Zitto atikisa bunge kwa hotuba nzito juu ya mauaji ya raia Kibiti

ZITTO Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini, amesema zaidi ya Watanzania 380 wa Kibiti wamepotezwa katika mazingira yenye utata, na ametuhumu serikali kwa uhalifu huo. Kwa sababu hiyo, ametaka Bunge lunde time maalumu ya kuchunguza mauaji hayo kama lilivyofanya kwenye “Operesheni Tokomeza.”I fuatayo ni sehemu ya tatu ya hotuba yake bungeni leo akijadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Mwaka 2018/19:

Mheshimiwa Spika

Juni 12, 2017 mchana, Bi Ziada Salum wa Kitongoji cha Maparoni wilayani Kibiti alikuwa nyumbani kwake akipika chakula cha familia yake, wakati ambao Jeshi la Polisi lilifika na kumchukua kwaajili ya kwenda kumhoji. Ni miezi 11 leo tangu bi Ziada Salum achukuliwe, hajarudishwa mpaka leo, familia yake haijaarifiwa chochote, bado imekaa na matarijio kuwa ipo siku atarudi.

Mwezi huo wa Juni 2017, si Bi Ziada tu aliyechukuliwa na kutokurudishwa mpaka leo, kwa staili ya namna hiyo ni wengi mno. Wakiwemo kinamama wa familia moja, Rukia Muhohi na Tatu Muhohi wa Kitongoji cha Msala, hapo hapo wilayani Kibiti, wao wakichukuliwa kwenda kuhojiwa na Jeshi la Polisi Juni 26, 2017, na mpaka leo hawajarudishwa. Kaka yao Nassoro Muhohi yeye alichukuliwa Juni 27, 2017, kisha kuachiwa (najua kwa kumtaja hapa Bungeni anaweza kuchukuliwa tena na mara hii kupotea kabisa).

Kitongoji hiki cha Msala kimewapoteza wengi, akiwemo Jumanne Rashid Pango, aliyechukuliwa naye siku moja pamoja na Rukia na Tatu Muhohi. Ni miezi zaidi ya 10 leo, watu hawa wote Jeshi la Polisi halijawarudisha, lakini pia halijatoa maelezo yoyote kwa ndugu zao juu ya walipo na lini watawarudisha.

Kina Muhohi sio ndugu pekee waliochukuliwa na Jeshi letu la Polisi na kutokurudishwa mpaka leo, katika Kata ya Mjawa wilayani Kibiti ndugu watatu wa familia moja nao walichukuliwa Juni 2, 2017, hao ni Hamisi Omari Nyumba, mwanawe, Sadam Hamisi Nyumba pamoja na nduguye, Juma Omari Nyumba. Nao Jeshi la Polisi limebaki nao mpaka leo, halijawarudisha, hatujui kama bado wako hai ama ni sehemu ya miili inayookotwa kwenye fukwe zetu.

Si hao tu, Julai 10, 2017, katika Kitongoji cha Nyantimba, wilayani Rufiji, Jeshi la Polisi liliwachukua watu watatu, bwana Hamisi Mketo, Bi Tabia Nyarwamba na Bi Pili Mkali, nao wakielezwa wanakwenda kuhojiwa, kama ilivyo kwa hao wengine, nao hawajarudishwa mpaka leo, zaidi ya miezi 9 sasa. Orodha niliyonayo Hapa ni kadhia 68 za namna hii, kadhia 62 zikiwa nimezithibitisha, na kadhia 8 nikiwa naendelea na uchunguzi. Kwa sababu ya muda niishie kutaja hao tu.

Kadhia za namna hii ni nyingi mno, na yeyote kati yetu, akipata wasaa tu wa kwenda MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji) ataelezwa mambo haya kwa undani, makadirio ni kuwa zipo kesi zaidi ya 380 za namna hii za watu kuchukuliwa na kutorudishwa kwa zaidi ya miezi 10 sasa, hizo ni tofauti na zile za watu waliokamatwa, kuteswa na kisha kuachiwa, au wale waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi.

Na si MKIRU tu, bali ukanda wote wa Kusini, wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Kilwa Kusini, mheshimiwa Suleiman Bungara ‘Bwege’ (CUF) naye alieleza kadhia za watu 10 wa Jimboni kwake Kilwa, kuchukuliwa Msikitini na Jeshi letu la Polisi, kupigwa risasi, wengine kutokurudishwa mpaka leo, na kuhisiwa kuwa wameuawa, wengine kurudishwa wakiwa na vilema vya kukatwa masikio, kuchomwa ndevu kwa moto nk.

