Kwanini mabalozi wa nje wametoa tamko kwa Kenya?

TAKRIBANI miezi mitano kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya, umoja wa mabalozi wal nchi mbalimbali walioko Kenya wameitaka serikali ya Kenya kuridia na kutekeleza Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala bora kama ulivyopitishwa Januari 30, 2007 na kuanza kutekelezwa rasmi mwaka 2012. 

Mabalozi hao ambao wametoa tamko la pamoja wanawakilisha nchi za Marekani, Denmark, Uingireza, Uholanzi, Australia, Norway, Sweden, Switzerland, na Canada.

Wote wamesisitiza uwazi katika mazingira ya uchaguzi huo na kuzingatia uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC). 

Licha ya Kenya kusaini mkataba huu wa Umoja wa nchi za Africa (AU) Juni 28 mwaka 2008, bado Kenya haijaridhia kuutekeleza hadi sasa licha ya kuwa kumefanyika uchaguzi mara tatu tangu mwaka 2007.

Kenya, kama ilivyo kwa nchi nyingine, inapata kigugumiziona katika kusaini kwa mkataba huu ambao umetoa uhuru mkubwa katika eneo la demokrasia, uhuru wa mawazo na mazingira ya usawa wakati wa uchaguzi.

Tamko hili lina maana gani kuelekea uchaguzi Mkuu wa Kenya?

Tamko la umoja wa mabalozi hawa linakuja huku kukiwa na msuguano unaoendelea kuelekea uchaguzi huo wa Kenya, huku Rais Uhuru Kenyatta akimuunga mkono mpinzani wake wa siku nyingi Raila Odinga, katika kile kinachoonekana kuwa ni maelewano yasiyoridhisha kati yake na makamu wake, William Ruto

Tamko hili si la kwanza kwa Kenya kwani mwaka  2017 kulitolewa tamko kama hili na mabalozi pamoja na makamishina wa juu.

Wadadisi wa siasa za Kenya wanasema tamko la mwaka huu huenda limechochewa na msuguano mkali wa kisiasa huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa kati ya wafuasi wa Rais Kenyattta na makamu wake William Ruto, jambo linaloweza kuathiri mazingira ya uchaguzi huu.

Kuelekea uchaguzi huu, tamko hili limesisitiza juu ya  uwazi, uwajibikaji, utawala wa sheria na kujali masuala ya haki za binadamu kama ilivyotamkwa katika mkataba huo.

Kwa mazingira ya sasa ya Kenya, uchaguzi huu unaangaliwa sana na Wakenya kwani kuna wanaotamani mabadiliko waliyosubiri kwa muda mrefu, wakitaka Raila Odinga apate fursa ya kuongoza nchi hiyo, huku wengine wakitaka Ruto apite.

Wengine wanasema Ruto, ambaye anajiita ‘hustler,’ yaani mchakarikaji, anaungwa mkono na wananchi wenye hali duni nchini Kenya, huku Raila odinga akiungwa mkono na kundi la wenye nacho jambo ambalo halina afya kwa siasa na umoja wa Wakenya

Licha ya maridhiano ya hivi karibuni kati ya Rais Kenyatta, baadhi ya viongozi wa serikali na wapinzani yajulikanayo kama Building Bridges Initiatives BBI, wakosoaji wa Rais Kenyatta wanaona hatua hiyo si nia dhati ya kuunganisha Wakenya, bali ni namna ya rais huyo kuhadaa Wakenya ili kumtengenezea mazingira mazuri Raila Odinga ambaye amegeuka swahiba wa karibu wa Rais Kenyatta.

Ruto anakosoa  mpango wa BBI licha ya ukweli kuwa alishiriki katika hatua za mwisho za BBI kwa kushikana mikono na wenzake.

Baadhi wa wanasiasa wenye ushawishi nchini Kenya walishiriki siku ya maombi waliyoiita “Nationa Day Prayer.” Baadhi yao ni Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Mosses Wetangula. Wengi walitafsiri hatua hii kama maridhiano ya kitaifa ingawa tofauti zimeendelea kuwepo.

Licha ya vuguvugu ndani ya serikali ya Rais Kenyatta, ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga mpango wa BBI pia ulipingwa vikali.

Mwanasiasa na mwanaharakati maarufu wa chama hicho ambaye pia ni Gavana wa Siaya, Seneta James Orengo, alisema hakubaliani na mpango huo wa BBI, na akasema ataendelea na msimamo wake ambao ni kinyume cha msimamo wa chama chake cha ODM. Hali hii inaonesha msuguano mkali na tofauti za mawazo kulekea uchaguzi wa Kenya

Ndani ya mpango wa BBI kulikuwa na marekebisho ya sheria ya uchaguzi wa Kenya ambayo baadhi ya watu wanasema huenda ni mpango wa kunufaisha walio wachache tofauti na wanasiasa wanavyoimba majukwaani. 

Wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichotokea mwaka 2007 baada ya uchaguzi mkuu ambapo vurugu zilisababisha vifo vya takriban watu 1000, Wakenya wengi wasingependa kuingia katika machafuko kama hayo.

Mazingira ya sasa ya Kenya yanahitaji siasa safi ambazo zitawaunganisha pamoja kama taifa.

Kwanini nchi za Afrika zinasita kutekeleza mkataba wa ACDEG?

Ikiwa ni takribani miaka 15 tangu kuanzishwa kwa mkataba huu mwaka 2007, bado kuna kile kinachoonekana kusuasua kwa baadhi ya nchi katika kuuridia na kuutekeleza makataba huu wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala. Hadi sasa hali iko hivi

  • Waliosaini: Nchi 46 kati ya 55
  • Waliothibitisha/ kuridhia:  Nchi 34 kati ya 55
  • Waliotekeleza, kuufuata au kufanyia marekebisho madogo: Nchi  34 kati ya 55

Nchi nyingi za Afrika zinasuasua kuuridhia na kuutekeleza mkataba huu kutokana na yaliyomo ndani ya mkataba. Mkataba huu wenye jumla ya ibara 63, unaoagiza kufuata kwa mazingira huru na yenye usawa kisiasa.

Kwa baadhi ya serikali za Afrika, imekuwa vigumu kukubali mazingira ya namna hii kwani bado vyama vya upinzani havijapewa nafasi sawa na walioko madarakani.

Kama mambo yote yaliyopo katika mkataba huu yangetekelezwa na serikali za Afrika katika kuboresha mazingira ya demkorasia na utawala wao, ni wazi kuwa malalamiko ama vurugu zisingeweza kutokea katika chaguzi mbalimbali zinazofanyika.

Kuna maswali mengi kwa baadhi ya viongozi wa Afrika kuhusu hili. Je, si aibu kukumbushwa kuridhia na kutekeleza mkataba ambao tuliuandaa wenyewe mjini Addis Ababa tukishirikiana na wenzetu?

 Jambo hili linatoa picha isiyoridhisha hasa kwa demokrasia ya nchi nyingi za Afrika na si Kenya pekee, ingawa mabalozi wameelekeza tamko hili kwa Kenya.

Ni wakati sasa wa viongozi wa Afrika waamke na kutekeleza mkataba huu, kwa maenedeleo ya demokrasia ya bara letu na mataifa yetu. Kutekeleza mkataba huu ni jambo letu, si suala la kukumbushwa.

Like