Mange au Magufuli? Mshindi amepatikana

KWA wiki kadhaa kumekuwepo mchuano mkali kati ya mwanaharakati Mange Kimambi na Rais John Magufuli wa Tanzania. Mange, mwanamitindo na mwanaharakati wa uhuru wa kujieleza, anatumia mitandao ya kijamii. Magufuli anatumia vyombo vya dola. Mange anahamasisha wananchi waandamane kupinga utawala wa Magufuli. Magufuli anatumia polisi kutisha wananchi. Maandamano ya awali yalipangwa yafanyike tarehe 26 Aprili 2018.

Kumetokea nini tarehe 26 Aprili?

Katika siku tatu kuelekea siku ya maandamano, polisi nchi nzima wamekuwa wanakamata watu – hasa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika maeneoo mbalimbali. Baadhi yao wamelazwa kwenye vituo vya polisi, wengine wamehojiwa, wametishwa, na wameachiwa baada ya kuonywa kwamba wasithubutu kuandamana au kuhamasisha wananchi kuandamana.

Siku moja kabla ya maandamano, jeshi la polisi lilitoa tangazo kupitia vyombo vya habari kwamba wananchi ambao wangeandamana wangepata kipigo cha mbwa koko. Kuanzia usiku wa tarehe 25 Aprili 2018, polisi walikuwa barabarani wakiwa na silaha za moto.

Kesho yake asubuhi, katika maeneo mengi ya nchi, wananchi walishuhudia misafara ya magari ya polisi wenye silaha nzito. Kimsingi, ingawa polisi walifanya hivyo wakidhani wanazuia maandamano, wao ndio walikuwa wanaandamana.

Hapa kuna mambo ya kujifunza

Kwanza, Mange amefanikiwa kutikisa serikali nzima kwa wiki kadhaa mfululizo. Na inavyoonekana, atendelea kuitikisa. Wananchi, kwa kutambua nguvu yake hiyo, tayari wanamwita jeshi la mtu mmoja. Serikali nzima inakimbizana na mtu ambaye haimwoni. Vikao visivyoisha na vinafanyika usiku na mchana kupambana na binti mmoja siye na rungu wala jiwe, “anayeishi mtandaoni.”

Pili, tuna taarifa zisizotiliwa shaka kuwa usiku wa kuamkia siku ya maandamano, Rais Magufuli hakupata usingizi mnono. Alikuwa anahaha, anapiga simu huku na kule, anafanya vikao visivyo rasmi, huku akijiuliza maswali ambayo hakupata majibu.

Anajiuliza, “Mange anapata wapi nguvu ya kusumbua serikali yangu? Nimefanya nini hasa, hadi watu hawa wanisumbue na wanichukie kiasi hiki?”

Kwa maoni ya Rais Magufuli, Mange anapewa kiburi na Chadema. Wazo hili linatuleta katika hoja ya tatu, kwamba tuna rais asiyejua nchi inaelekea wapi; tuna serikali ambayo inatumia nguvu nyingi, akili ndogo, inayojihangaisha na mambo madogo madogo huku ikishindwa kulinda usalama wa taifa. Inashindwa kuona na kutafakari hoja za Mange, ambazo kimsingi ni hoja za wananchi, inakimbilia kutafuta mchawi katika vyama vya upinzani, hasa Chadema. Ni serikali iliyojaa hofu kwa sababu ya hofu alizonazo rais mwenyewe.

Na sasa nasikia Rais Magufuli ameamuru mashushu wake waongeze nguvu ya kufuatilia vikao rasmi na visivyo rasmi vya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Magufuli bado anadhani nguvu ya Mange inatoka Chadema. Haoni kwamba udhaifu wake ndio unampa nguvu Mange na wananchi wanaomfuata.

Nne, kwamba Rais Magufuli haoni makosa yake ni ajabu na hasara kubwa kwa nchi. Hasikii vilio vya wananchi. Haoni madhara ya damu ya raia anayomwaga. Haoni madhara ya kufunga midomo wabunge, waandishi wa habari na wanaharakati. Haoni hasara inayoweza kutokana na vitisho vyake vya kuvunja miguu wananchi wake. Haoni makosa kwa kuzuia uhuru wa wananchi kufikiri, kutoa maoni na kukusanyika. Kimsingi, upofu huu wa rais, ni msiba kwa taifa!

