Madiwani Ngorongoro wagomea ardhi yao kumegwa tena

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro limegoma kupisha mpango wa matumizi bora wa ardhi wa wilaya hiyo kwa kile walichoeleza kuwa hauna maslahi kwa wananchi kwani haukuwashirikisha wananchi kuanzia ngazi za vijiji na umelenga kutwaa ardhi zaidi.

Aidha, wamedai kuwa mpango huo umelenga kuhalalisha hatua ya serikali ya kutwaa ardhi yao kilometa za Mraba 1,500 kwenye eneo la Loliondo ambalo kwa sasa limepandishwa hadhi na kuwa pori la Pololeti na uondoaji wa wananchi kwenye tarafa ya Ngorongoro.

Madiwani hao 30 kati ya 32 wanaounda halmashauri hiyo walitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki (Mei 19, mwaka huu) mara baada ya kugoma agenda hiyo kujadiliwa na kupitishwa kwenye wa baraza la madiwani la halmashauri hiyo.

Walisema kuwa mpango huo haujawahi kuwa kipaumbele cha halmashauri hiyo bali umeletwa na serikali kuu kwa kushirikiana na mashirika ua uhifadhi NCAA, FZS na KfW ili kuhalalisha umegaji wa ardhi kilometa za mraba 1,500 kwenye tarafa ya Loliondo.

“Wananchi wa Ngorongoro hawajawahi kuridhia kwa vyovyote vile. Hivyo kaqma baraza la madiwani hatutaridhia mpango huu,” ilisisitiza sehemu ya tamko hilo la pamoja.

Madiwani hao wanadai kuwa kuna mashauri manne kwenye mahakama Kuu ya Tanzania na  Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, (EACJ) kuhusiana na ardhi ya wilaya hiyo hivyo kufanya jambo lolote kwenye ardhi hiyo ni kinyume cha sheria na nidharau kwa mahakama hizo.

“Mpango wa matumizi ya ardhi wa wilaya ya Ngorongoro haukufuata matakwa ya sheria inayotaka ushirikishwaji wa mikutano mikuu ya vijiji (sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 kifungu vha 12 na 13. Sheria ya matumizi bora ya ardhi namba 6 ya mwaka 2007 kifungu 3.4 na 22) ambazo zinatoa utaratibu wa kufanya mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kushirikisha mikutano mikuu ya vijiji,” inasomeka sehemu hya tamko hilo.

Madiwani hao wanadai kuwa halmashuri hyao ina kata 28 na vijiji 72 ikiwa ukubwa wa kilometa za mraba 14,030 ambapo aslimia 75 ya ardhi hiyo ni eneo la hifadhi huku 25 ikiwa ni kwa ajili ya  wananchi zaidi ya 274 ambao wanaitumia ardhi hiyo kwa ajili ya makazi, kilimo na malisho ya mifugo yao.

“Hivyo kupitisha mpango huu ni kuhalalisha mwisho wa kuishi kwa kuendelea kukosa makazi, kilimo na nyanda za malisho,” inasomeka sehemu ya tamko la madiwani hao 30.

Madiwani watoa kauli

Diwani wa kata ya Nainokanoka, Edward Maura amekataa mpango huo kwa sababu  eneo lililotengwa kwa ajili ya  Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake za uhifadhi na wanyamapori ni asilimia 85 huku  wananchi wakipewa asilimia 15 tu  ya ardhi.

Alisema kuwa waliyoachiwa wananchi  ni dogo ukilinganisha na idadi ya watu zaidi ya laki mbili , mifugo zaidi ya laki tatu, maeneo ya taasisi za serikali, mita 60 za mito yote iliyo kwenye eneo hilo na mita za akiba ya barabara  hivyo unakuta wananchi wanabaki na ardhi chini ya asilimia 10.

“Ajenda ya nne ya kikao ilikuwa kupitia, jadili na kupitisha rasimu ya mpango wa matumizi ya ardhi wa miaka 20 kuanzia 2023 mpaka 2043 ambapo baada ya kuisoma na kuielewa kwa pamoja madiwani wote wameikataa,” alisema Maura ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro na kuongeza:

“Hatujawahi kukaa kama baraza la madiwani kuwekea azimio au ‘vision’ kama kipaumbele na kusema tunahitaji mpango kazi utakaoenda kutusaidia kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi,”.

“Sisi kama baraza la madiwani ambao ndiyo chombo kikubwa cha uendeshaji halmashauri tumekuja kuona kuna jambo linaendelea baada ya kuitishwa kikao cha wadau,”.

“Ukiangalia tarafa ya Ngorongoro ina vijiji 25 kata 11 hakuna mwananchi au kiongozi aliyehusishwa kwenye mchakato huo na ukiangalia kwenye kitabu hicho eneo la tarafa ya Ngorongoro wanaenda  kuiondoa kwenye eneo la matumizi mseto ambapo kwenye kitabu inaoneka Hifadhi ya Ngorongoro yenyewe,”.

