“Kila mtu ana Membe wake”

Togolani Edriss Mavura, Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea aliyepata kuwa Katibu wa Waziri wa Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 2009 hadi 2014, ndiye mwandishi wa tanzia hii, ambayo SAUTI KUBWA imeitunza hapa ili kuhifadhi madini yaliyomo kwa ajili ya rejea za baadaye. ENDELEA. 

NIMEJARIBU kukusanya ujasiri wa kuandika japo kwa uchache namna nilivyomfahamu Hayati Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe, Mwanadiplomasia mahiri, Mwanasiasa kwa ajali, na Mwanaharakati kwa asili yake.

Wengi walimjua kwa sifa hizo nilizoziainisha. Rafiki zake wa karibu aliosoma na kukua nae walimjua kama ‘Berna’. Ndugu na wanafamilia wa karibu walimfahamu zaidi kama ‘Baba Cessy’.
Wengine walimuona mnyenyekevu na mpole, wengine walimuona mbabe na mtemi. Wako waliomuona mbishi na wale waliomuona mpenda demokrasia. Walikuwepo waliosema ni mtu mjivuni na anayejisikia, wakati wengine wakisema alikuwa ni mtu wa watu, rahimu na mcheshi kupindukia. Alimradi kila mmoja anaye Membe wake kwa namna alivyomjua na namna alivyogusa, au kupamia maisha yake.

Hata mimi ninaye Membe wangu.

Sina shaka wengi watamzungumia Bernard Membe kwa upande wa uongozi, diplomasia na siasa. Hivyo ndivyo alivyojulikana na wengi. Ninahisi kuwiwa na wajibu wa kujaziliza hadithi ya maisha yake kwa kuelezea uzoefu wangu mdogo wa kuishi na Bernard Membe kama Msaidizi wake. Nafanya hivyo sababu, mimi na wenzangu tuliowahi kumsaidia kazi, tumepata fursa ya pekee ya kumuona katika majira na mazingira tofauti.

Nimebahatika kati ya wengi kumfahamu kwa karibu sana nikiwa Katibu wake alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Nilikuwa Katibu wa Waziri kwa miaka 4 na miezi 3, ama kwa uchache siku 1,531. Aliniteua nikiwa Afisa mdogo mwenye miaka mitatu tu Wizarani. Alipenda ‘ukorofi wangu’ wa mawazo. Aliniamini sana, alinipenda sana na alinijenga sana.

Ukiwa Katibu wa Kiongozi unajikuta maisha ya kiongozi yanakuwa sehemu ya maisha yako. Furaha yake inakuwa furaha yako. Huzuni yake inakuwa huzuni yako. Jamii yake inakuwa jamii yako. Hali kadhalika mapito yake nayo yanakuwa sehemu ya mapito yako. Unajikuta unarithi ndugu na rafiki zake, na bahati mbaya unaweza hata kuchukiwa na mahasimu wake, na hata kugharimu ukuaji wako kikazi baadae.

Bernard Membe niliyemjua alikuwa na haiba ya kipekee sana. Muono wake wa dunia, mtazamo juu ya masuala mbalimbali, misimamo yake na hata maamuzi yake hayakufanana na wengi. Alikuwa ni mtu mwenye kuamini katika misingi ya haki, ukweli na utu. Aliamini sana katika miiko, yamini na viapo vyake, hata kama kwa kufanya hivyo, kungemlazimu kuwapoteza marafiki zake, kutengwa au kuchukiwa.

Si ajabu hata kidogo kwamba hali hii wakati mwingine ilipelekea kutoeleweka au kutafsiriwa vinginevyo na wenzake na jamii. Hilo nalo halikumsumbua hata kidogo. Alifurahia sana upekee wake kama alivyofurahia kutofautiana na wengine. Mara kwa mara alirejea nadharia maarufu ya Hegel na Karl Mark ya *_‘Unity of the Opposites’* inayozungumzia ‘migongano ya fikra kama fursa ya kuleta mabadiliko na maendeleo’. Aliamini kutofautiana ndio mwanzo ama wa kuelewana, au kutengeneza muafaka mpya. Kila ulipombishia au kumpinga, ndivyo ulivyoamsha ari yake ya kushawishi na kushawishiwa. Alipenda mjadala na alijua kujadili.

