Zitto asema udikteta, uendeshaji mbovu wa uchumi vimeporomosha shilingi

Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amefanya uchambuzi unaoonyesha kuwa shilingi ya Tanzania inaporomoka thamani kwa sababu ya uendeshaji Mbovu wa Uchumi na ubinywaji wa demokrasia. 
Thamani ya sarafu yetu ya Tanzania imezidi kuporomoka kwa kasi dhidi ya Dola ya Marekani katika wiki za hivi karibuni. Mwisho ni mwa wiki jana dola moja imeuzwa mpaka shs 2415, mporomoko wa karibia 15% kulinganisha na thamani ya Dola mwezi January Mwaka 2018. Kwa maoni yangu, Watanzania wanapaswa kujua kuwa Haya ni matokeo ya Mambo 2 makubwa.
Moja, maamuzi ya hovyo Kuhusu Zao la Korosho ambalo ni zao kiongozi katika kuleta fedha za Kigeni. Kutokana na maamuzi ya Serikali ya kutaka sifa za muda mfupi za kisiasa, mwaka 2018 Tanzania haikuuza Korosho nje ya nchi kutoka msimu wa 2018/19. Pia kitendo cha Serikali kuingia mkataba na kampuni ya kitapeli kutoka Kenya ili kununua Korosho kumesababisha Tanzania kuchelewa kuwahi soko kabla ya msimu ambao nchi za Nigeria, Guinea Bissau, Benin, Ivory Coast na Indonesia wanaingiza Korosho zao kwenye soko la dunia. Hasara ya Korosho itafikia shs trilioni moja na zaidi;
Mbili ni ubinywaji wa Demokrasia kwa kuporwa kwa ushindi wa Chama cha CUF Uchaguzi wa Zanzibar Mwaka 2025, kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, kuwabambikia kesi wanasiasa wa upinzani ikiwemo kupigwa risasi Tundu Lissu na Kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa hivyo kupelekea wafadhili kutoleta fedha za kigeni nchini. Haya pamoja na mambo mengine ya ukandamizwaji wa haki za binadam kumesababisha mahusiano ya Tanzania na nchi wafadhili na hata mashirika ya kimataifa kudorora. Nchi nyingi hazijafuta misaada bali zimechelewesha kutoa fedha za kusaidia bajeti yetu ya Maendeleo.
Nini matokeo ya Hali hii? 
Serikali itashindwa kulipa wakandarasi wa miradi yake mikubwa au kama ikiwalipa basi ita ‘default’ malipo ya madeni yaliyowiva au kuchelewesha mishahara ya watumishi wa umma. Mwaka 2019 kiwango cha fedha zinazotumika kuhudumia deni la Taifa kimeongezeka sana kwa sababu madeni kadhaa yamewiva na pia Serikali ya Rais Magufuli inachukua mikopo mingi kutoka Benki za Biashara na muda wa kulipa unakuwa mfupi sana. Kwa miaka 2 sasa mikopo ya kuendesha Bajeti inatoka Benki kama HSBC, CreditSuisse na mabenki mengine ya Nje yenye riba kubwa na kutukopesha kwa fedha za kigeni.
Serikali itafanya nini? Nionavyo, Kwa kuwa Serikali hii ni kiburi itaamua kuendelea kukopa kutoka benki za nje kwa fedha za kigeni ili kuficha aibu kwa Wananchi na hivyo kuingiza nchi kwenye madhara makubwa zaidi. Gharama za kuhudumia deni ( debt services) litakuwa kubwa kiasi cha Serikali kushindwa kutoa fedha kwa matumizi mengine kama vile Elimu na Afya.
Kwa upande  wa Sekta binafsi, ununuzi wa malighafi za viwanda itakuwa ghali zaidi kwa sababu malighafi nyingi zinatoka nje ya nchi. Matokeo yake bei ya bidhaa za Viwanda itapanda Sana. Wananchi watatumia shilingi nyingi zaidi kununua bidhaa ile ile waliyokuwa wakinunua kwa bei ndogo wakati sarafu yetu Ina nguvu sokoni. Tayari Wafanyabiashara Katika sekta binafsi wameanza kuhangaika kupata fedha za kigeni maana hazipatikani sokoni. Sekta binafsi itajikuta inafunga Biashara na kusababisha watu wengi kukosa Ajira.
Ushauri wangu?
Serikali ikubali uchunguzi huru wa shambulio la Tundu Lissu na kuachia vyama vya Siasa Kuwa huru kufanya siasa ikiwemo kufuta kesi zote za kisiasa dhidi ya wanasiasa wapinzani. Muhimu zaidi Rais kama Mkuu wa Nchi aombe kikao na Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF, kupata suluhisho la haki ya Wazanzibari kupata Serikali waliyoichagua Oktoba 25, 2015. Ikishafanya Hivi Serikali iwaombe baadhi ya wanasiasa kwenda kwa Donors kuomba waachie fedha za misaada walizozizua kwa sababu ya kupinga ubinywaji wa Demokrasia nchini.
Pili Serikali iache kubana Sekta binafsi ili uwekezaji uje nchini na kuongeza ‘inflows’ za fedha za kigeni. Tangu Serikali ya awamu ya 5 iingie madarakani mitaji kutoka nje imeshuka kutoka 5% ya Pato la Taifa Mwaka 2015 mpaka 2% ya Pato la Taifa Mwaka 2018. Sio hali nzuri hata kidogo.
Pia Mabadiliko makubwa yafanyike Wizara ya Fedha na Benki Kuu ili kuweza kutekeleza sera bora za Uchumi na Rais amwombe Prof. Ndulu kuwa Mshauri Mkuu wa Uchumi kwa angalau mwaka mmoja. Namna Hazina yetu inavyosimamiwa ni simanzi kubwa sana.
Najua Rais magufuli hatafanya Haya licha ya yeye mwenyewe kujua hali ni mbaya sana kiuchumi. Akiendelea na sera zake, mtaniambia dola imefika ngapi tarehe kama hii mwezi machi. Wananchi wanashuhudia hali mbaya ya maisha yao sio kwa sababu ya kinachoitwa vita ya Uchumi, bali ni kwa sababu ya uendeshaji mbovu wa Uchumi hususan kutokana na watawala tuliowakabidhi  kuendesha Uchumi wetu kukosa MAARIFA ya namna Uchumi wa kisasa unapaswa kuendeshwa.
Like
9

Leave a Comment

Your email address will not be published.