Je, maandamano yamefanikiwa au yameshindwa?

Hapa kuna maoni mchanganyiko. Wanaotazama juu juu, waliotarajia ‘tifu’ mitaani, wanaopenda kazi ya misuli na mituringa, waliotarajia kuona umati mkubwa wa watu barabarani, wanasema maandamano hayakufanikiwa. Hata rais anadhani amefaulu kuyazima.

Lakini kuna wengine wanaotazama suala hili kwa kina zaidi. Kwa usumbufu ambao serikali imepata kukimbiza watu ambao haiwaoni; kwa pesa ambazo zimetumia kuandaa na kulipa polisi wanaotumwa kwenye shughuli hii; kwa adha iliyowapata polisi mitaani kunyeshewa mvua kwa zaidi ya saa mbili wakikimbia hovyo kama vichaa (katika maeneo ya Mwanza na kwingineko); kwa hofu iliyompata Rais Magufuli usiku kucha anawaza jinsi ya kudhibiti Mange na wananchi wanaomsikiliza binti huyo; kwa nguvu ya akili ya rais na watu wake inayopotea bure kuwaza maandamano; kwa dhamira yao kuua wananchi halafu wakawakosa; kwa usumbufu wa jumla wa kisakolojia na kimfumo katika serikali; nadiriki kusema maandamano yamefanikiwa katika siku ya kwanza.

Kama shabaha ilikuwa ni kumwondoa Magufuli madarakani tarehe 26, bado maandamano hayajafanikiwa. Kama shabaha ilikuwa kumsumbua na kumfikishia ujumbe kwamba wananchi wamemchoka, maandamano yamefanikiwa. Kama shabaha ilikuwa kutesa akili yake na askari wake, maandamano yamefanikiwa. Kama shabaha ilikuwa ni kumjulisha kuwa pamoja na vyombo vyote alivyo navyo, siku wananchi wakiamua kumwondoa watafanikiwa bila kuingia barabarani, maandamano yamefanikiwa. Ajue tu kuwa siku ya kumwondoa, wananchi hawatampa taarifa mapema. Atakutana nao sehemu asiyotarajia, bila kujiandaa.

Vile vile, kwa kuwa Magufuli anaamini katika mabavu, njia ya kupambana naye si kutumia mabavu. Ukitumia mabavu unamsaidia kufanikisha ajenda yake ya kuua watu. Kama Mange amefaulu kumtikisa hivi, kwa akili ya mtu mmoja, hebu tafakari akili za mamilioni ya Watanzania “walio nyuma ya Mange,” na mamilioni ya wananchi wasiopenda ubabe na ukatili wa Magufuli!

Watanzania kadhaa waishio ughaibuni waliandamana katika maeneo yao. Walibeba mabango kuonyesha hisia zao. Nani anakumbuka kama jambo hili liliwahi kutokea tangu 1961? Wapi, na lini?

Zaidi ya hayo, hebu tazama vikosi vya polisi vilivyozurura barabarani eti vinazuia maandamano. Tazama magari yao, mabomu yao, mitutu yao ya bunduki, magwanda yao na mbwembwe zao. Jiulize. Watu wote hawa, na nguvu zote hizi wanazotumia, wanapambana na nani? Mange Kimambi? Kama bado wanajisifu wameshinda, waulize tena. Mmemshinda nani?

Magufuli ajue au asijue, kutumia polisi ili wazuie wananchi kuandamana hakumuingizi yeye kwenye mioyo ya wananchi. Kama anapenda wananchi, na kama ana uhakika kuwa anawatendea mema na wanampenda, kwanini anawaogopa? Huwezi kushinda wananchi wanaoandamana mioyoni mwao dhidi yako.

Kama unataka kujua kwamba Rais Magufuli ana hofu, fuatilia kwanini aliingia uwanjani kwenye sherehe za Muungano bila kuwa katika gari la wazi na kupunga mkono kama tulivyozoea. Haijawahi kutokea.

