MGAWO wa umeme umeendelea kuathiri maisha ya Watanzania, ikiwemo mahitaji binafsi ya nishati hiyo katika ngazi ya familia, uzalishaji bidhaa na huduma, hali inayotishia hatma ya ukuaji uchumi wa taifa.
Huku uchumi wa duniani ukianza kuimarika baada ya mdororo uliosababishwa na ugonjwa wa UVIKO 19, Tanzania bado inajikongoja, huku ukosefu wa umeme ikiwa changamoto ya msingi, itakayosababisha nchi kutokwenda sambamba na wengine.
Kuanzia Novemba 15, 2021, mikoa 11 ya Tanzania inakosa umeme kwa saa 12 kutokana na matengenezo yanayofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Kidatu hadi Iringa, matengenezo yanayolenga kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika gridi ya Taifa.
Kwa miaka 30 sasa, upatikanaji wa umeme imeendelea kusuasua, kutokana na kupungua kwa uzalishaji kwenye vyanzo mbalimbali, hasa kupungua kwa maji kwenye mabwawa yanayozalisha nishati hiyo, ambayo yalikuwa chanzo kikuu cha umeme, kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwa sasa viwanda na shughuli mali vimeendelea kupunguza muda wa uzalishaji, huku gharama za uzalishaji kupanda, kutokana na matumizi ya umeme wa dharura.
Hali hii imechochea mfumuko wa bei za bidhaa, hasa zile za viwandani, pamoja na gharama za huduma kuendelea kuwa juu na kuumiza mifuko ya watanzania.
Ukosefu wa umeme pia umesababisha wajasiriamali wengi kufunga biashara kutokana na kutomudu umeme wa dharura, hali inayosababisha wengi wao kukosa fursa za ajira kwa ajili ya kujikimu.
Tatizo la umeme vilevile linasababisha kuchelewa na kudorora kwa utoaji wa huduma za msingi za jamii ikiwemo afya, elimu, usambazaji wa maji na sekta ya mawasiliano, ambavyo ni muhimu kwa maisha ya kila mtanzania.
Upungufu wa umeme pia umesababisha shule kushindwa kutumia vifaa vya kisasa vya elekroniki kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi.
Madhara haya kwa ujumla, yanapunguza ushiriki wa Watanzania katika kuzalisha mali, kupunguza kodi za serikali, ongezeko la bei kutokana na uhaba, ambavyo hudumaza ukuaji wa uchumi.
Wachumi mbalimbali wanasema kwamba, hali hii ikiendelea hadi robo ya kwanza ya mwaka ujao, ambayo ni robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2021/22, ukuaji wa uchumi utaathirika, huku Watanzania wakipoteza na kukosa ajira.
Pamoja na jitihada zote zilizofanywa tangu uhuru, uzalishaji wa umeme nchini umeendelea kuwa wa kiwango kidogo sana, ikilinganishwa na mahitaji halisi ya nchi, kuanzia kwenye ngazi ya familia hadi uzalishaji wa bidhaa na huduma.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba, wakati Tanzania inapata uhuru, uzalishaji wa umeme ulikuwa ni Megawati 67, ambazo zilitosheleza shughuli za uchumi wakati ule.
Matamanio makubwa ya awamu ya kwanza ilikuwa ni kuwa na umeme wa uhakika wa maji, ambao ni bei nafuu, ikizingatiwa kwamba rasilimali za maji zilikuwa nyingi.
Wakati huo, mradi wa umeme wa maji ulifikiriwa, lakini inawezekana haukuwa kipaumbele, ama sababu za kimazingira, au kwa sababu ya uwezo mdogo wa serikali kutekeleza mradi huo, miaka michache baada ya kutangazwa kwa azimio la Arusha.
Awamu zilizofuata ziliendelea na harakati, hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 nchi ilipoingia kwenye mfumo wa soko huria, na kushirikisha wazalishaji binafsi.
Kuanzia mwaka 1994, sekta ya umeme ilianza kupokea wazalishaji umeme wa binafsi, japokuwa mikataba mingi iliingiwa kwa taratibu ambazo si shirikishi na imeendelea kutesa taifa.
Hadi mwaka jana, inakadiriwa kuwa uzalishaji wa umeme kwenye gridi ya taifa ulikuwa Megawatt 1,573.7, kutoka MW 1,366.0 mwaka 2016, huku mahitaji kwenye grid yalikuwa MW 1,180 mwaka 2020 kutoka MW1,041.6 mwaka 2016.