Kumuelewa Bernard Kamillius Membe unapaswa kuelewa kwanza mapito yake. Haiba yake ni matokeo ya muingiliano wa mambo mengi. Machache kati ya haya ni mafunzo na urithi wa jadi ya familia ya kiwindaji, utamaduni na jando la kimwera, mafunzo ya usemimari wa Kanisa Katoliki, ubobezi katika fani ya ujasusi, na taaluma ya utatuzi wa migogoro na uongozi wa Serikali aliyosomea katika Chuo Kikuu bora cha John Hopkins nchini Marekani. Kwa kiasi kikubwa sana, haya yaliathiri mtazamo wake na tafsiri yake ya maisha na dunia.

Kutokana na mapito, makuzi na malezi hayo, Bernard Membe alikuwa mtu mwenye hofu ya Mungu na mwenye imani kubwa. Bernard Membe alikuwa ni Mkatoliki mzuri. Alilithamini sana Kanisa Katoliki lililomlea. Alijenga Kanisa kubwa la Katoliki eneo analotoka la Rondo Chiponda ambalo lilimgharimu fedha na muda mwingi. Huu ndio ujenzi mkubwa ambao amewahi kuufanya katika maisha yake. Hata hivyo hilo halikumfanya kutothamini wenye imani ya dini nyingine. Alikuwa rafiki wa Waislamu sawia. Alijenga misikiti mitano yenye hadhi katika tarafa zote tano za jimbo lake la Mtama. Bila kusahau kufadhili wahujaji wa Kikristo na Kiislamu wasiopungua mia moja kwenda kwenye ibada za Hija huko Israeli na Mecca, Saudi Arabia. Aliamini sana katika nafasi ya imani ya Mungu katika maisha ya binadamu na katika ustawi wa jamii na malezi ya Taifa.

Membe alikuwa mtu jasiri sana kiasi cha kututisha Wasaidizi wake. Alijiamini sana na pengine kupita kiasi. Mara kadhaa tulilazimika kumsihi sana asichukue maamuzi au avute subira. Hakuogopa hoja, mjadala wala mtu yoyote. Hulka yake hii ilichangiwa sana na malezi ya Baba yake Mzee Kamillius aliyekuwa Mwindaji. Malezi yake ya kiseminari na mafunzo yake ya kijasusi nayo yalichachua ujasiri wake huo. Kadri ulivyomtisha, ndivyo ulivyompandisha ari ya kupambana. Anapokabiliwa na hatari ndipo ambapo machale na akili yake vilifanya kazi vizuri ajabu. Katika kuishi nae niliona akiogopa vitu viwili tu. Kwanza, Mungu wake. Pili, aliogopa sana fedheha na kujilaumu kwa kutotimiza wajibu (regrets/guilt consciousness).

Kwa sababu hiyo, uonevu kokote, na dhidi ya yo-yote, yeye ulimhusu. Membe alikuwa ni kaka, baba, babu, mjomba, binamu na rafiki wa kila aliyeonewa. Hakujiuliza mara mbili mbili ‘kununua’ vita vyako. Vivyo hivyo, watu walinunua na kununulishwa vita yake. Membe aligeuka na kuwa alama ya kila kijana aliyeonyesha ujasiri na msimamo. Wengi wa hao walioitwa ‘Team Membe’ hata hakuwahi kuwajua. Namkumbuka mmoja ambaye ni Mbunge sasa alikuja tukiwa Arusha na kumuambia, *“Mzee mimi hatujuani lakini mimi nashughulikiwa na kina fulani naambiwa ni mtu wako na ninatumwa na wewe. Basi walau nikujue tu”.* Ninayo mifano mingine kadhaa ya watu hawa ambao baadhi yao sasa ni Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.

Membe alikuwa rafiki mkubwa wa hoja, falsafa na mantiki. Hakuogopa kupingwa wala hakuogopa kubadilika kama alishawishiwa tofauti iwe na mkubwa au mdogo. Hapo ndipo tulipopatana zaidi. Pengine alinipendea ‘ubishani’. Alipendelea zaidi kupingwa kwa hoja kuliko kusifiwa. Siku moja, Waziri mmoja alikuja ghafla kumtembelea ofisini akaingia na kukuta mimi na Waziri Membe tunabishana (debate). Alishangaa sana. Hayo yalikuwa maisha yetu ya kawaida. Akiwa na jambo ananiita na kuniuliza wewe hili unalionaje. Tunajadili hadi tunafikia muafaka. Moja ambalo tulijadili sana kwa zaidi ya siku moja ni lile la ‘Uraia Pacha’.

