Kesi ya Mbowe: Jamhuri yawafutia kesi washitakiwa

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia, BJ, leo tarehe 4 Machi 2022.

SIKU chache baada ya Mahakama kutoa uamuzi kuwa Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu, Jamhuri imefuta mashitaka dhidi yao kwa maelezo kuwa Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Uamuzi huo umewasilishwa mahakamani na mawakili wa mashitaki mbele ya Jaji Joachim Tiganga leo asubuhi katika siku iliyotarajiwa kuwa ya washitakiwa kuanza kujitetea.

Kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamuhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe inatajwa mahakamani.

Watu wako makini kusikiliza.

Wakili wa Serikali: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, ikikupendeza naitwa Robert Kidando, Wakili wa Serikali Mwandamizi na nipo pamoja na:Pius Hilla

Abdallah Chavula

Jenitreza Kitali

Nassoro Katuga

Esther Martin

Ignasi Mwinuka

Tulimanywa Majige

Peter Kibatala: Mheshimiwa Jaji, iIkupendeza naitwa Peter Kibatala na nipo na

Paul Kisabo

Sisty Aloyce

Gaston Garubindi

Iddi Msawanga

Evaresta Kisanga

Maria Mushi

Nashon Nkungu

John Malya

Jeremiah Mtobesya

Fredrick Kihwelo

Dickson Matata

Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji

Jaji: Shauri lilikuwa linakuja kwa utetezi. Je, mna habari zozote za wateja wenu?
(Mahakama iko kimya).

Kibatala: Mheshimiwa Jaji ni kweli kwamba shauri lilikuwa limepangwa kwa ajili ya utetezi. Kwa upande wangu tulifanya maandalizi mazuri sana. Mimi, John Mallya, Dickson Matata, Fredrick Kihwelo na wengine juzi na jana tulikuwa Ukonga na Segerea. Tulikutana nao wakiwa na bashasha kabisa, kwamba leo tunaendelea na utetezi. Lakini leo ssubuhi tumepata taarifa kutoka kwa askari Magereza kwamba Mbowe amepata matatizo ya kiafya. Kwa hiyo hatuwezi kuendelea. Tunaweza kupanga kuendelea Jumatatu.

Kibatala: Tunaweza kupanga Jumatatu kwa ajili ya washitakiwa kuendelea kujitetea. Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

Jaji: Jumatatu itakuwa tarehe ngapi?

Kibatala: Tarehe 7 Machi 2022.

Wakili wa Serikali: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, shauri limekuja kwa ajili ya utetezi, na tumewasikia wenzetu maombi waliyowasilisha. Sasa tusingependa kujibu hoja hiyo kwa sababu na sisi tuna maombi mengine. Kwa hiyo kujibu hoja hiyo haitakuwa na maana sana.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji tunaomba moja la kufanya mbele ya Mahakama yako. Na ombi hili Mheshimiwa Jaji ni kwamba Mkurugenzi Wa Mashitaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri anaomba kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia na kuendelea na shauri hili.

Wakili wa Serikali: Na taarifa hiyo tunaitoa chini ya Kifungu cha 91(1) kwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji taarifa hii tunaiwasilisha kwa njia ya maandishi. Kwa maombi hayo ya kifungu cha 91(1) tunaomba kuondoa mashitaka yote dhidi ya washitakiwa wote.
Wakili wa Serikali: Sababu zote zipo katika Noel Prosecui ambayo tumeiwasilisha.

Wakili wa Serikali anapeleka nyaraka mbele ya Karani wa Jaji, na karani anampatia Jaji.

Wakili Jeremiah Mtobesya: Mheshimiwa Jaji tumesikia taarifa ya notes hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, na kwa bahati mbaya hatuwezi kusema lolote zaidi ya kusema tunaichia Mahakama kwa sababu kifungu kinatoa maelezo yote kwamba baada ya kusema hivyo tunaichia Mahakama dhidi ya amri zake za mwisho.

Jaji: Je umezungumza kwa niaba ya defense wote?

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji naomba kila mmoja aseme.

John Malya: Mheshimiwa Jaji, notes iliyotolewa inastushgika mikono wote, pamoja na kujiandaa kwa ajili ya kujitetea, mikono yetu imefungwa na hatuwezi kusema lolote. Tulitaka sana warudishe gharama zetu na mengine lakini wacha tusubiri maamuzi ya Mahakama.

Kihwelo: Kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu tumesikia taarifa iliyotolewa. Tunaichia Mahakama iweze kutoa amri.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji na sisi tunaichia Mahakama. Sheria inajielezea wazi.
(Mahakama imetulia kimya wakati Jaji anaandika)
(Bado mahakama iko kimyaaaaaa!).

Jaji: Baada ya Mahakama kusikiliza hoja iliyoletwa na wakili mwandamizi wa Serikali kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka hana nia ya kuendelea na kesi hii, na upande wa pili wakaridhia, Mahakama inasema shauri hili lililokuwa linawakabili washitakiwa Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe linaondoshwa mahakamani na washitakiwa wanaachiwa huru bila masharti. Kwa sababu kuna vielelezo vililetwa Mahakamani, naandaa AMRI ya kuviachia, na hivyo naelekeza Mkuu wa Magereza kuwaachiwa mara moja leo na si vinginevyo. NATOA AMRI.
Jaji anaondoka mahakamani.

Habari zaidi zitafuata baadaye.

Like