Musiba ashindwa kuwasilisha utetezi dhidi ya Membe mahakamani

KESI ya madai kati ya Bernard Membe na Cyprian Musiba iliitwa jana tarehe 26 Februari 2019 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini mdaiwa – Msiba – alishindwa kuwasilisha majibu ya utetezi kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Membe, amewahi kuwa waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa. Musiba ni raia ambaye amejitokeza kuwa msemaji asiye rasmi wa Rais John Magufuli anayetumia ukaribu wake na Ikulu kushambulia au kutisha watu wanaokosoa au wanaopinga baadhi ya mipango ya Rais Magufuli.

Kwa kukosa hati ya utetezi jana mahakamani, mawakili wake walipewa muda wa nyongeza waiwasilishe tarehe 28 Machi 2019 – nje ya muda wa kisheria (siku 21) waliokuwa wamepewa.

Musiba anashitakiwa kwa kutoa matusi dhidi ya Membe na kumtuhumu kuwa anamhujumu Rais Magufuli, na kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020. Kwa mujibu wa Musiba, ambaye amekuwa anaropoka kila mara katika utetezi wake kwa rais, mipango ya Membe ni sawa na uhaini.
Membe alikuwa mshindani wa Magufuli katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM mwaka 2015. Jina lake lilikwama katika ngazi ya halmashauri kuu ya CCM.

Kwa mara ya kwanza kesi yao iliitwa jana tarehe 26 Februari 2019, lakini Musiba na Membe hawakutokea mahakamani. Waliwakilishwa na mawakili wao. Hadi leo Membe yupo nje ya nchi, lakini anatarajiwa kuwa amerejea Tanzania Machi 28 ili afike mahakamani.

Musiba yupo Tanzania lakini hakufika mahakamani. Taarifa ambazo SAUTI KUBWA ilizipata ni kwamba Musiba amekuwa anakwepa kupokea wito wa kimahakama tangu Membe alipofungua shauri hili Desemba mwaka jana.

Madalali wa mahakama walipata wakati mgumu kufikisha wito kwa Musiba, kwani kila alipopelekewa wito ofisini kwake, yalitengenezwa mazingira ya kutopokea wito huo. Kwanza, alikuwa hapatikani hata kwa namba zake za simu. Hata mhariri wa gazeti lake, ambaye ni mmoja wadaiwa, na awali alikuwa amepokea barua ya madai, aligoma kuupokea wito wa mahakama zaidi ya mara tatu.

Ndani ya mwezi mmoja uliopita, hata ofisini kwake alikuwa anafika kwa machale au hafiki kabisa, kwani ofisi zake zilizopo Mwananyamala kwa Kopa zimekuwa zinakutwa zimefungwa. Hata katika Tanzanite House jirani na Mlimani City, mara nyingi amekutwa mlinzi pekee.

Katika ofisi za magazeti Kijitonyama jirani na kituo cha Polisi cha Mabatini nako hakupatikana, na waliokutwa mle waligoma kupokea wito huo. Zaidi ya hayo, mwanzoni mwa Septemba 2018 wenzake na Musiba walitoa tangazo kuwa yeye si mkurugenzi wa CZ Information and Media Consulting, lakini baada ya hapo amekuwa ananukuliwa kwa cheo hicho akijiita mmiliki wa magazeti yale yale.

Hatimaye, alifikishiwa wito huo kwa njia ya EMS, mwishoni mwa Januari. Kwa kawaida, alitakiwa kujibu madai dhidi yake ndani ya siku 21 tangu alipopokea wito huo, lakini hadi jana shauri linaitwa mahakamani, mawakili wake walikuwa hawajajibu madai ya mlalamikaji.

Watu wa karibu na Musiba wanasema shauri hili limemkalia vibaya, hana majibu, kwani tuhuma zake dhidi ya Membe zilikuwa za kutunga, kama ambavyo amekuwa anafanya dhidi ya wengine. Vile vile, habari hizo zinasema Musiba ameshauriwa na “watu wazito” amtafute Membe na kuomba shauri liishie nje ya mahakama. Bado hajafanikiwa.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati kesi hiyo inaitwa jana, majina ya ubini ya Membe na Musiba hayakutajwa. Mleta maombi aliitwa Bernard Kamillius na mdaiwa aliitwa Cyprian Majura.

Shauri hili lina uzito wa kisiasa. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Bashiru Ally, aliwahi kubeba tuhuma za Musiba na kumtaka Membe ajisalimishe na kujitetea ofisini kwake. Kauli yake iliibua mjadala mkali. Baadaye Bashiru alinyamazia suala hilo, akapuuza hata ujumbe wa  Membe aliyeomba miadi ya kukutana naye rasmi ofisini.

Kwa ulinzi wa kiserikali anaopewa Musiba, na kwa katibu mkuu wa CCM kuunga mkono tuhuma zake, shauri hili linachomoza kama shauri la Membe dhidi ya wakubwa katika chama chake, hasa kwa kuwa tayari imebainika Musiba anasema yale anayokuwa ameagiza kusema.

Katika shauri hilo, Membe anawakilishwa na kampuni ya Millennium Law Chambers ya Dar es Salaam. Mawakili wa Musiba waliofika mahakamani jana ni Hamza Jabir na Hosea Chamba.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Like
8

Leave a Comment

Your email address will not be published.