Akili ya Membe ilifanya kazi mara dufu ukimpinga au kukiwa na ukinzani kuliko kukiwa na muafaka. Hakuweza jizuia kuhoji jambo ambalo halileti maana kwake hata kama lingekuwa limesemwa na nani. Katika jamii ambayo kuhoji huchukuliwa kama *‘shambulio la kutumia silaha’* hili lilimletea madhara makubwa na alibeba gharama hiyo kwa furaha na amani.

Kupenda kwake hoja kulimfanya awe na uvumilivu mdogo sana dhidi ya ujinga, haswa ujinga kutoka katika jamii ya wasomi. Angeliweza kuvumilia ujinga kutoka kwa mtu mwenye elimu ndogo sababu alipenda sana kuelimisha. Lakini kwa msomi, alipenda na kutegemea kujadiliana na kubishana (debate) zaidi. Hata hivyo, hakuwa na uwezo wa kuvumilia matusi au dharau sababu alithamini sana na kulinda utu wake kwa wivu mkubwa sana. Hakupenda kutukanwa sababu yeye mwenyewe hakuwa mtu mwenye matusi. Binafsi kwa muda niliofanya naye kazi, sikuwahi kumsikia akitukana hata mara moja, hata alipokasirika.

Membe aliamini sana katika demokrasia na aliwapenda sana Wapinzani. Wapinzani pia walimpenda. Mara nyingi alikutana nao nyumbani kwake na niliratibu mikutano yake hiyo. Wote walimfikia na wakajadiliana nae. Aliamini kwa dhati kuwa tunahitaji upinzani imara ili nchi yetu iwe imara, na CCM iwe imara. Hakuacha kuwasikiliza na hata kuwaunga mkono pale alipoona wanayo hoja nzuri. Jambo ambalo lilimletea tabu ndani ya Serikali na Chama chake. Aliwaona Wapinzani kama ni watani tu maana kwenye desturi za kabila la Wamwera, utani ulikuwa ni jambo la kawaida.

Membe aliamini sana katika vijana na alijihisi anao wajibu wa kuwalea kiuongozi ili walitumikie Taifa mbeleni. Yeye mwenyewe alisimulia jinsi alivyoaminiwa katika majukumu makubwa katika umri mdogo. Akaamini anao wajibu kwa kuwafanyia hivyo vijana. Amesaidia vijana wengi na kuwalea kiuongozi na aliwapigania sana ndani ya Serikali na Chama. Binafsi, aliniita kuwa Katibu wa Waziri nikiwa na miaka 29 tu. Aliamini sana pia katika kuwapa nafasi ya pili vijana pale walipokosea, na kuwakinga dhidi ya hujuma na vita yoyote ya kuwanyong’onyesha.

Alipotofautiana na uongozi wa awamu iliyopita, na kulazimika kuhama Chama baadae, nilimuuliza sababu zake, alinijibu kuwa, *“Chama changu kimenifukuza. Sijakiacha, kimeniacha. Kwangu kubwa ni kupigania kesho bora ya Watoto wa Taifa hili. Hilo brother siachi. Nimetafuta jukwaa lingine”.* Akaendelea kuniambia *“Natimiza kiapo changu na wajibu wangu kwa Taifa hata kama nitabaki peke yangu, maana kiapo changu kwa Taifa nilikula peke yangu”.*

Membe alikuwa na moyo mpana na mkono mrefu aliyetoa na kujitoa sana kwa wahitaji na jamii. Alitoa alichonacho na hata alichotarajia kukipata kesho. Hii ilifanya wenye shida kumiminika kwake. Haikujalisha ikiwa alimjua mtu. Alimradi aliguswa na shida ya mtu hiyo ilikuwa sababu ya kutosha ya kumsaidia. Yatima kwa wajane, wenye ulemavu na wenye umasikini. Kilichotustaajabisha tuliokuwa naye, hatukuuona utajiri wake wa pesa wala mali nyingi. Alikuwa na maisha ya kawaida tu. Tulimuona alivyojisikia vibaya na kuumia pale aliposhindwa kumsaidia mtu. Wema wake huu ulimponza pia pale alipotoa ahadi akiwa na nia njema ya kutafuta njia ya kusaidia na akashindwa kuitimiza. Mara nyingine, alitoa zake zikaisha hata akatuazima Wasaidizi wake na kuturejeshea baadae, alimradi tu atatue shida ya mtu.