“Wameenda kuchukua maeneo ya Oldonyosambu Ngaresero ambayo yalikuwa hayajawahi kuguswa … kwa sasa wameyawekea alama ya kijani kuashiria na hayo wanaenda kuyachukua hivyo wananchi wa hawataweza kuyatumia.”

Msikilize hapa:

Naye Diwani wa viti maalum, Moi Sikorei amesema kuwa hawakuiridhia rasimu hiyo kwa kuwa haina maslahi kwa wananchi kwani Ngorongoro yote inaenda inaenda kuwa hifadhi na msitu.

Msikilize hapa:

Naye Diwani wa Viti Maalum, Sein Lekeni, alisema kuwa wangepitisha rasimu hiyo wangekuwa watu wa ajabu sana .

“Sisi kama madiwani wawakilishi wa wananchi tuliona huo mpango hauna maslahi na wananchi kwani imemega maeneo hasa eneo la tarafa ya Ngorongoro tuliona ni kijani tupu tulijadili tukaona eneo lote la Ngorongoro linaenda kuwa hifadhi na misitu hivyo sisi kama wawakilishi wa wananchi hatutakuwa tayari leo na hata kesho ikirudishwa hatuwezi kuendelea na hiyo rasimu.”

Msikilize hapa:

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohamed Bayo Marekani ambaye ndiye alikuwa akiongoza kikao hicho,  alisema kuwa walishindwa kujadili rasimu hiyo kwa kuwa ilikuwa imeandikwa kwa Kiingereza na ilikuwa na zaidi ya kurasa 300.

Bayo, ambaye ni diwani wa kata ya Olgosorock alikana kulitambua tamko la madiwani hao ingawa nay eye ni miongoni ,wa waliolisaini akiwa namba 25 huku akisisitiza kuwa walioleta rasimu hiyo wameshata taarifa hivyo wataangalia namna ya kutoa semina kwa madiwani ili rasimu hiyo ijadiliwe na kupitishwa.

“Mpango ule uliingia kwa mara ya kwanza kwenye baraza la madiwani ingawa mpango ule tumewahi kuujadili kwenye vikao vingine vya kijiji na wadau,” alisema Marekani na kuongeza:

“Changamoto ule mpango ule ulekuja kwa lugha ya kiingereza na unajua sisi mabaraza ya madiwani ni ya watu wa chini. Ingekuja kwa lugha eleweka madiwani na wananchi wanasoma wanelewa hiyo lugha ya kiingereza si kila mtu anajua hata kama anaelewa lakini rasmi katika kuendesha vikao vya halamshauri.”

“Na kwa kuwa ni kikao cha wazi inabidi itumike lugha ambayo wananchi wote wataelewa.Si kila mtu anajua Kiingereza na hata kama wanaijua lakini siyo lugha rasmi ya kuendesha vikao vya baraza la madiwani,”

“Lakini kwa kuwa ni baraza la wazi inabidi usome kitu ambacho wananchi wote wanaelewa hivyo madiwani waliuona wakashauri mpango huo uwe shirikishi wapate muda wa kuupitia na kushauri na maeneo ya kurekebishwa.”

Marekali alisema kuwa  mpango huo  unazungumzia kila kilichopo Ngorongoro binadamu, wanyama na kila kitu hivyo wakaona mpango huo umeandikwa kwenye kurasa 309 halafu unatakiwa waujadili kwenye kikao ambacho kina  agenda 11 jambo alilodai kuwa haingewezekana lazima utalipua.

“Ule mpango hatujakataa tumeusitisha ili madiwani wapate muda wa kuupitia kisha washauri hivyo madiwani walikataa ili madiwani na serikali wakae chini ili kuona ni njia gani ya kufanya ule mpango  tuwe na ushahidi,” alisema Marekani na kuongeza.

…Kitu kimesitishwa ni lazima kitarudi tena hivyo wale waandaaji wa ule mpango wakiona ni mpango umekataliwa ni lazima wajue ni kwa nini umekataliwa,”.

Mkurugenzi wa halmashauri Dkt Jumaa Mhina, hakuweza kupatikana kupitia nsimu zake ingawa juhudi za kumpata kuzungumzia suala hili zinaendelea.

Kumekuwa na mvutano wa muda mrefu baina ya wananchi wa wilaya ya Ngorongoro na serikali hasa baada ya kuja na mpango wa kuondo watu kwenye Tarafa ya Ngorngoro kwa madai kuwa wamekuwa wengi pamoja na mifugo hayo hivyo wanahatarisha uhifadhi wa NCAA.

Aidha kwenye tarafa ya Loliondo serikali imechukua ardhi kilometa za mraba 1,500 na kuzifanya pori tengefu la Pololeti hivyo kuwafanya wananchi waliokuwa wakilitumia kwa ajili ya malisho ya mifugo yao kushindwa kulitumia.

 

Like