi. Hapa kazi kubwa ni kuzifanya siasa zioane na malengo makuu ya kiuchumi.
  5. Kazi kubwa ya eneo hili ni kuwa na siasa ambazo zinazingatia somo la kwanza la uchumi ambalo ni kuelewa kuwa;  muda wote rasilimali ni hafifu na zenye matumizi mengi na kuwa siasa haziwezi kuwa njia ya kudogosha na kudhibiti somo la kwanza la uchumi.

Mh Rais, kwa muda mrefu sasa, taifa letu linahangaika sana juu ya jinsi gani tutapatia kiungo cha kutuvusha kutoka rasilimali za asili kuwa rasilimali za kiuchumi. Kwa ujumla hatujafanya vizuri na sehemu nyingi tumefanya makosa mengi kwa kuanza na maswali ambayo yanahitaji kujibiwa na maswali tuliyoshindwa kuyabaini.

Katika mapambano yetu ya kukuza uchumi tumejikuta tunadhani kuwa bila kuwa na uendelezaji wa watu tunaweza kuchupa kiuchumi kwa kutumia wawekezaji walioandaliwa na mataifa mengine.

Hii si kusema kuwa; hutakiwi kupata wawekezaji kutoka nchi nyingine, lakini ni kukiri tu kuwa; wawekezaji(watu) walioandaliwa na nchi nyingine watawajibika zaidi kwa nchi zao zilizowaandaa kuliko nchi zilizowakodisha.

Vivyo hivyo, taasisi zilizoandaliwa na kunolewa na nchi zingine haziwezi kuwa na wajibu mkubwa kwa nchi zilizokopa taasisi hizo.

Hii ni sawa pia kwenye siasa. Siasa ambazo zimeratibiwa kuzaa wawekezaji mahiri na taasisi imara haziwezi kuwa zinafanya hivyo ili kuboresha maisha ya watu wa nchi zingine. Siasa hizo zina wajibu kwanza nyumbani kupitia wawekezaji na taasisi zinazozituma huko duniani.

Hapa kwetu, tumekuwa na wawekezaji ndani ya nchi yetu kwa ajili ya nchi wanakotoka wawekezaji hao. Tumekuwa na taasisi au kampuni ambazo zinalinda maslahi ya nchi zilikotoka na tumekuwa na mikataba kwenye uwekezaji nchini kwetu inayolinda siasa za nchi ambako mikataba hiyo inaasisiwa.

Mkataba kati ya Tanzania na Dubai ni muendelezo wa kushindwa kubaini kiini kutoka kwenye kuwa na rasilimali za asili tu ili kuzifanya ziwe rasilimali za kiuchumi.

Mkataba unaingiwa kwenye mazingira ya kidharura mno kana kwamba ni lazima tuwe na wawekezaji wao leo; kana kwamba ni lazima kuwa na taasis yao leo; na kana kwamba ni lazima serikali ya Tanzania iingie makubaliano na kampuni yao leo ambayo ni matokeo ya siasa zao.

Mheshimiwa rais, ipo dhana kuwa unapokuwa nchi maskini na huna mtaji na teknolojia, basi ukubali wanachokupa wao hata kama hakikidhi malengo mapana ya uchumi wako. Na hii siyo hali iliyoanza wakati wako. Ni utamaduni tulioujenga kwa muda mrefu na kuupa vionjo vizuri hata vya misemo isiyokuwa na mantiki kiuchumi.

Mwaka( 2004) nikiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu, nilitazama kipindi cha mahojiano kuhusu hali yetu ya uchumi kupitia kituo cha televisheni cha channel ten. Mgeni alikuwa hayati Mzee Kingunge Ngombale Mwiru.

Kwenye mahojiano hayo, Mzee Kingunge alitetea uwekezaji unaolipa hasara taifa kwa kusema: “kwenye haya mazingira ambayo huna uwezo wa kuendeleza rasilimali zako, unapokea unachokipata mpaka pale utakapopata unachokitaka.”

Mzee Kingunge alikuwa akitetea msimamo wa serikali juu ya sera za ubinafsishaji na uwekezaji wakati huo. Na kwa kweli, kwa wakati huo, nilijihisi kuwa nimejifunza jambo kubwa la busara sana.

Nilitumia msemo huo kila nilipopata nafasi ya kuutumia kuonesha ubabe wangu wa kuelewa mambo. Nilipata kilema hicho kwa muda mrefu sana na ilinitumia muda mrefu mpaka nilipokuja kutibu elemavu huo.

Hata hivyo, bado kilema hiki ni kikubwa kwenye muundo na mfumo wa uchumi wetu. Uendeshaji wa uchumi wetu umegota kwenye huo muono wa Mzee Kingunge.

Mheshimiwa rais, zipo fikra na vitendo vya kutosha kuwa, serikali yako bado inaamini kwenye uchumi wa pokea unachokipata mpaka utakapopata unachokitaka.

Njia hii ina nia njema lakini ina matokeo hafifu na yenye kuzubaisha uchumi wetu. Kwa kuwa tunaishi kwenye dunia ambayo ni rahisi kujifunza na kupata taarifa nyingi kuliko ilivyowahi kuwa kwenye maisha ya mwanadamu, na sisi tunao wajibu wa kujifunza haraka na kuhakikisha hatufanyi makosa waliyofanya waliotutangulia.

Ni kwa msingi huu, dunia ina ushahidi wa kutosha wa kuwa; kila wakati ambapo nchi zilijiondoa kwenye umaskini na kutengeneza uendelevu wa uchumi kwa vizazi vinavyokuja, zilibaini kiini endelevu kwenye safari yao ya kutoka kuwa nchi zenye rasilimali za asili na kuzifanya kuwa rasilimali za kiuchumi.

Na kwa mpangilio, hazikuweka matumaini yao kwa “pokea unachokipata mpaka utakapopata unachokitaka”. Na umekuwepo ushahidi kwa miaka zaidi ya elfu mbili(2000) iliyopita.

Mheshimiwa rais, ni kwa msingi huo; kwa heshima, nakuomba uwatake wasaidizi wako wakuletee kitabu kiitwacho Contours of the World Economy: 1-2030 cha Angus Maddison kilichochapishwa mwaka 2007. Kitabu hiki kina sehemu kuu tatu;

  1. Sehemu ya kwanza ni kuhusu himaya ya Roma na sababu zilizosaidia au kuzubaisha uimarikaji wa uchumi Asia, Afrika, Europe na Amerika.
  2. Sehemu ya pili inahusu zana za kuchambua uchumi mpana kati ya karne ya 17 mpaka leo.
  3. Sehemu ya tatu ni kuhusu vitu vitakavyoamua hali ya mambo kiuchumi kufikia mwaka 2030.

Mheshimiwa rais, kitabu hiki kinaweza kuwa nguzo kuu kwenye safari ya kuvuka kutoka kwenye rasilimali za asili na kuzifanya rasilimali za kiuchumi kwa uendelevu.

Itaendelea kesho na sehemu ya tatu.

Like
1