Kupanga miadi na Membe ilikuwa ni ngumu sana. Uwezekano ulikuwa ni mkubwa kuwa utasubirishwa na utalazimika kusubirisha wengine. Binafsi, nililazimika kumvizia usiku sana ikiwa nina jambo ambalo lilihitaji utulivu na mjadala mrefu na yeye. Hata katika kumvizia huko, ni mara chache nilifanikiwa, maana bado nilikuta watu. Alikuwa na muda na kila mtu wa kila hali.

Maisha ya Membe yalikuwa ni maisha ya kiasi. Alijipendea maisha ya kawaida na alipenda zaidi kuishi kijijini kwake Rondo Chiponda na akihama hapo basi Mbambabay, Nyasa kwa wakwe zake. Katika makazi yake yote, ni kijijini kwake ndipo alipojenga makazi makubwa. Alikaa jijini Dar es Salaam ikiwa tu kulikuwa na jambo la kumuweka mjini. Unaweza kusema Membe alikuwa raia wa kimataifa (global citizen) na mwanakijiji wa Rondo Chiponda. Membe hakuwa raia wa mjini (Cosmopolitan). Dar es Salaam kwake ilikuwa ni sehemu ya kukutana na watu tu.

Mwenyezi Mungu alimjalia Membe ‘nyama ya ulimi’. Alikuwa na kauli tamu na sauti yenye ushawishi. Alikuwa mtu mcheshi sana mwenye kupenda utani na msimulizi nzuri. Aliweza kukusimulia jambo unalolijua na ukaliona jipya na ukacheka upya. Alipenda sana kuwinda na hadithi za uwindaji. Hadithi kuhusu uwindaji ungeweza kuanzisha nae wakati wowote katika hali yoyote. Katika muda wa faragha alipenda sana kusoma vitabu na kufanya chemsha bongo (Sudoku). Michezo pekee aliyoifurahia ilikuwa ni ndondi na kuwinda.

Alijipenda sana na kujali afya yake. Alikuwa makini katika chakula alichokula na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara. Alipenda sana kufanya mazoezi. Aliishi maisha ya kadiri. Alikuwa ni mtu wa kutosheka na kukinai. Utajiri wake mkubwa ulikuwa ni roho yake, akili yake, maarifa yake na imani yake.

Membe alikuwa mwanafamilia. Aliipenda sana familia yake japokuwa majukumu yake na wajibu wake kwa Taifa vilidhulumu sana muda na familia yake. Alijitahidi kila alipopata nafasi kuwapo nyumbani. Mara nyingi kama hayuko safarini ungemkuta nyumbani kwenye ‘mdule’ wake. Alihusiana vizuri na mke wake na watoto wake siku zote. Alikuwa huru sana na watoto wake nao walikuwa huru sana nae.

Ninamshukuru Hayati Bernard Membe kwa malezi yake mazuri kwangu. Amenijenga sana na ana mchango mkubwa katika maisha yangu. Niliteuliwa kuwa Mwandishi wa Hotuba wa Rais nikiwa Katibu wake. Nakumbuka siku ile akiniambia alifurahia sana kuaminiwa kwangu ingawa alisikitika naachana nae. Niliachana nae Dodoma tukiwa katika Kikao cha Bunge nikaenda kuripoti katika kazi yangu mpya.

Sikuwapo alipofariki na sitakuwepo anapoagwa na kupumzishwa. Hili linalipa maumivu makubwa sana yasiyopimika. Nasikitika sana sitaweza kuwahi kumpumzisha Mzee wangu na kumfariji Mama Ceccy, na wadogo zetu.

Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapa ujasiri wa kukabiliana na mtihani huu mkubwa. Nawakumbusha kuwa baba yao amewaachia utajiri mkubwa sana wa heshima, marafiki na kumbukumbu njema.
Nafahamu alikuwa anaandika kitabu chake. Hajakimaliza. Tutakimalizia kwa kuyaishi mafunzo mema na malezi mazuri aliyotupatia ili kupitia yeye, nasi tukaguse maisha ya wengine kwa namna tulivyoguswa na yeye.
Nikuhakikishie Bernard Kamillius Membe kuwa umeacha sadaka nyingi zitakazoishi baada ya maisha yako. Nenda Membe!

*_Mwandishi wa Tanzia hii ni Togolani Edriss Mavura, Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea aliyepata kuwa Katibu wa Waziri wa Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 2009 hadi 2014

Like