Mlipuko mpya wa Corona walazimisha Tanzania kutangaza tena takwimu baada ya kimya cha miezi 14

Waziri wa Afya Dorothy Gwajima

SASA ni dhahiri kwamba maambukizi ya virusi vya Corona nchini Tanzania ni makubwa kuliko inavyoweza kufichwa, kwani kumebainika kuwepo ongezeko la vifo, hasa maeneo ya mijini kutokana na chazo kinachotajwa kuwa ni COVID-19; wimbi la tatu.

Idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa hospitalini za rufaa baada ya kuambukizwa COVID-19 ni kubwa huku vitanda vya kuwalaza katika hospitali nyingi vikikosekana. Mitungi ya gesi ya oksijeni nayo haitoshi.

Uchunguzi wa siku 10 wa SAUTI KUBWA katika Hospitali ya Taifa Muhimbili; hospitali za rufaa za Dar es Salaam; Temeke, Mwananyamala na Ilala; Bugando – Mwanza na KCMC – Moshi, umebaini  kuwepo kwa wingi wa wagonjwa, huku maeneo hayohayo, familia nyingi zikizika ndugu zao kutokana na vifo vinavyochochewa na maambukizi ya janga hilo.

Mapema leo kwa mara ya kwanza, baada ya zaidi ya mwaka mmoja tangu kusimamishwa kwa takwimu za maambukizi na vifo vya janga hilo, Tanzania imetangaza takwimu za ugonjwa huo, huku ikielezwa kwamba maeneo ya nijini ndiyo yanayoathirika zaidi kwa kuwa na maambukizi mapya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima akiwa jijini Dodoma, amesema Tanzania hadi Juni 8, mwaka huu ilikuwa na wagonjwa 408 katika hospitali zake kubwa.

Dk. Gwajima amesema katika Hospitali ya Benjamn Mkapa, Dodoma, kuna wagonjwa 26 waliolazwa kwa kukutwa na maambukizi ya COVID-19 na kati ya haom 22 wanapumua kwa kusaidiwa na mitungi ya oksijeni.

Kutokana na wingi wa wagonjwa wa COVID-19, Hopitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, iliishiwa mitungi ya oksijeni kwa wagonjwa. Uongozi wa hospitai hiyo ulieleza kuwa na upungufu wa mitungi 500 ili kuhimili idadi kubwa ya wagonjwa wa Corona. Baada ya tangazo hilo la kumba msaada, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilipeleka mitungo 300.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekiri kuwepo kwa maambukizi ya wimbi la tatu la janga hilo (Delta Variant – 3th wave), na ameonya wananchi kuacha kupuuza kuepo kwa ugonjwa huo. Amehimiza  wananchi kuchukua tahadhari kubwa ya kujikinga na ugonjwa huo.

Rais Samia baada ya kuingia madarakani – akichukua uongozi wa nchi kufuaia kifo cha John Magufuli, rais aliyekaidi kujilinda na hata kuwakinga wananchi wake dhidi ya janga hilo, amekuwa akihimiza kila mtu kuchukua hadhari kwa kuzingatia makatazo ya Shirika la Afya Duniani (WHO); ikiwamo kunawa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko. Hata hivyo, ado kua idadi kubwa ya Watanzania hawazingatii makatazo haya.

Tofauti na Magufuli,Rais Samia amekiri kwamba COVID-19 ipo Tanzania na kwamba nchi hiyo iko tayari kupokea chanjo kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuhudumia wananchi watakaopenda kuchanjwa. Tanzania imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuagiza chanjo, huku serikali ikiingia mikataba ya kupokea chanjo zenye kusimamiwa na WHO kwa nchi masikini kupitia utaratibu maalum wa COVAX..

Kutokana na hali kuwa mbaya na kuwepo kwa tishio kubwa zaidi la maambukizi na vifo, Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo ameshauri serikali kupiga marufuku mikusanyiko yote mikubwa ili kuokoa wananchi na nchi na madhara ya COVID-19, ikiwamo vifo.

“Tunapoteza Maisha ya watu wengi mno, ni vyema mikusanyiko mikubwa ikasimamishwa mara moja, hali siyo nzuri,” amesema Shigongo na kuhoji – “huku misiba mingi, huku matamasha , hivi tuko makini kweli?”

Like