Kiwango hiki ni chini ya matarajio ya sera ya nishati, ambayo ilikadiria kuwa hadi kufikia 2020, Tanzania ingekuwa ikizalisha si chini ya megawati 5,000 za umeme kwenye grid ya taifa, hasa baada ya ugunduzi wa gesi asilia kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Kwa mujibu wa sera ya kwanza ya nishati ya mwaka 2003, sekta hiyo ilikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kisheria, usimamizi na muundo wa kitaasisi.
Sera hiyo ilifanyiwa mapitio na serikali kuja hadi ikapatikana sera mpya ya nishati ya mwaka 2015 ambayo iligundua kwamba bado kuna upungufu mkubwa wa kushughulikia kwenye sekta ndogo ya umeme.
Upungufu huo, kwa mujibu wa sera ya mwaka 2015, ni ushiriki mdogo wa sekta binafsi katika kuzalisha kiwango kikubwa cha umeme, utegemezi kwenye vyanzo vichache vya kuzalisha nishati, utegemezi wa ruzuku ya serikali pamoja na ujuzi mdogo wa wahusika katika masuala ya nishati. Hayo yote yamechangia kudidimiza sekta hiyo.
Sera mpya ya mwaka 2015 inalenga kutengeneza mazingira mwafaka kwa ajili ya kuvutia wawekezaji binafsi katika sekta ya nishati.
Hatua hii inalenga kuhakikisha Tanzania inaenda sambamba na mpango wa dunia wa kuwa uhakika wa nishati kwa watu wote, kwa kuzingatia uhifadhi na ufanisi.
Kwa mujibu wa sera hiyo, hadi mwaka 2014, uwezo wa uzalishaji umeme ulikuwa ni Megawati 1,483, ikiwemo asilimia 28 toka vyanzo vya maji, asilimia 32 gesi asiliia na asilimia 30 ni mafuta.
Tanzania pia inanunua umeme kutoka nchi za nje – Megawati 5 kutoka Zambia, Megawati 10 kutoka Uganda, Megawati moja kutoka Kenya – kwa mujibu wa sera ya nishati 2015.
Mwaka 2014, wastani wa matumizi ya umeme kwa Mtanzania yalikuwa 105 kWh, kiwango ambacho ni cha chini kabisa kinapolinganishwa na kiwango cha 500kWh cha dunia.
Malengo ya sera hiyo pia ni kuhakikisha ongezeko la matumizi rasilimali za ya nishati jadidifu, ili kuongeza uzalishaji wa umeme.
Lengo jingine la sera hiyo ni kuhakikisha ongezeko la sekta binafsi katika kuzalisha na kusambaza umeme.
Mabadiliko ya uongozi
Hata hivyo, baada ya miezi kadhaa baada ya kupitishwa kwa sera ya nishati, yalifanyika mabadiliko ya uongozi wa nchi kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Baada ya kuingia madarakani, serikali ya awamu ya tano, ikiongozwa na Rais John Magufuli, ilibadili mwelekeo wa sera ya nishati, hasa umeme.
Hatua ya kwanza iliyofanya ni kuhakikisha kwamba inaondoa wazalishaji binafsi wa umeme, kinyume cha sera ya mwaka 2015, ikidaiwa kwamba mikataba yao ni ya kinyonyaji na imeingiwa kimakosa.
Hatua ya serikali kuvunja mikataba kumeingiza serikali katika msukosuko wa kisheria, hasa baada ya wawekezaji kuishitaki na kuishinda. Mfano mzuri wawekezaji waliovunjiwa mkataba na wakaishinda serikali ni Symbion – ingawa jambo hili lilifanyika kwa usiri mkubwa.
Hata hivyo, serikali iliendelea kutunga sheria zinazokinzana na matakwa ya sera ya mwaka 2015, ambazo zinazuia ushiriki wa sekta binafsi katika kuzalisha na kusambaza umeme.
Wataalamu wanasema kwamba utekelezaji wa sheria zinazosimamia umeme ziliwekwa kando miaka mitano iliyopita. Kwa mfano, sheria ya umeme ya mwaka 2008 haikuzingatiwa.
Baada ya miaka michache, wazalishaji binafsi wa umeme walifunga virago vyao, na kufurushwa, huku uzalishaji na usambazaji ukiendelea kufanywa na shirika la umma, kutumia vyanzo vile vile, ukiondoa vya sekta binafsi ambavyo vingine vilifungwa.
