‘Askofu’ Gwajima matatani CCM

WAKATI wowote kuanzia kesho, kiongozi na mmiliki wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, ataamriwa kuthibitisha msimamo wake kwamba chanjo dhidi ya COVID-19 ni sumu na zinaua; akishindwa “ataadhibiwa vikali,” SAUTI KUBWA imeelezwa.

Taarifa zilizofikia SAUTI KUBWA leo kutoka Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, iliyoko Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, zinaeleza kuwa vikao vya juu vitamhoji ili aeleze kwanini anaendelea kupingana na msimamo wa kitaalamu unaoungwa mkono na serikali kuhusu chanjo hiyo.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa ‘Askofu’ Gwajima amekuwa akipingana na Rais Samia Suluhu Hassan, serikali na chama chake kwa madai kwamba chanjo dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona ni hatari na kwamba waliochanjwa “watakufa kati ya miaka miwili hadi 10 kutoka siku walipochanjwa.”

Amekuwa akitoa msimamo huo madhabahuni, ndani ya kanisa lake na kurekodiwa na kusambazwa kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, huku akitamba kwamba kwa msimamo wake, hakuna wa kumgusa wala haogopi kupoteza ubunge wake. Gwajima ni mbunge wa Jimbo la Kawe, Dar es Salaam.

SAUTI KUBWA inafahamu kuwa Gwajima ni mmoja wa watu waliokuwa washauri wa karibu wa Rais John Magufuli ambaye alisema Tanzania hakuna Corona huku ikiua watu, wakiwemo baadhi ya wabunge, mawaziri na wasaidizi wake wa karibu; hatimaye ikamchukua na yeye mwenyewe – ingawa taarifa rasmi zilisema akikufa kwa ugonjwa wa moyo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamidu Shaka, amesema kuwa chama chake tayari kimetafakari kuhusu kile alichoita “upotoshaji wa Gwajima na kupingana na serikali ya CCM,” sasa chama kinachukua hatua. Hakueleza hatua zinazoweza kuchukuliwa kwa mbunge huyo.

Zipo tetesi kwamba endapo Gwajima ataendelea kuwa na “kiburi” chake, anaweza kufukuzwa uanachama, hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge – nafasi ambayo aliipata kwa nguvu za dola, si kwa kura za wananchi.

Kuhusu Humphrey Polepole, ambaye naye amekuwa na msimamo kama wa Gwajima, Shaka alisema naye bado uchunguzi unaendelea kuhusu namna wanavyokipinga chama na serikali yake na kwamba wakikamilisha kazi hiyo, watachukua hatua kali.

“Ndani ya CCM hakuna mtu mwenye mapembe wala ukubwa kuliko chama chenyewe, lazima atakayethibitika yuko kinyume na msimamo wa chama na serikali yake, ataadhibiwa kwa mujibu wa taratibu zetu,” alionya Shaka.

Pamoja na CCM kuamua kumhoji Askofu Gwajima, leo serikali imesema msimamo wa kiongozi huyo wa kidini ni kupotosha umma na haielewi ana nia gani.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Gwodin Mollel amesema “Gwajima sasa anavuka mipaka, anapotosha taifa na kuogopesha wananchi juu ya usalama wa chanjo dhidi ya COVID-19.

“Gwajima anakosea na anapotosha sana, hawezi kupingana na serikali bila uhibitisho wa kisayansi, lazima aitwe na ahojiwe ili athibitishe, akishindwa tutamshughulikia,” alionya daktari huyo mtaalamu wa kinywa na meno. Hata hivyo, hakueleza ni namna gani watamshughulikia.

Askofu Gwajima amekuwa na msimamo wa kupinga chanjo kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania hayati John Magufuli, ambaye siyo tu kwamba alisema Tanzania haina maambukizi ya Corona – baada ya Mungu kujibu maombi ya kuifurusha, bali alisema hadharani “haya ma-chajochajo, ni biashara tu za Wazungu, yana madhara makubwa zaidi kuliko kuponya wala kuzuia.”

Wakati chama kikisema hivyo, Waziri wa Afya Dorothy Gwajima naye amepigilia msumari dhidi ya Askofu Gwajima akiagiza vyombo vya dola vimchukulie hatua kwa kutuhumu viongozi wa serikali – hasa rais na waziri wa afya – kuwa wameleta chanjo kwa sababu wamehongwa pesa.

Kauli ya waziri imepokelewa kwa hisia mchanganyiko, huku wengine wakimuunga mkono waziri na wengine wakimuunga mkono ‘askofu.’

Rais Magufuli, baada ya kuwa amesisitiza kuwa Tanzania haina Corona, huku watu wakiendelea kuugua na wengine kufariki dunia, alizuia kutangazwa kwa takwimu za ugonjwa huo Aprili 29, mwaka jana, huku akionekana ‘kituko’ mbele ya dunia kwa kupingana na sayansi. Magufuli alifariki dunia baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo Machi 17, mwaka huu.

Like
1