Najua haja ya kudhibiti hali mbaya ya usalama iliyojitokeza mwaka jana. Mauaji yale ya Askari Polisi na raia yaliyokuwa yakiendelea MKIRU yalipaswa kukomeshwa, lakini bado ukomeshwaji husika ulipaswa kufanyika ndani ya utaratibu wa kisheria tuliojiwekea kama Taifa. Kwa haya yanayoripotiwa sasa kutoka MKIRU, ni dhahiri kuwa utaratibu wa kisheria ulikiukwa, haki za binaadam zilivunjwa, raia wema na wasio na hatia waliuawa na jeshi ambalo lilipaswa kuwalinda, na wananchi wengi wakiwa wamepotea tangu wachukuliwe kwenda kuhojiwa.

Mambo ya namna hii si mapya nchini mwetu, ya nia nzuri ya kudhibiti jambo baya, kutumika kuwaumiza wananchi. Mwaka 2013 Nchi yetu ilikumbwa na janga kubwa la Ujangili, tembo na faru wetu wakiuawa na magenge ya wahalifu. Kwa nia njema ya kudhibiti ujangili huo, Serikali kwa kutumia majeshi yetu, ilianzisha Operesheni ya kutokomeza Ujangili huo.

Kwa kipindi kifupi cha Operesheni husika, malalmiko juu ya wananchi kubakwa, kuteswa, kuuawa, kuporwa mali zao, na mengine mengi mabaya ya unyanyasaji wa raia yaliripotiwa. Unyanyasaji na ukiukwaji huo wa haki za binaadam kwa wananchi wetu uliripotiwa wilayani Babati mkoani Manyara, Tarime mkoani Mara, Kasulu mkoani Kigoma, Meatu mkoani Simiyu, Ulanga mkoani Morogoro, Urambo na Kailua mkoani Tabora, pamoja na maeneo mengine ya Nchi yetu.

Malalamiko ya wananchi yaliletwa hapa bungeni, Bunge letu lilichukua hatua juu ya mamaliko hayo, kwanza kwa kuitaka Serikali kusitisha Operesheni Tokomeza, na kisha kwa kuunda Kamati Teule ya Bunge, kuchunguza juu ya utekelezwaji wa Operesheni Tokomeza. Kamati Teule ilithibitisha ukweli wa madai ya wananchi kunyanyaswa, kuuawa, haki zao kubinywa nk. Na hatua kadhaa njema zilichukuliwa ili kurekebisha jambo hilo.

Malalamiko ya MKIRU ni makubwa mno, Unyama unaoripotiwa kufanywa huko na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama hata hauelezeki, umehusisha kupotezwa kwa watoto, kinamama na wazee, haukujali jinsia wala rika, kadhia chache nilizozielezea hapa zimeonyesha taswira ya maumivu na ukubwa wa jambo hilo, zaidi taarifa juu ya kupotea kwa zaidi ya watu zaidi ya 380 zikishtusha na kuamsha hisia.

Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa mwaka 1987, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo; “Panapokuwa hapana Haki, wala Imani na Matumaini ya kupata Haki, hapawezi kuwa na Amani wala Utulivu wa kisiasa. Hatima yake patazuka fujo, utengano na mapambano”.

Watu hawa wa MKIRU na kusini kwa ujumla ni ndugu zetu, ni Kaka na Dada zetu, ni Watanzania wenzetu ambao tuko humu Bungeni kuwawakilisha. Unyama huu unaosemwa kufanywa dhidi yao umewaondolea kabisa HAKI yao ya Uhai, umewaondolea IMANI ya kupata Ulinzi wa Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, Bunge letu lichunguze jambo hili kuwapa MATUMAINI ya kupata Haki, ili wasibaki na vinyongo, na ili wasichague fujo, utengano na mapambano kama njia ya kuponya majeraha yao na kudai Haki zao zilizominywa. Sisi Bunge tunao wajibu huo.

Kwahivyo basi, kwa maelezo hayo niliyoyatoa, kwa mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, naomba kutoa Taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu kadhia za Mauaji, Kupotea, Kupigwa Risasi, Kuteswa watu wa MKIRU na Kusini kwa ujumla.

Ni imani yangu kuwa Wabunge wenzangu mtaunga mkono jambo hili.

Naomba kuwasilisha

Katika chapisho jingine, SAUTI KUBWA inakuletea orodha ya waathirika 68 wa kwanza kama alivyosema Zitto.

Like
1
3 Comments
 1. Amani 6 years ago
  Reply

  Nchi inaelekea wapi?Bwana mkubwa hataki kusikia hayo aanapenda kuogopwa lakini madaraka yana mwisho,Pia watu wamechefukwa sana hata huku vijijini

  1

  0
 2. Kakakuona 6 years ago
  Reply

  When dictatorship is a fact, revolution becomes a right.
  #kakakuona#nchiyaahadi#

  0

  0
 3. Mmbogo, Steven 6 years ago
  Reply

  Haki haiwezi kudhulumiwa…..

  0

  0

Leave a Comment

Your email address will not be published.