Serikali ya awamu ya tano pia ilikataa katakata kupanua mradi wa umeme wa gesi asilia, ambao bomba la kusafirisha gesi hiyo kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam, ambako kuna mitambo ya kuzalisha gesi asilia, lilijengwa kwa mkopo wa dola bilioni 1.2 kutoka Benki ya Exim nchini China.
Deni hilo ambalo hadi leo halijamalizika kulipwa, linaendelea kulipwa kupitia vyanzo vingine, pamoja na kuwa na mradi kuwa na uwezo wa kuzalisha mapato ya kulipa deni.
Kwa mujibu wa takwimu, matumizi ya bomba hilo kwa sasa ni asilimia 6, huku asilimia 94 zikiwa hazitumiki, ambayo wataalamu wanasema ni hasara kubwa kwa taifa.
Wataalamu wanadai kwamba iwapo bomba hilo lingetumika kwa uwezo wake kwa asilimia 50 tu, lingesaidia kuongeza umeme wa uhakika, ikilinganisha na vyanzo vingine kama maji, ambavyo mabadiliko tabia nchi, yafanya visiamikine.
Tanzania inakadiriwa kuwa na akiba ya gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 57, rasilimali ambayo inaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 50 ijayo, ikiwa na uwezo wa kuzalisha umeme na nishati ya gesi kwa ajili ya majumbani.
Mradi wa Umeme wa Maji Rufiji
Baadaye, serikali ya awamu ya tano ikaanza mchakato wa ujenzi wa Bwana la Julius Nyerere katika eneo la pori la akiba la Selous, wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3, kwa kutimia fedha za ndani.
Hata katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni moja kwa ajili ya mradi huo, pamoja na miradi midogomidogo ya umeme vijijini.
Imeelezwa na wachambuzi kwamba, kiasi hicho cha fedha kingeelekezwa kwenye kujenga miradi ya umeme wa kutumia gesi asilia, basi Tanzania ingekuwa na umeme wa uhakika zaidi.
Pamoja na kupigiwa kelele na wanaharakati wa mazingira na wataalamu wa masuala ya nishati, kuhusu athari za kimazingira na kibinadamu zitakazotokana na ujenzi bwawa hilo, serikali iliendelea kutekeleza mradi huo, ambao hivi karibuni bwawa litajazwa maji.
Bwawa hilo, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,100, limeanza kupata changamoto za ukame, hali inayoleta hofu, iwapo malengo ya mradi huo yatafanikiwa.
Pamoja na dunia kuonya kuhusu miradi ya umeme wa maji, ikizingatiwa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, Tanzania imeendelea kutekeleza mradi huo kwa kutumia tathmini ya mazingira iliyofanywa miaka hamsini iliyopita.
Hata tathmini ya mazingira ya mradi huo, ilifanywa mwaka 1970, na haiwezi kutoa tafsiri halisi ya ya athari zake au kuathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Wachambuzi wa masuala ya nishati wanasema tathmini za mazingira mradi wa Julius Nyerere Hydro Power (JNHPP) haielezei athari hasi kwa jamii na mazingira kwani hakuna vielelezo vya kutosha vya utekelezaji, vielelezo hafifu kuhusu mtiririko, matarajio ya mtiririko wa maji kwa kila majira ya mwaka na haujaonyesha ni namna gani utashighulikia iwapo utaathiri maisha ya watu wanaioshi karibu na mradi huo.
Pia, tathmini ya mradi huo pia haijaonyesha namna ya kushughulikia upotevu kwenye vijito vya asili na mchanga, upotevu wa miti ya asili kwenye eneo hilo, ikizingatiwa eneo hilo ni kati ya maeneo ya urithi wa dunia.
Mbali na athari kwenye pori la akiba la Selous, mradi huo utaathiri maisha ya wakazi ambao wanategemea maisha yao kwenye mto Rufiji ikiwemo uvuvi na kilimo, kutokana na kupungua kwa maji ambayo yanaelekea kwenye bwawa hilo.
Pia, athari zingine ni kuathiri akolojia ya maji, hasa samaki wanaohamahama mto Rufiji na bonde la mto Kilombero, Mafia na maeneo ya Kilwa.
Waziri wa zamani wa nishati Profesa Sospeter Muhongo, alikaririwa na gazeti la Mwananchi kuwa umeme uliopo nchini ni mdogo, na Tanzania inahitaji zaidi ya megawati 10,000 kwa miaka mitano ijayo, kwa ajili ya kufanikisha matumizi yake ya ndani na kuuza nje ya nchi, kama ilivyopanga kulingana na vyanzo ilivyonavyo.
