Mzozo wa Ukraine, Urusi kuathiri michezo 

KATIKA dunia ambayo ushirikiano katika sekta zote hauwezi kuepukika, uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ambao sasa ni vita baina ya mataifa haya mawili, umeanza kuleta mabadiliko makubwa  katika sekta ya michezo, hasa kwa kampuni za Urusi na wamiliki wa vilabu wenye asili ya Urusi.

Katika hali isiyotarajiwa, kuna matokeo hasi  kwa michezo huku baadhi ya wadau wakiendelea kutoa uamuzi mgumu siku hadi siku. Baadhi ya athari za moja kwa moja tangu kuanza kwa vita hii ambayo haijatimiza hata wiki moja, ni hizi zifuatatazo:

Moja, tayari Roman Abramovich, mmiliki wa klabu ya Chelsea na tajiri wa Urusi ambaye ni rafiki mkubwa wa Rais Vladmir Putin,  amejiondoa katika umiliki wa timu hiyo kwa muda. Uamuzi juu ya klabu sasa utakuwa mikononi mwa viongozi wa taasisi inayojulikana kama Chelsea Foundation.

Chelsea, ambayo kwa sasa inashikilia makombe ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya (UEFA) na Klabu Bingwa ya FIFA (2021), imepata mafanikio makubwa  tangu iliponunuliwa na Roman Abramovic mwaka 2003.

Timu hii ya jiji la London huenda ikayumba kutokana na tajiri wake kujiweka pembeni kwa muda, sababu ikiwa ni kuwekewa vikwazo na Uingereza kutokana na ukaribu wake kwa Rais Putin.

Ikumbukwe Roman Abramovich aliwahi kukiri kumsaidia Putin katika kampeni zake, jambo lililowakasirisha mahasimu wa Putin kipindi cha nyuma. Tangu Abramovoch anunue Chelsea timu hii imepata mafanikio makubwa, huku ikibeba zaidi ya makombe 20. Je, nini hatima ya Chelsea? Mwenendo wa vita hii utaleta jibu.

Pili, tayari Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA), limetoa uamuzi ya kuondoa fainali za klabu bingwa Ulaya kuchezwa katika mji wa St. Petersburg nchini Urusi. Badala yake, michuano hiyo sasa itafanyika katika uwanja wa Parc de Prince mjini Paris nchini Ufaransa.

Uamuzi huu wa UEFA umetokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine huku suala la usalama likiwa kipaumbele.

Ni uamuzi utakaoathiri pia wadhamini wa soka, na waandaaji na kila shughuli kuelekea mechi ya fainali hii iliyopangwa kufanyika Mei 28 mwaka huu.

Uamuzi wa UEFA unaweza pia kutafsiriwa kama sehemu ya vikwazo dhidi ya Urusi. Ina athari kwa wapenda soka, maendeleo ya soka, na uwekezaji ambao unafanyika katika soka.

Kutokana na vita kati ya Ukraine na Urusi, uamuzi wowote utakayofanyika dhidi ya Urusi unaweza kuleta matokeo hasi katika sekta nyingi, ikiwemo michezo na burudani.

Tatu, Poland imetoa uamuzi wa kutoshiriki mechi yao dhidi ya Urusi kwa ajili ya kufuzu Kombe la Dunia. Msimamo huu wa Poland unakuja siku chache baada ya majeshi ya Urusi kuvamia Ukraine.

Sababu iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini Poland (PZPN), ni za kiusalama lakini wachambuzi wanaona hatua hii pia inaonesha msimamo wa Poland kama mwanachama wa NATO kutokubaliana na Urusi kwa kile kinachoendelea Ukraine.

Kama Poland haitabadili msimamo, itabidi ama Urusi ikubali mchezo wao kuchezewa katika nchi nyingine au wajitoe katika mbio zao za kuelekea Qatar mwezi wa 11 mwaka huu katika michezo ya Kombe la Kunia.

Nhi nyingine zinazotakiwa kuchuana na Urusi ni Jamhuri ya Czech na Sweden. Muda mfupi uliopita nazo zimechukua hatua kama ya Poland. Urusi hapa inatakiwa ichague kati ya kusuka au kunyoa, huku tukisubiri uamuzi ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) dhidi ya Urusi.

Nne, udhamini wa kampuni za Urusi katika ligi mbalimbali barani Ulaya umekataliwa, huku baadhi ya timu zikiondoa mabango ya kampuni hayo.  Kampuni zitakazoathirika zaidi ni Gazprom na Aeroflot ambazo zinadhamini ligi nyingi barani Ulaya. Hizi zote ni hatua za nchi na mbalimbali kulaani hatua ya Urusi dhidi ya Ukraine. 

Kitendo hiki cha nembo na mabango ya kampuni haya kuondolewa kina madhara makubwa kimatangazo lakini pia kitaathiri faida za kampuni ya Urusi katika michezo.

Klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani ni miongoni mwa timu za mwanzo kuchukua uamuzi wa kuondoa nembo ya Gazprom katika jezi zao, huku Manchester United wakiachana na Aeroflot.  Mifano ya ligi ambazo tayari zimeondoa mabango ya kampuni za Urusi ni Uingereza, Ujerumani na Ufaransa.