Ends

Like
42
16 Comments
  1. Nellie muganda 6 years ago
    Reply

    Asante kwa ujasiri wako.Damu ya Bwana Yesu iwafunike. Amen

    1

    0
  2. Sebastian 6 years ago
    Reply

    Hakika na ni dhahiri maandamano yamefanikiwa sana tena kwa asilimia mia maana nchi nzima polisi wameandama kwa niaba yetu!

    Nchi inaendeshwa na jocker na magarasa yanayoitwa mawazari. Wanatia aibu na wanatufanya tunaonekana wapumbavu kwa majirani zetu Kenya. Mkenya mmoja aliniuliza juzi nilipokuwa Nairobi hivi ilikuwaje mkamchagua mtu mpumbavu kuwaongoza! Nilibaki tu mdomo wazi maana sikuwa na jibu sahihi maana kuna ukweli katika swali na maoni yake.

    Nadhani huu sasa ni wakati wa kujiunga na Chadema kwa nguvu zote. Wanaoondoka huko ni wapumbavu tu na wapuuzi.

    Nina amini Lissu ni kiongozi anayefaa kuingoza Tanzania katika wakati huu wa giza.

    Nasikia Pombe anajilimbikizia pesa kwa ajili ya 2020 maana anafahamu hata pata msaada kutoka kwa wafanyabiashara ndio maana anawaumiza na kuwakamua iliawe vizuri kipindi cha uchaguzi!

    Wakati mwingine watanzania tuwe makini kuchagua viongozi mtu hata jina lake ni dhambi tunakimbilia kumweka patakatifu angalia sasa anavyopatia najisi.

    Ee Mola tuchukulie roho hii ni ya kuzimu haitufai ikafie mbele huko!

    Sebastian

    2

    0
  3. mr ndege 6 years ago
    Reply

    Kiukweli mange kafanikiwa ila watz ndiyo tumemuangusha

    0

    0
  4. Tang Zhou 6 years ago
    Reply

    Tutaandamana tena Mei Mosi…hadi ATUBU!

    1

    0
  5. joy 6 years ago
    Reply

    jamani fungua account pia instagram na fb ili iwe raisi watu kufikisha ujumbe

    0

    1
    • Ansbert Ngurumo 6 years ago
      Reply

      Tayari zimeshafunguliwa akaunti za Fb, Twitter, Instagram etc. Asante!

      2

      0
      • Dodo 6 years ago
        Reply

        Majina tuweze kufollow

        0

        0
  6. KitichaMpingo 6 years ago
    Reply

    Dunia ya kutumia nguvu imepitwa na wakati na Magu anaamini wakati wa nguvu ni sasa, kila anachofanya si kipya duniani! Mange yupo safi Maana anatumia kifaa cha wakati huu yaani akili wakati Huyu kiongozi anadhani nguvu zinaweza kuliko utu na heshima!

    0

    1
  7. Mwamba 6 years ago
    Reply

    Uko vzr mkuu

    1

    0
  8. Mti mkavu 6 years ago
    Reply

    Hahahahhahaha. ..

    0

    0
  9. Billy 6 years ago
    Reply

    Ahsante Ansbert,
    Hakika umesikika kwa Sauti Kubwa,
    Wenye uelewa wataelewa.
    Endelea kupambana, tunakuunga mkono.

    0

    0
  10. judith michael 6 years ago
    Reply

    barikiwa na mungu awalinde huko mliko

    0

    0
  11. Mtanzania 6 years ago
    Reply

    Mange kashinda. Mange yuko peke yake . Amemtingisha dikteta kulitumia jeshi letu la watu mil 55???

    0

    0
  12. makaveli 6 years ago
    Reply

    The truth won .’God save our queen’ I say this with pride. Keep up the fight.

    0

    0
  13. Kilogoja 6 years ago
    Reply

    Princess Mange ni mshindi daima!

    “Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.”
    (Methali 28: )

    0

    0
  14. Mayonene 6 years ago
    Reply

    Kazaazi kwelikweli

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.