“Kila siku nasikia mnaimba suala la umeme wa maji, lakini mtu anayejua masuala ya umeme, umeme wa maji kukupatia faida ni lazima uwe umewekeza fedha nyingi na inahitaji miaka mingi kurejesha gharama za uwekezaji ili umeme uwe wa bei nafuu,’ Profesa Muhongo alinukuliwa na Mwananchi akisema .
Alisema umeme wa maji bei yake haipungui baada ya kumaliza ujenzi wa bwawa, isipokuwa kwa mtu ambaye hataki kurudisha fedha za uwekezaji.
Alisema ni muhimu kuwa na mchanganyiko wa vyanzo vya uzalishaji wa nishati, kwa kuwa kuna matarajio kuwa bara la Afrika linaweza kukumbwa na ukame, hivyo kama njia ya kujiandaa na hali hiyo, alisema ni vyema kukawa na uzalishaji wa umeme unaotokana na maji, gesi asili, upepo, jua, jotoardhi na bayomasi.
WWF na Unesco katika ripoti yake walidai mradi huu utasababisha kukauka kwa vyanzo vya maji ndani ya mto rufiji ambayo hutegemewa na wanyama kwenye pori la akiba Selous, na nje ya pori hilo hivyo kuathiri sekta ya utalii.
Pia wanadai mradi huu utapelekea kupungua kwa rutuba katika ardhi na mazingira ya delta ya mto rufiji hivyo kuathiri kilimo.
Wadau hao wa mazingira na ekolojia walidai pia mradi huu utasababisha kupungua kwa samaki hasa wale aina ya “Kambakochi” na wengine wanaopatikana eneo hili hivyo kuathiri maisha ya wananchi wengi wanaopakana na eneo hili.
Pia walidai mradi huu utapelekea mmomonyoko mkubwa wa ardhi ambao ni hatari kwa mazingira ya eneo hilo.
Tuendako
Pamoja na hayo yote, Tanzania bado ina uhakika wa jua, joto ardhi na upepo, ambayo ni maeneo mengine Tanzania inatakiwa kuweka nguvu zaidi kuzalisha umeme wa uhakika zaidi, kuliko kutegemea umeme wa maji.
Takwimu zinaonyesha mchango wa sekta ndogo ya umeme umendelea kupungua kwa kasi kubwa toka mwaka 2015 hadi 2020 kwenye pato la taifa pia.
Kwa mujibu wa ripoti za ofisi ya Taifa ya Takwimu, mchango wa sekta ndogo ya umeme kwenye pato la Taifa, kwa bei ya sasa, umepungua kutoka shilingi bilioni 798.8 billion mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 398 mwaka 2020.
Ufanisi mdogo wa Tanesco
Shirika la Umeme Tanesco, ambalo ndilo mzalishaji na msambazaji bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimfumo na kiufundi
Machi mwaka huu aliyekuwa waziri wa nishati Dk Medard Kalemani alikaririwa shirika la harari Ujerumani akizilaumu Tanesco na kampuni ya Songas kuwa chanzo cha kero za mgao wa umeme.
Waziri huyo azitupia lawama mamlaka hizo kwa kuchukua muda mrefu kuifainyia ukarabati baadhi ya miundombinu yake hali inayosababisha sehemu nyingi kuendelea kupata umeme wa mgao.
Shirika hilo ambalo lina rasilimali za thamani ya shilingi trilioni 18, linazalisha mapato ya shilingi trilioni 1.8 kwa mwaka, lakini fedha hizo zote zinaenda kwenye gharama za uendeshaji.
Kwa miaka mingi shirika hilo limekuwa likiripoti hasara ya mabilioni kila mwaka, lakini limeendelea kupewa ruzuku ya serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji, ambayo mingi inadaiwa kuwa ni chakavu.
Baada ya kuteuliwa kuwa waziri wa Nishati, January Makamba alianza kufanya mageuzi mbalimbali, ikiwemo kuunda upya bodi na kuteua mkurugenzi mpya wa Tanesco.
Wengi wamekuwa na matumaini makubwa na uongozi mpya wa Tanesco, lakini matumaini haya yanaweza kuwa hewa, kwani mabadiliko ya uongozi pekee hayatasaidia ufanisi wa Tanesco.
Hata hivyo, waziri huyo mpya wa nishati, bado hajatoa mwelekeo halisi wa sekta ya umeme.