Hatua hii ya kimichezo ina athari za kiuchumi kwa maendelo ya soka katika mataifa mbalimbali pamoja na kuathiri uchumi wa kampuni za Urusi katika michezo, si tu barani Ulaya bali hata katika mataifa mengine nje ya Ulaya.

Tano, Ligi Kuu ya Ukraine ambayo ilikuwa imesimama ili kuanza msimu mpya, ilitarajiwa kuanza rasmi leo lakini tayari Shirikisho la Soka nchini Ukraine limetoa siku 30 ili kuangalia kama ligi hiyo inaweza kuchezwa licha ya mapigano yanoyoendelea.

Ni wazi kuwa kama vita hii itaendelea, ligi ya Ukraine haitachezwa, huku ushiriki wa timu za Ukraine katika mashindano ya kimataifa ukiwa shakani.

Sita, zaidi ya wachezaji 25 raia wa Brazil wanaocheza soka la kulipwa katika klabu za Shakhtar Donetsk na Dynamo Kyiv zote za Ukraine, wamekwamia nchini humo huku wakitaka kuondoka.

Haya ni madhara ya mzozo wa Ukraine na Urusi. Na huenda wachezaji hawa wasiendelee kuchezea timu hizi kama hali ya kisiasa nchini Ukraine haitarudi katika hali yake ya kawaida katika wiki chache zijazo.

Madhara ya uamuzi wa Urusi bado yanaendelea kutokea katika michezo. Wachambuzi wanaamini kama vita haitasitishwa, basi uvamizi huu unaweza kuathiri uhusiano ya kimichezo hasa barani Ulaya.

Katika mbio za magari

Waandaaji wa mbio za magari maarufu duniani, za Formula One (F1), wamefuta mbio zake za Russian Grand Prix ziliyopangwa kufanyika katika mji wa Sochi Autodrom nchini Urusi Septemba 25 mwaka huu. Hatua hii pia inaweza kumwathiri dereva wa Urusi Nikita Mazepin. Tayari waandaji wa Formula 1 wamesema uamuzi juu ya dereva huyo utatolewa.

Katika hatua nyingine kuna sintofahamu juu ya timu ya Haas F1 (timu ya madereva) ambayo miongoni mwa wadhamini wake ni tajiri aliye karibu na Rais Putin. Huenda timu hiyo ikaondolewa katika mashindano ya magari mwaka huu.

Katika Olympic

Kumezuka maswali kuhusu uhusino kati ya Mashindano ya Olympic na uvamizi wa Urusi katika mataifa mbalimbali ya Ulaya. Historia inaonesha kwa miaka 14 sasa Urusi hufanya uvamizi wake katika mwaka ambao kunachezwa michezo ya Olympic. Je, ni kwa bahati mbaya haya hutokea au kuna uhuasiano?

Uhusiano wa uvamizi wa Urusi na mashindano ya Olympic

  • Mwaka 2008: Urusi ilivamia Georgia wakati mashindano ya Olypmpic yakifanyika mjini Beijing.
  • Mwaka 2014: Urusi ilivamia Crimea  wakati mashindano ya Olypmpic yakifanyika Sochi nchini Urusi
  • Mwaka 2022: Na mwaka huu Urusi imevamia Ukraine wakati wa kufunga mashindano ya Olympic mjini Beijing nchini China yaliyomalizika Februari 20 siku chache kabla ya uvamizi.

Wanamichezo walaani Uvamizi wa Urusi

Katika michezo iliyochezwa mwishoni mwa wiki hii tayari, baadhi ya timu pamoja na wachezaji wamelaani kile kinachoendelea katika ardhi ya Ukraine

Katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza kati ya Everton na Manchester City jana timu hizo zilivaa jezi zilizoandikwa ‘NO WAR’ wakimaanisha HATUHITAJI VITA. Maneno haya ni kiashiria cha kutaka kusitishwa kwa vita hivyo.

Timu hizo zilikutana kukiwa na wachezaji wawili raia wa Ukraine, Alexsandr Zincheko na Vitalii Mykolenko ambao walionesha hisia kali hata wakatokwa na machozi baada ya kukumbantiana kabla ya mchezo huo.

Katika ligi ya Hispania, timu kubwa ya Barcelona nayo ililaani vita hiyo. Kwa ujumla, wanamichezo katika maeneo mbalimbali duniani wamelaani vita hii wengi wakitaka mapigano yasitishwe.

Picha halisi ya michezo itaathirika vipi na mzozo huu, inategemea uamuzi wa Urusi kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Ukraine.

Baadhi ya watu wanatabiri anguko katika sekta ya michezo nchini Urusi kutokana na vikwazo inavyowekewa na nchi mbalimbali duniani vikiwemo na vyama vya kimataifa vya kusimamia michezo. Wakati haya yakiendelea, kiu ya wapenda michezo kote duniani ni kusitishwa kwa vita kati ya Urusi na Ukraine.

Katika mwendelezo wa hatua kali dhidi ya Urusi, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Umoja wa Mashirikisho ya Soka ya Ulaya (UEFA) yamefungia klabu za nchi hiyo kushiriki michuano ya kimataifa hadi hapo baadaye. Habari kamili hii hapa.

Like